MKURUGENZI WA VETA NYANDA ZA JUU ATEMBELEA HOSPITALI YA PERAMIHO MJINI SONGEA

Mkurugenzi wa VETA nyanda za juu,Monica Mbele akiangalia moja ya darubini katika karakana ya vifaa tiba kwenye Hospitali ya St. Joseph Peramiho,wengine ni fundi mkuu wa karakana hiyo Baraka Chumbwi kushoto na katikati kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Benedict Ngaiza.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya elimu na mafunzo (VETA) nyanda za juu,Monica Mbele akiangalia moja ya vifaa tiba vilivyoharibika katika karakana ya Hospitali ya St Joseph Peramiho,Songea vijijini.VETA ina tarajia kufundisha wataalam na mafundi wa hospitali mbalimbali kutengeza vifaa vilivyoharibika ambapo itasaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kwa kuagiza au kuleta mafundi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya ukarabati wa vifaa hivyo.
Mkurugenzi wa VETA nyanda za juu,Monica Mbele akiangalia mshine ya kufuria nguo ambayo imeharibika.
Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma (homso) Dkt Benedict Ngaiza kulia na mkurugenzi wa VETA nyanda za juu,Monica Mbele wa pili kulia wakiangalia kiti kinachotumika kwa ajili ya shughuli za upasuaji katika hospitali ya St Joseph Peramiho jana.
Fundi mkuu wa karakana ya vifaa tiba katika hospitali ya st Joseph Peramiho Baraka Chumbwiakionesha mojawapo ya mshine ya kupiga picha kwa wataalam na mafundi kutoka chuo cha veta Songea,mafundi kutoka hospitali ya mkoa Ruvuma na ujumbe wa mamlaka ya elimu na mafunzo(veta)nyanda za juu ukiongozwa na mkurugenzi wake Monica Mbele.
PICHA NA MUHIDIN AMRI - GLOBU YA JAMII,RUVUMA.

Tatizo La Maji Songea Sasa Latikisa Ndoo moja Lita Sh 500







Mjengwa blog

Mafuta Yawa adimu Songea



Picha kwa hisani ya http://mwambije.blogspot.com/

HAFLA YA KUMUAGA KANAL MJENGWA DC MBINGA YAFANA SANA


Kutoka kushoto mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi,mkuu wa wilaya ya mbinga mstaafu Kanal Edmund Mjengwa,mkuu wa mkoa wa Ruvuma,Said Mwambungu,mkuu mpya wa wilaya Mbinga Senyi Ngaga na Mama Hanab Mwambungu wakigonga cheers wakati wa sherehe ya kumuaga Kanal Mjengwa jana mjini Mbinga.
Mkuu wa zamani wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Kanal mstaafu Edmund Mjengwa akizungumza jana mjini Mbinga wakati wa sherehe yake ya kumuaga,katikati mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu na kulia mkuu mpya wa wilaya hiyo Senyi Ngaga. 

Serikali Mkoani Ruvuma imetoa mwenzi mmoja kwa Wafugaji wa ng'ombe kuhama mkoani Ruvuma



kundi kubwa la ng'ombe katika poli la hifadhi ya selous
Serikali Mkoani Ruvuma imetoa mwenzi mmoja kwa Wafugaji wa jamii za Kisukuma na Wamang‘ati walioingiza Ng’ombe wao kiholela bila kufuata utaratibu kuondoka Mkoani humo vinginevyo Sheria itafuata mkondo wake ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa Oparesheni ya kuwafukuza.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Said thabity Mwambungu, wakati akiongea na Viongozi wa Serikali Wilayani Tunduru kutokana ukiukwaji wa taratibu za kuingiza wanyama hao bila kufuata taratibu hali ambayo inaweza kuleta madhala na kuzuka kwa mapigano makubwa baina ya wakulima na wafugaji.

Bw. Mwambungu akatumia nafasi hiyo kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Chander Nalicho na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bw.Albert Nehata kusimamia zoezi hilo na kuhakikisha kuwa Watendaji wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji, Maafisa tarafa kuhakikisha kuwa wanasimamia kwa nguvu zao zote utekelezaji wa tukio hilo na kwa kiongozi anaye jiona kuwa hata mudu basi aachie dhamana hiyo aliyopewa na Serikali.

Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ililidhia kupokea Ng’ombe elfu kumi tu (10,000) na wafuagaji hao kutengewa maeneo katika kata za Mhuwesi, Masonya na Ngapa lakini cha kushangaza wafugaji hao wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku na kuenea katika maeneo yote ya Wilaya hiyo.

Wanachi wa wilaya ya Tunduru wamelalamika kuona wafugaji hao kuendelea kuvamia hadi katika hifadhi ya Taifa ya Selous, na hifadhi zamapori tengefu amabazo hutumika katika bishara ya uwindishaji wa Kitaali zilizopo katika maeneo mbali mbali ya vijiji vilivyo Wilayani humo huku kukiwa na makatazo ya kuwazuwia wanachi kuingia na hata kulima.

Afisa Kilimo na Migfugo wa Wilaya ya Tunduru Bw. Chiza Malando mbali na kukiri kwa uingizaji holela wa mofugo hiyo alisema kuwa hivi sasa Wilaya ya Tunduru imeonekana kuelemewa na wingi wa mifugo hiyo,kwani hadi sasa Wilaya hiyo inakadiliwa kuwa na zaidi ya Ng’ombe 40,000 kutoka kwa wafugaji hao tofauti na malengo ya kuwa na Ng,ombe 10,000 

SHEIKH ASHAMBULIWA, AJERUHIWA ALAZWA HOSPITALINI, VIONGOZI WA UAMSHO KIZIMBANI




Na Mwinyi Sadallah

Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Waziri Ally Chilakwechi, amepigwa na watu wasiojulikana baada ya kumvamia nyumbani kwake eneo la Mchangani mjini Tunduru na kujeruhiwa vibaya. 

Sheikh Chilakwechi akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru alikolazwa, alisema alishambuliwa na watu wasiojulikana juzi.

Akielezea mkasa huo, alisema siku ya tukio alifuatwa na watu watatu majira ya saa 2:30 usiku nyumbani kwake wakidai kuwa kuna vurugu zimetokea katika msikiti wa Kitumbini eneo la Majengo, hivyo anahitajika kwenda kutuliza vurugu hizo.

Alisema kwa kuwa alikuwa hawatambui watu hao, isingekuwa vyema kwenda huko kutokana na umbali kwa kuwa kutoka nyumbani kwake hadi kwenye msikiti huo ni zaidi ya kilomita mbili.

Shekhe Chilakwechi alisema baada ya kuwajibu hivyo, watu hao walitoka nje na ghafla kundi jingine la watu lilimvamia kwa kumrushia mchanga usoni na kuanza kumshambulia  sehemu kadhaa za mwili.

Alisema wakati watu hao wakiendelea kumshambulia, mke wake alitoka nje na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani ambao walitoka na kuanza kuwakimbiza watu hao na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Rajabu Abdallah Likoto (17).

Shekhe huyo alisema mtu huyo alikamatwa baada ya kukwama kwenye matope wakati anavuka mto Mlingoti na alijeruhiwa kwa kukatwakatwa na mapanga. Mtuhumiwa huyo naye amelazwa katika hospitali hiyo.

MGANGA WA WILAYA ANENA

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, Dk. Fred  Wenandi,  akizungumzia tukio hilo, alisema Sheikh huyo amejeruhiwa vibaya usoni na amelazwa katika hospitali hiyo na anaendelea na matibabu.

KAULI  YA DC

Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho, alithibitisha taarifa za kupigwa kwa Sheikh huyo na kufafanua kuwa alimtembelea hospitalini kumjulia hali.

Nalicho alisema bado hazijafahamika sababu za kushambuliwa kwa Sheikh huyo na kwamba uchunguzi wa tukio hilo unafanywa na vyombo vya dola.

“Nilikuwa na Sheikh katika sherehe za miaka 50 ya Kanisa la Biblia zilizofanyika hivi karibuni wilayani hapa katika kuendeleza mahusiano na dini nyingine. Ni mtu anayependa mahusiano mazuri na dini nyingine, sifahamu sababu za kushambuliwa kwake,” alisema.

VIONGOZI WA UAMSHO KORTINI

Viongozi saba wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar jana wamefikishwa mahakamani na kusomewa shitaka la kufanya uchochezi na kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani, maafa, na mtafaruku dhidi ya Serikali.

Viongozi waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe ni kiongozi mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi Ahmed (41), mkazi wa Mbuyuni.

