POLISI RUVUMA WADAIWA KUMPIGA RISASI DEREVA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Polisi Mkoa wa Ruvuma imeingia matatani baada ya askari wake kudaiwa kumpiga risasi dereva wa bodaboda, Sallgo Nduguru (22) na kumjeruhi kiganja na paja la mguu wa kushoto.
Inadaiwa kuwa, dereva huyo alifikwa na mkasa huo baada ya kutaka kumpora silaha mmoja wa askari waliomkamata kwa kosa la usalama barabarani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Mihayo Msikhela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi ili kutuliza ghasia zilizotokea baada ya madereva wengine wa bodaboda kutaka kupambana na askari.
Kamanda Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 12 jioni katika eneo la Kombezi, Mfaranyaki, Manispaa ya Songea na kudumu kwa muda wa dakika 30.
Kwa mujibu wa Kamanda Msihkela, askari polisi wawili waliokuwa doria walimkamata kijana aliyetambulika kwa jina moja la Aggrey kwa kosa la kuvunja sheria za usalama barabarani, lakini dereva huyo alimpigia simu mmiliki wake, Sallgo Nduguru ambaye naye ni dereva wa bodaboda na kuja na kundi la madereva wengine.
“Baada ya mmiliki huyo kufika na madereva wengine walianzisha vurugu, ambapo Nduguru alidaiwa kutaka kumpora mmoja wa askari hao silaha,” alisema.
 Chanzo;Mwananchi

TANESCO YAKATAA UMEME WA BEI GHALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limekataa mkataba wa kununua umeme wa makaa ya mawe kwa gharama kubwa kutoka Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), kwa kuwa utavuruga mpango wao wa kupunguza gharama ya umeme kwa wananchi.
Akizungumza juzi mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, Meneja Uzalishaji wa Tanesco Makao Makuu, Costa Rubagumya, alisema bei ya umeme wa NDC kwa Tanesco ni kubwa, tofauti na mapendekezo yao kwa shirika hilo la maendeleo.
Kwa mujibu wa Rubagumya, NDC wanataka kuiuzia Tanesco uniti moja ya umeme kwa dola za Marekani senti 9.5, wakati Tanesco walipendekeza iwe dola za Marekani senti saba, ili wafanikishe lengo la kuwauzia wananchi umeme kwa gharama ya chini.
“Kwanza hawa si wazalishaji umeme, bali ni madalali, kwa sababu wakishaingia mkataba na sisi Tanesco, watatafuta mtu mwingine wa kuzalisha umeme, wao ni wachimba madini,” alisema Rubagumya.
Msimamo huo wa Tanesco, ulitolewa wakati Maswi alipotembelea mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, unaoendeshwa na kampuni ya Tancoal kwa ubia na NDC.
Salamu mbaya
Katika hatua nyingine, msimamo huo wa Tanesco ni salamu mbaya kwa wafuaji umeme wa kutumia mafuta mazito na dizeli, ambao wamekuwa wakiiuzia Tanesco umeme kwa bei ghali maradufu, kuliko hiyo ya senti 9.5 ya NDC ambayo imekataliwa.
Maswi mwenyewe alikiri kuwa ni matarajio yake kwamba mgodi huo ukianzishwa, utasaidia kutatua tatizo la umeme unaozalishwa na kuendeshwa kwa gharama kubwa za mafuta.
Wafanyabiashara hao bei yao ni kati ya dola za Marekani senti 33 na 50, wakati Shirika hilo la Umeme linalazimika kuuza umeme kwa Watanzania kwa kati ya dola za Marekani senti 10 mpaka 19, hivyo kujikuta shirika likijiendesha kwa hasara.
Hali hiyo ilisababisha mwanzoni mwa mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kuchakata gesi Mtwara na Lindi, kuahidi kupambana na wafanyabiashara hao mara tu gesi itakapofika Dar es Salaam, ili washushe bei ya umeme wanaouza Tanesco mpaka angalau senti za Marekani nane kwa uniti moja.
Unyonyaji Tanesco
Kwa mujibu wa Pinda, kutokana na bei ya sasa ya wafanyabiashara hao wanaotoa karibu asilimia 80 ya umeme wote wa Gridi ya Taifa, shirika hilo limekuwa likinyonywa karibu Sh bilioni nne kila siku.
“Sisi tunaona kuwa suluhu ya kuondokana na gharama hizi ni gesi, lakini kuna watu wanajua watanyang’anywa tonge mdomoni, vita hii tunaijua; lakini sisi hatuwezi kurudi nyuma katika hili ni lazima tuendelee mbele,” alisema Pinda.
Alisema kuna watu kwa sasa wananufaika na kitendo cha Tanesco kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme. Alisisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuachana na umeme huo wa mafuta.
Alisema kama wafanyabiashara hao, watataka kuendelea na biashara ya kuuzia Tanesco umeme ni vyema wabadilishe mitambo yao iwe ya gesi na sio ya mafuta, kama ilivyo sasa hivi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema bei ya umeme iliyopo kwa sasa ni ya muda tu na itashuka baada ya ujenzi wa bomba la gesi kukamilika, ambapo mitambo ya kufua umeme inayotumia mafuta, itatumia gesi na mitambo mipya ya gesi italetwa.
“Serikali inataka umeme mwingi utokane na gesi, jua, upepo na joto ardhi, lakini wapo wanaokataa bomba lisije Dar es Salaam na hao hao wanalalamika umeme bei juu, mtu yeyote anayejua dunia inakwendaje, hawezi kupinga kujengwa bomba la gesi. “Miaka ijayo, chanzo kikubwa cha umeme nchini kitakuwa gesi asilia… nyie mtanitukana, mtanisema sana lakini mimi nitabaki kwenye utaalamu na wala siwezi kuyumba, tatizo la umeme wa Tanzania litatatuliwa na gesi, kila kitu kikikamilika Tanesco na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji), hawawezi kuendelea kuweka bei juu,” alisema Profesa Muhongo.
Katibu Mkuu ashangaa
Akizungumzia mvutano kati ya Tanesco na NDC ulioibuka katika ziara yake inayoendelea mikoani, Maswi alisema hata yeye anashangaa bei hiyo ya NDC, wakati ufuaji wa umeme wa makaa ya mawe ni nafuu kuliko hata huo wa gesi.
Aliagiza mashirika hayo, NDC na Tanesco, yapeleke taarifa zao za hesabu kuhusu bei hizo ili kupata suluhu ya mradi huo wenye uwezo wa kufua megawati 200 na kuacha kugeuka walalamikaji.
Alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa pande zote kuhusu uanzishwaji wa mtambo huo. Alisema anashangazwa namna mashirika hayo, ambayo yote ni ya umma, yanavyoshindwa kuelewana.
“Kitu kinachotuumiza nchi hii ni wote kugeuka kuwa walalamikaji, sasa Tanesco na NDC wote ni mashirika ya umma, inakuwaje mshindwe kuelewana na kukubaliana kuhusu jambo hili muhimu kwa Watanzania ambao wote mnawahudumia?” alihoji.
Chanzo;Habari Leo 