Wengine ni Sheikh Mselem Ali Mselem (52), mkazi wa Kwamtipura; Sheikh Mussa Juma Issa (37), mkazi wa Makadara; Sheikh Azzan Khalid Hamdan (43), mkazi wa Mfenesini; Suleiman Juma Suleiman (39), mkazi wa Makadara; Hassan Bakari Suleiman (39), mkazi wa Tomondo na Khamis Ali Suleiman.

ULINZI MKALI WA POLISI

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani majira ya saa 4:00 za asubuhi wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakisindikizwa na magari matatu yenye namba PT 873, PT 1159, PT 859 na gari walilokuwa wamepakizwa washitakiwa hao ni PT 1891.

Aidha, viongozi hao wa Uamsho walikuwa wamezungukwa na askari wasiopungua 10 katika kila gari moja, waliobeba bunduki aina ya SMG zisizopungua 25 mbali na mabomu ya machozi kama hatua za tahadhari kwa vurugu zozote endapo zingetokea katika viwanja vya Mahakama hiyo.

Ulinzi uliimarishwa katika eneo hilo la Mwanakwerekwe na askari wa Jeshi la Polisi na vikosi vya SMZ na kabla ya kuwasili kwa viongozi hao, wananchi wote waliojitokeza mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo waliamriwa kuondoka. Pia hatua zilichukuliwa za kuzuia watu kukatisha katika njia za eneo hilo.

Vile vile, maeneo ya shule nne zilizopo jirani na Mahakama ya Mwanakwerekwe wanafunzi wote walitakiwa kurejea majumbani kabla hata ya washitakiwa hawajafika kwa lengo la kuhakikisha eneo hilo linakuwa na utulivu.

Akiwasomea mashitaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Maulid Ame Mohamed, alidai kuwa viongozi hao wa Uamsho Agosti 17 majira ya saa 11:00 jioni, wanadaiwa kufanya makosa ya uchochezi na kufanya fujo kinyume na kifungu cha 45(10) (a) na (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004  ya mwenendo wa makosa ya Jinai ya Zanzibar.

Alidai kuwa watuhumiwa hao wakiwa katika Msikiti wa Magogoni Msumbiji, walitenda kosa la uchochezi na kusababisha uvunjifu wa amani, matukio ya vurugu, maafa na kusababisha mtafaruku dhidi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Baada ya kusomwa mashitaka dhidi yao, ulitokea mvutano mkali huku wakili wa upande wa utetezi, Abdallah Juma Mohamed, akitaka wateja wake waachiwe huru na kesi itupiliwe mbali kwa madai kuwa imefunguliwa kinyume na kifungu cha 45(1) (a) na (b) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Alidai kuwa sheria hiyo inasema hakuna mtu atakayefunguliwa mashtaka kabla ya kutolewa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka cha wahusika kufunguliwa kesi na kueleza kwa nini upande wa mshitaka haujaweka wazi juu ya kuwepo kwa kibali hicho mbele ya Mahakama.

“Mheshimiwa Hakimu, kesi zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, Mahakama isiingie katika mtego huu, washitakiwa hawapaswi kujibu mashitaka waliyosomewa kwa vile hakuna kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka,” alidai Abdallah Juma na kuongeza:

“Naamini Mahakama hii ipo kwa mujibu wa sheria, haiendeshi shughuli zake kama kesi za kwenye mwembe wala haipigi ramli wala bao katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo naomba wateja wangu waachiwe, labda kibali hicho kiwe kimepenyezwa mezani kwako sasa hivi,” aliiambia Mahakama.

Hata hivyo, hoja hiyo ilitupiliwa mbali baada ya kuthibitika kuwa taratibu za ufunguaji kesi zimefuatwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka kilikuwepo na Hakimu Msaraka Ame Pinja, alikionyesha na kuwataka washitakiwa kujibu mashitaka dhidi yao.

Hoja zilizoibuliwa na upande wa utetezi katika kesi hiyo, ni pamoja na ombi la kutaka kupatiwa hati ya mashitaka pamoja na haki ya dhamana kwa washitakiwa hao na jopo la mawakili watatu walielezea na kuvitaja vifungu na kuiomba Mahakama hiyo kupunguza masharti ya dhamana.

Waliyataja masharti hayo kuwa ni washitakiwa kudhaminiwa na wafanyakazi wa serikali, barua ya Sheha na kuangaliwa uwezo wa washitakiwa endapo watatikiwa kutoa fedha taslimu kwa ajili ya dhamana wakati hali zao za kiuchumi sio nzuri.

Wakili wa washitakiwa hao, Suleiman Salum, alidai kuwa ni vigumu kwa wafanyakazi wa serikali kujitokeza kuwawekea dhamana kutokana na woga na vile vile ofisi nyingi za masheha hivi sasa zimefungwa kwa kuwakomoa ndugu na jamaa wanaofuatilia kuwekewa dhamana jamaa zao wasifanikiwe kupata barua za kuwachukulia dhamana.

Alidai kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa kwa kuwa ofisi za masheha zimefungwa na wameacha magizo kuwa watakapouliziwa na mtu yeyote wajibiwe kuwa wamesafiri, jambo ambalo alidai linawanyima wateja wake haki ya kupata dhamana.

Hata hivyo, Mwanasheria wa Serikali, Maulid Ame Mohamed, alimtaka wakili huyo kuacha kuzungumza nadharia na badala yake kuonyesha ushahidi kuhusu madai yake ya dhamana ikiwamo masheha kufunga ofisi na watumishi wa umma kuogopa kuwawekea jamaa zao dhamana kwa sababu kesi hiyo imefunguliwa na mwajiri wao ambaye ni serikali.

“Hakuna chombo cha habari kilichowahi kuripoti kuwa ofisi za masheha zimefungwa, hivyo ni vyema akaonyesha ushahidi wa yote anayodai mbele ya mahakama,” alidai Mwanasheria huyo wa Serikali.

Baada ya mwanasheria huyo kutoa maelezo hayo, Wakili wa utetezi, Suleiman Salum, alidai kuwa wateja wake wana haki ya kupatiwa dhamana kwa vile ni watu wenye heshima na busara na hata polisi walikwenda wenyewe, lakini pia wamesaidia kwa kiwango kikubwa kupatikana kwa hali ya amani na utulivu miongoni mwa wafuasi wao.

Hoja hiyo ilisisitizwa na Abdallah Juma Mohamed, kwa kuileza mahakama hiyo kuwa Ibara ya 12 (1) (6) (a), inaeleza haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa Mahakama au chombo kingine kinachohusika.

Alidai kuwa ibara hiyo inasema mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa na pia haki ya kukata rufaa kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo kingine kinachohusika.

“Tulizo la washitakiwa sio mabomu wala virungu, bali ni dhamana kwa kuwa hivi sasa utulivu unatokana na wao, ndio maana hali ya amani inaendelea na wananchi wanafanya shughuli zao kama kawaida,” alidai.

Wakili huyo alidai kuwa washitakiwa hao, wana haki ya kupata dhamana kwa vile kosa hilo sio la mauaji, uhaini au uhalifu wa kutumia silaha, bali wanashitakiwa kwa makosa ya jinai ambayo bado Mahakama haijathibitisha kama wametenda makosa hayo.

Baada ya mvutano uliochukua muda mrefu katika Mahakama hiyo iliyojaa askari na wafuasi wa Uamsho waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo, Hakimu Msaraka Ame Pinja alieleza kuwa suala la dhamana ni haki ya washitakiwa, lakini Mahakama haiwezi kuamua kwa haraka, kunahitajika kutafakari kwa umakini kabla ya kutoa uamuzi.

Aliongeza kuwa vile vile si jambo la busara suala hilo la dhamana kuamuliwa haraka haraka na pia kuchelewesha maamuzi, hivyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 25, mwaka huu  na kwamba mahakama itatoa uamuzi wa kuwapa dhamana ama la.

Wakati wanafunzi waliporuhusiwa kuondoka shuleni, baadhi yao walikuwa wakilalamikia vurugu za Uamsho zinazosababisha kukosekana kwa utulivu na kushindwa kuendelea na masomo kutokana na kurudishwa nyumbani mara kwa mara kutokana na vitendo hivyo.

”Tunamuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwachukulia hatua wahusika wote wa vurugu, sisi tunakosa kuendelea na masomo, leo (jana) tulikuwa tunafanya mitihani ya majiribio, lakini tumeshindwa kuendelea, baada ya walimu kutuambia turudi nyumbani,” alisema mwanafunzi mmoja.

Mwanafunzi mwingine wa shule ya Mwanakwerekwe C aliyejitambulisha kwa jina la Rahma, alisema watu wanaofanya vurugu na kuathiri masomo yao, hawataingia peponi kwa kuwa vitendo hivyo vinamkera na kumchukiza Mwenyezi Mungu.