WARIDHIA KOROSHO KUUZWA MFUMO WA STAKABADHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WADAU wa zao la korosho wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma wameridhia kuuza korosho kupitia mfumo wa Stakabadhi ya mazao ghalani kuanzia msimu huu wa mwaka 2014/2015 zikiwa ni juhudi za kujiletea maendeleo tofauti na sasa ambapo wakulima hao wamekuwa wakipata hasara na kuwanufaisha wajanja wachache pindi wanapouza mazao yao kupitia mfumo wa soko holela.

Aidha wadau hao pia wamewapiga marufuku viongozi wa Vyama vya Msingi vya Wakulima wilayani humo kuendelea na utaratibu wa kwenda kukopa mikopo katika mabenki na kwenda kuwalipa fedha hizo kama malipo yao ya awali na kwamba hali hiyo pekee ndiyo itakayo saidia kuondoa manung'uniko kwa wakulima kulalamikia kuibiwa fedha zao.

Wajumbe hao waliendelea kubainisha kuwa fedha hizo za mikopo zimekuwa ni mzigo mkubwa kwa wakulima kutokana na kutakiwa kulipiwa riba kubwa ambazo hutozwa na mabenki hayo hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakulima kushindwa kulipwa malipo yao ya pili na ya tatu baada ya fedha hizo kuishia kulipia riba za mikopo hiyo katika mabenki ambayo hukopwa na viongozi hao wa vyama vya ushirika, mambo ambayo yamekuwa yakileta ugumu kwa wakulima kuupenda mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani.

Tamko hilo lilifikiwa katika mkutano uliohusisha wadau wa korosho wa kujadili mfumo wa kisheria wa kuuza mazao yao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani.

Aidha katika kuhakikisha kuwa mfumo wa ununuzi wa mazao hayo kwa wakulima unafanikiwa, wakulima hao walikubali kutekeleza makubaliano ya kukusanya mazao yao katika maghala yaliyopo katika maeneo yao na kusubiri wanunuzi waende kununua hukohuko na kugawiwa fedha zao kulingana na idadi ya kilo alizozikabidhi.