Chanzo: Nipashe


KATIBU MKUU UN AZUNGUMZIA MPAKA WA ZIWA NYASA

Na Mwandishi wetu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki- Moon, amepongeza msimamo wa Tanzania kutafuta majawabu ya amani katika kujadiliana kuhusu mzozo wa mpaka kati yake na Malawi kwenye Ziwa Nyasa.

Amesema uamuzi wa Tanzania ndiyo njia sahihi na inayokubaliwa kimataifa kutafuta na kupata suluhisho la migogoro ya namna hiyo.

Ban Ki Moon ametoa pongezi hizo kwa Tanzania mjini hapa juzi wakati alipomkaribisha na kukutana kwa mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko New York, kwa ziara ya siku mbili.

“Majuzi nilikutana na Rais Joyce Banda wa Malawi na akanielezea mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa na mazungumzo ambayo nchi zetu mbili zinafanya ili kupata ufumbuzi wa amani. Hii ndiyo njia sahihi na Umoja wa Mataifa unaunga mkono njia hiyo,” Ban Ki Moon alimemweleza Rais Kikwete.

Rais Kikwete alimweleza Katibu Mkuu huyo wa UN kuwa Tanzania bado inaamini kuwa njia sahihi na maelewano zaidi ni kutafuta ufumbuzi wa mvutano huo wa mpaka kwa njia ya mazungumzo.

Rais Kikwete alisema: “Wazo la awali la kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili la miaka mingi sana lilitokana na Rais wa Malawi, marehemu Bingu wa Mutharika ambaye aliniandikia barua ya kutaka nchi zetu zianze mazungumzo kuhusu mzozo huo. Nasi tulikubali. Hivyo, ndivyo tulivyoanza kuzungumza.”

Rais Kikwete alisema kuwa Tanzania inaongozwa na msingi mkuu wa mipaka inayopita kwenye maeneo ya maji ambako mipaka hiyo inakuwa katikati.

“Mpaka kati ya Malawi na Msumbiji kwenye ziwa hilo hilo, Nyasa, umekuwa katikati ya Ziwa tokea mwaka 1954 wakati nchi hizo zilipokubaliana kusahihisha makosa ya kuuweka mpaka huo nje ya Ziwa. Mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye mto mkubwa zaidi unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa uko katikati ya mto wenyewe,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kila mahali ambako nchi zinatengenishwa na maji, mpaka unakuwa katikati ya nchi.  Sisi tunadhani hata kwenye mpaka wetu wa Malawi kwenye Ziwa Nyasa ni lazima uwe katikati ya Ziwa.”
Chanzo: Nipashe

JK: TUVUTE SUBIRA MGOGORO ZIWA NYASA

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kuwa na subira kuhusu tatizo la mpaka wa Ziwa Nyasa.

Alisema katika kushughulikia utata wa mpaka huo na nchi ya Malawi, Tume maalumu ilikuwa ikutane Septemba 10 hadi 15 mwaka huu lakini mkutano huo haukufanyika.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana katika hotuba yake ya kila mwezi kwa Watanzania na kusisitiza kuwa, nchi ya Malawi iliomba mkutano huo usogezwe mbele.

“Sisi tumekubali ombi lao hivyo tunawasubili kwani subira yavuta heri, upande wetu tunaendelea na matayarisho husika kama tutaamua kwenda Mahakama ya Kimataifa (ICJ) nchini Uholanzi,” alisema.

Alitoa wito kwa Watanzania kuitunza na kudumisha amani iliyopo kwa kuheshimu misingi ya katiba, kuepuka vitendo vya uvunjifu wa sheria, kuheshimiana na kuvumiliana kwa tofauti zetu.

“Wananchi wenzangu tuione tunu hii ya amani tuliyonayo kuwa ni ya kuitunza kama mboni ya macho yetu badala ya kuibomoa, wako wenzetu wanaitafuta hawaipati.

“Amani ikitupotea si rahisi kuipata na hata ikirudi madhara yake mtaishi nayo miaka mingi au hata kudumu daima, ni rahisi sana kubomoa nyumba iliyojengwa kwa siku nyingi kwa uzembe wa siku moja tu, lakini kuijenga upya itachukua muda,” alisema Rais Kikwete.

Mkutano wa AGRA

Akizungumzia Mkutano Mkuu wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Rais Kikwete alisema umeiletea sifa na heshima kubwa Tanzania.

Alisema kati ya asilimia 70-80 ya watu katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, wanaishi vijijini na maisha yao yanategemea kilimo ambacho ndio chanzo kikuu cha ajira kwa watu waishio vijijini. 

Aliongeza kuwa, kilimo hutoa mchango mkubwa kwenye pato la Taifa la nchi nyingi pia ndio chanzo kikubwa cha fedha za kigeni na malighafi za viwandani ambapo kutokana na umuhimu wake kama hakijastawi vizuri barani Afrika, hali za watu wengi zinakuwa duni, uchumi wa nchi kudorora na maendeleo kudumaa.

“Katika mkutano huu tulikubaliana kwa pamoja kuwa bila kuongeza uwekezaji na matumizi ya maarifa mapya katika kilimo chetu, uzalishaji hautaongezeka Afrika.

“Tatizo la upungufu wa chakula na njaa litaendelea na watu wengi hasa wa vijijini watabakia kuwa maskini, hivi sasa watu wapatao milioni 239 barani Afrika wanaishi bila ya uhakika wa chakula.

“Hiki kimekuwa chanzo kimojawapo cha utapiamlo na vifo vya akina mama wajawazito na watoto katika nchi za Afrika,” alisema.



Miaka 20  ya vyama vingi

Alisema katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, tumeona maendeleo makubwa ya ukomavu wa demokrasia inavyozidi kushamiri.

Wananchi wa Tanzania wamepata uhuru wa kuanzisha na kujiunga na vyama vya siasa, uhuru mkubwa zaidi wa kufanya na kushiriki katika shughuli za kisiasa, kufanya maandamano na kuitisha mikutano ya hadhara ya kisiasa, kijamii na mingineyo.

Aliongeza kuwa, hivi sasa wananchi wana uhuru mkubwa wa kutoa maoni yao kupitia majukwaa ya mikutano ya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya habari au mitandao ya intaneti na simu za mikononi. 

Utendaji wa vyama vya Siasa

Rais Kikwete alisema CCM imefanikiwa kuleta mageuzi ya kweli ya kupanua demokrasia nchini, kuendeleza haki za binadamu na haki za msingi za raia wa Tanzania.

Alisema mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi ulipoanza kulikuwa na chama kimoja cha siasa ambacho ni CCM na mwaka 1995 vyama 13 vyenye usajili wa kudumu. 

Idadi hiyo ilibakia hivyo mpaka mwaka 2001 na ilipofika mwaka 2005 kulikuwa na vyama 18 na mwaka huu 2012 vyama hivyo vimefikia 20 vyenye usajili wa kudumu.
Chanzo: Majira

RC: WATENDAJI WAZEMBE WAWAJIBISHWE



na Julius Konala, Songea
MKUU wa Mkoa (RC) wa Ruvuma, Said Mwambungu, amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na manispaa mkoani humo kuwawajibisha kwa kuwasimamisha kazi au kuwafukuza maofisa watendaji wa vijiji na kata wazembe ambao watashindwa kuwadhibiti watu wanaofanya uharibifu wa mazingira kwa kuchoma moto na kukata miti ovyo.
Mwambungu alitoa agizo hilo jana wakati akifungua kongamano la kuweka mikakati ya kudhibiti moto hatarishi kwenye maeneo ya misitu mkoani humo lililoandaliwa na kitengo cha Misitu Uenezi, Kanda ya Kusini.
Mkuu huyo wa Mkoa (RC), alisema maofisa watendaji hao wengi wao wamekuwa wakiwafumbia macho wananchi wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira na kwamba vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa viumbe hai na uoto wa asili ambao ni rasilimali ya taifa kwa vizazi vijavyo.
“Vitendo hivi vya uharibifu wa misitu vimekidhiri sana hasa katika tarafa ya Madaba kwa kazi ya kuendeleza biashara ya uchomaji wa mkaa kinyume na taratibu za uvunaji wa misitu hiyo kwa kuwa kasi ya ukataji misitu haiendani na upandaji miti,” alisema Mwambungu.
Aidha, aliwaonya mabwana miti kuacha tabia ya kukaa ofisini kwa lengo la kutoa vibali vya uvunaji wa misitu badala yake wazungukie vijijini kwa ajili kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko, akifunga kongamano hilo alisema katika kukabiliana na tatizo hilo ni vema kamati za mazingira katika kata na vijiji zikapewa nguvu ili kupunguza kasi ya uharibifu huo.
Chanzo: Tanzania Daima