Awali akitoa mada ya dhana ya bei dira na utekelezaji wake Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Bw.Mfaume Juma alisema kuwa mfumo huo ulianza kuhamasishwa msimu wa mavuno na mauzo ya korosho mwaka 2013/2014 na kuanza kutumika katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.

Alisema kuwa baadaye wilayani Tunduru mkoani Ruvuma msimu wa mwaka 2007/2008 na kwamba kabla ya hapo wanunuzi walikuwa wakinunua kupitia mfumo wa soko holela lakini wakiwa wananunua kupitia bei dira ambayo ilikuwa ikipangwa na Bodi ya Korosho Tanzania.

Bw.Juma aliendelea kufafanua kuwa pamoja na bodi hiyo kujipanga kusimamia utaratibu huo kwa uwazi kwa kuwashirikisha wawakilishi wa wakulima wakati wa kuuza korosho zao pia wameandaa mkakati maalumu na mazingira ya kusimamia uuzwaji wa korosho za Tunduru ikiwezekana hata kuhakikisha korosho hizo zinauzwa kwa utaratibu wa malipwani.

Alisema kuwa kwa tani 1 huuzwa hadi kwa dola za Marekani 1400, sawa na sh.2,240,000 tani moja sawa na kila kilo moja itauzwa kwa bei ya sh. 2,240 zikiwa ni juhudi za kumuondoa mtu wa kati yani Madalali na viongozi wa vyama vya ushirika mabavyo vimekuwa vikijinufaisha kupitia mgongo wa wakulima, Bw. Juma Aliendelea kueleza kuwa Kupitia mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani kazi za vyama vya msingi ni kukusanya mazao na kuyatunza katika maghala ya chama,kupanga madaraja,kufungasha katika magunia yenye uzito sahihi, kusafirisha korosho hadi sokoni, kusimamia mauzo wakati wa minada na kuwagawia wakulima fedha zao.

Alisema kwamba mtindo wa kukopa fedha katika mabenki haupo katika utekelezaji wa mfumo huo na kwamba viongozi wabadhirifu katika vyama vyao wawatoe wakati wa uchaguzi na kuwaweka madarakani viongozi waadilifu.

Akifafanua matumizi ya mfumo huo Mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la korosho Tanzania, Bw.Athuman Nkinde alisema kuwa pamoja na mkakati huo wa kuwadhibiti walanguzi hao mfuko huo umetenga sh. bilioni 6 kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Mtwara na Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Alisema katika mpango huo kila kiwanda kimetengewa sh. bilioni 2 zikiwa ni juhudi za serikali kukuza soko la ndani ili kuwainua wakulima na kuwawezesha kuuza mazao yaliyosindikwa na kwamba, mkutano huo umelenga kuwajengea uwezo na kufungua upeo kwa wakulima na kuwawezesha wakulima kupata faida na kuiwezesha halmashauri kupata ushuru mkubwa na kuifanya halmashauri yao kujitosheleza katika bajeti zake za matumizi ya ndani

Chanzo:MMjira

UMUHIMU WA ELIMU YA UJASIRIAMALI KATIKA SHULE NA VYUO -1

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Elimu ya ujasiriamali katika nchi yetu haina ‘umri’ mkubwa kama zilivyo taaluma nyingine zikiwamo lugha, historia, siasa na sayansi. Hii ni kutokana na historia ya nchi yetu hasa baada ya kupata uhuru, kwamba tuliamua kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea kupitia Azimio la Arusha.
Siasa ya ujamaa na kujitegemea haikushadidia ujasiriamali kwa vile ulifananishwa na ubepari ambao ulichukuliwa kama unyama. Wale wote waliokuwa wanajihusisha na shughuli za kijasiriamali hasa biashara katika kipindi hicho walionekana kama ‘wanyama’ au watu ambao walikuwa wamechepuka kutoka katika njia kuu ambayo ilikuwa inaaminiwa na jamii kubwa wakati huo.
Wafanyakazi serikalini walikuwa hawaruhusiwi kujihusisha na biashara na kwamba shughuli za ujasiriamali zilionekana kufanywa na watu ambao hawakuwa na elimu ya kutosha kupata ajira, na wageni hasa kutoka Bara la Asia kama vile Wahindi.
Hata hivyo, kutokana na hali halisi ya maisha katika nchi yetu na duniani kwa jumla, kwenye miaka ya katikati ya 2000, taifa lilianza utaratibu wa kuingiza elimu ya ujasiriamali katika elimu ingawa haikuwekewa kipaumbele sana. Kwa sasa elimu ya ujasiriamali imekuwa kama wimbo wa taifa, siyo shuleni na vyuoni bali hata katika sekta ambazo si rasmi kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia matangazo mbalimbali juu ya kuendesha elimu ya ujasirimali katika makundi mbalimbali ya jamii yetu.
Kutokana na wanajamii na taifa kwa jumla kuanza kuona elimu ya ujasiriamali kama mwarobaini wa matatizo yanayowakabili kama vile ajira na umaskini, lengo la makala haya ni kuelezea umuhimu wa elimu ya ujasiriamali katika shule na vyuo kama njia mojawapo yenye kuonyesha jinsi elimu ya ujasiriamali inavyoweza kuisaidia jamii na taifa katika kuleta maendeleo.
Ujasiriamali ni mchakato au hali waliyonayo baadhi ya watu ya kutaka mafanikio yanayoshadadiwa na moyo wa ushindani, kujiamini, uwezo binafsi wa kukabiliana na kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na uthubutu wa kukabiliana na changamoto ambazo wakati mwingine huweza kuathiri maisha yao katika kipindi cha mpito.
Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kama ujasiriamali hufundishwa au mtu huzaliwa nao ingawa si lengo la makala haya kujikita katika mjadala huu, kwa kuwa tunaelewa nguvu iliyonayo elimu katika kuyatengeneza maisha ya mwanadamu.
Elimu ya ujasiriamali ni muhimu sana katika ngazi zote za elimu kwa ajili ya kuwatayarisha vijana juu ya maisha yao ya baadaye.
Tunaamini kuwa vijana wana maono na matamanio yao katika maisha kama walivyo watu wazima ingawa watu hawa wawili wanaweza kutofautiana hapa na pale kutokana na sababu za umri, mazingira, wakati na uzoefu katika maisha.
Elimu ya ujasiriamali katika shule na vyuo hujenga msingi mzuri wa kujiamini miongoni mwa vijana na hivyo kuwafanya wayakabili maisha bila woga, jambo ambalo litawafanya kufanya kazi zao wanazozipenda kwa umahiri, weledi na kujiamini zaidi.
Badala ya kuwafanya vijana wajiamini katika yale wanayoyafanya na wanayoyapenda kulingana na uwezo na vipawa vyao, tumekuwa tukiwatia hofu ya maisha kwa njia ya mitihani kiasi hata cha kutoa mikopo ya elimu kwa kuzingatia madaraja ya ufaulu, jambo ambalo linajenga taifa la watu wasiojiamini katika kazi ambazo si lazima ziwe za kukaa ofisini.
Chanzo;Mwananchi

WAKULIMA WATAKIWA KUJIUNGA NA VIKUNDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WAKULIMA mkoani Ruvuma wameshauriwa kujiunga kwenye vikundi ili waweze kukopa zana za kisasa za kilimo yakiwemo matrekta aina Power Teller, mashine za kisasa za kupukuchua mahindi ili kuweza kuongeza tija uzalishaji kwani kilimo ni biashara hivyo kuweza kujiongezea kipato.

Ushauri huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Bapt Company Mkoa wa Ruvuma, Ayoub Mbilinyi ambayo inajishughulisha na uuzaji na usambazaji wa zana za kisasa za kilimo alisema ili wakulima waweze kuzalisha mazao kwa wingi wanapaswa kubadilisha kilimo chao na kulima kilimo cha biashara kwa kutumia zana za kisasa za kilimo.

Mbilinyi aliongeza kuwa kampuni hiyo inatoa mkopo kwa vikundi na mwananchi mmoja moja ambapo wanachoangalia ni vyanzo vyake vya mapato lakini kwa mkulima anaweza akatoa asilimia 70 ya malipo ya awali ambapo kiasi kinachobakia atalipa kulingana na makubaliano maalumu watakayokubaliana au baada ya mavuno ambapo zana hizo zinapatikana wakati wote ambapo mteja akitoa oda yake anapatiwa zana hizo ndani ya siku saba.

Alisema wakulima hao wanaweza kujiunga na kukopa matrekta makubwa 45hp-95hp(4WD) kwani ni imara na zina nguvu na zinatumia mafuta kidogo badala ya kung'ang'ania kutumia jembe la mkono kwani limeshapitwa na wakati.

"Bado mkoani Ruvuma wakulima hawana mwamko wa kutumia zana za kisasa za kilimo nawashauri wakulima wabadilike na kuanza kutumia zana za kisasa za kilimo kwani mbali na kuuza pia tunakopesha vifaa mbali mbali vya kilimo matrekta, powertiller aina ya Maize Thresher