UHABA WA DAWA WAITESA SONGEA

na Stephano Mango
BAADHI ya wagonjwa wanaopata matibabu katika kituo cha afya cha Mjimwema kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, wamelalamikia uhaba mkubwa wa dawa kituoni hapo na kusema waganga wanawashauri kununua dawa katika maduka binafsi ambako zinauzwa kwa bei kubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wagonjwa hao walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifika kituoni hapo kwa lengo la kutaka kupata matibabu, lakini badala yake wamekuwa wakipewa ushauri wa waganga na kuandikiwa dawa ambazo kwenye kituo hicho hazipo.
Mmoja wa wagonjwa hao, alisema kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na kidonda, lakini kila alipokwenda kwenye kituo hicho kwa ajili ya kusafisha alikuwa akishauriwa akanunue dawa kwenye maduka ya watu binafsi, kwani kituo hicho kina uhaba wa dawa kwa muda mrefu.
Mgonjwa mwingine, alisema alipofika katika kituo hicho akiwa anasumbuliwa na malaria, aliambiwa hakuna dawa na badala yake akaelekezwa akanunue kwenye maduka binafsi.
“Jambo la kushangaza hata Panadol nazo wanadai hawana. Tunaiomba serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuona umuhimu wa kuihimiza Bohari ya Dawa (MSD) kuhakikisha inasambaza dawa kwenye zahanati na vituo vya afya kwa wakati muafaka, ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi,” alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Dk. Daniel Mtamakaya, alipohojiwa kuhusiana na malalamiko ya wagonjwa hao, alikiri kwa muda mrefu kituo chake hakijapokea dawa kutoka MSD, jambo ambalo amedai limekuwa likileta usumbufu mkubwa kwa wagonjwa.
Dk. Mtamakaya alisema wamekuwa wakilazimika kuwapa ushauri wa kitaalamu wagonjwa, lakini dawa ni lazima waende wakanunue kwenye maduka ya watu binafsi, kwani tangu Juni mwaka huu hawajapata dawa.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea, Nachoa Zacharia, alisema kuna tatizo kubwa la uhaba wa dawa kwenye zahanati zote za manispaa hiyo kikiwamo kituo cha afya cha Mjimwema.
Chanzo: Taaanzania Daima

Wanajeshi Nao Watoa Maoni Katiba Mpya


Baadhi ya wapiganaji wa JWTZ Brigedi ya Kusini wakifuatilia kwa makini Mkutano wao na Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo(jana) katika kikosi cha JWTZ 411 KJ Songea.

Picha na Mjengwa blog

DC MSTAAFU ADAI KUTELEKEZWA

na Julius Konala, Songea
SERIKALI imedaiwa kumtelekeza bila matibabu mpigania uhuru ambaye amewahi kuwa mkuu wa wilaya kadhaa nchini, Josephat Mhagama (75), maarufu kama (Lilikuliku) aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo, mkewe, Eva Komba, alisema kuwa Mhagama alilazwa zaidi ya mwaka mmoja bila msaada wowote toka serikalini na kwamba hakuna kiongozi yeyote aliyewahi kumtembelea.
Eva ambaye alisoma darasa moja na Spika wa Bunge, Anne Makinda, katika Shule ya Kati Peramiho, alisema mumewe anasumbuliwa na maradhi mbalimbali yakiwemo matatizo ya kibofu cha mkojo, kwikwi na uti wa mgongo hali inayomfanya alale muda mrefu.
Alifafanua kuwa Mhagama alizaliwa mwaka 1937 katika kijiji cha Njoomlole, wilayani Namtumbo, na kusoma shule ya kati Peramiho kisha Sekondari ya Kigonsera ambapo alikutana na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alimtangulia darasa moja mbele.
Alisema kuwa baada ya kumaliza masomo yake aliajiriwa kama bwana shamba wa wilaya ya Songea na kuamua kuacha kazi baada ya kutofautiana na serikali ya kikoloni wakati huo kwa vile alitaka usawa kati ya Wazungu na Waafrika ambapo alirudi kijijini Njoomlole na kuwa Katibu wa TANU wa tawi.
“Mwaka 1963 hadi mwaka 1970 mume wangu alikuwa Katibu Mtendaji wa TANU wa Wilaya ya Songea na mwaka 1965 akagombea ubunge katika jimbo la Songea Kaskazini akichuana na Otien Kambona na kumshinda,” alisema Eva.
Aliongeza kuwa mumewe huyo mwaka 1970 aliteuliwa kuwa Katibu wa TANU wa Mkoa wa Dodoma na mwaka 1971 alipelekwa Singida ambako alifanya kazi na hayati Moses Nnauye ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa mkoa huo na baadaye alifanya kazi na Kingunge Ngombale Mwiru.
“Baadaye walihamishiwa Tanga wakati yeye akiwa Katibu wa TANU, Kingunge alikuwa Mkuu wa Mkoa na Oktoba 1975 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, mwaka 1976 akahamishiwa wilayani Biharamulo hadi mwaka 1980 alipohamia Muheza,” alisema.
Eva aliongeza kuwa mwaka 1981 mumewe alihamishiwa wilayani Manyoni hadi mwaka 1983 aliporejeshwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Songea na mwishoni mwaka huo akastaafu na kurudi kijijini kwake Njoomlole.
Chanzo: Tanania Daima

DC AOMBWA KUINGILIA MZOZO WA ARDHI

na Julius Konala, Mbinga
UONGOZI wa Shule ya Sekondari Agustino iliyoko katika wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, umemuomba mkuu wa wilaya (DC) hiyo, Senyi Ngaga, kuingilia kati kutatua mgogoro wa ardhi baina yao na wananchi wenye mashamba yanayozunguka eneo la shule hiyo.
Ombi hilo lilitolewa jana na mkuu wa shule, Moses Mapunda kwa mkuu wa wilaya hiyo wakati akitoa taarifa ya shule yake katika mahafali ya kwanza ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo.
Mapunda alisema mpango wa shule hiyo ni kuendeleza upanuzi na kujenga chuo cha ualimu kwa ngazi ya cheti na stashahada, lakini juhudi hizo zinapingwa na wananchi wenye mashamba yanayozunguka eneo hilo kwa kutaka fidia kubwa ya sh milioni sita kwa shamba la nusu hekari lisilo na zao lolote.
Alisema kuwa serikali imeshayatenga maeneo hayo kisheria kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa taasisi za elimu pamoja na viwanja vya michezo na sio kwa matumizi ya kilimo au makazi, jambo ambalo amemuomba DC Ngaga kushirikisha wahusika wa Idara ya Ardhi pamoja na mthaminishaji wa ardhi wa serikali ili aweze kufanya tathmini ya mashamba hayo kwani mkurugenzi wa shule hiyo yuko tayari kulipa fidia halali.
Mbali na suala hilo, aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuzisaidia vifaa vya maabara, vitabu na fedha shule za watu binafsi pindi inapopata msaada toka nje badala ya kuelekeza nguvu kwenye shule za serikali pekee kwani zote zinatoa mchango mkubwa wa elimu kwa Watanzania.
Akizungumzia kwa upande wa taaluma alisema shule yake imeweza kufanya vizuri ambapo mwaka 2009 shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza kati ya shule zote zilizofanya mitihani ya wilaya kwa kidato cha kwanza ambapo kati ya wanafunzi kumi bora walitoa wanafunzi saba.
Alisema mwaka 2010 shule ilishika nafasi ya kwanza katika mitihani ya kidato cha pili kwa mkoa ambapo ilishika nafasi ya 46 kati ya shule 387 za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo wanafunzi wote 70 waliofanya mitihani hiyo walifaulu.
Aliongeza kuwa katika matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha sita mwaka 2011, walishika nafasi ya pili kati ya shule sita kimkoa na ya 32 kati ya 129 kitaifa kwa shule zenye watahiniwa chini ya 30 na kwamba wanafunzi 11 walifaulu na kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Alizitaja changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa vitabu vya kiada na ziada, vifaa vya maabara na udogo wa eneo la shule na ukosefu wa viwanja kwa ajili ya kufanyia michezo ya wanafunzi, huku akipongeza jitihada zinazofanywa na serikali katika kusogeza huduma ya nishati ya umeme jambo ambalo litawezesha wanafunzi kujifunza masomo ya kompyuta na kujisomea usiku.
Kwa upande wake DC Ngaga alisema kuwa serikali kwa muda mrefu imekuwa ikithamini michango inayotolewa na sekta binafsi katika suala la elimu na kwamba itaendelea kutoa ushirikiano katika hilo kwa kuweka mazingira mazuri.
Chanzo: Tanzania Daima
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa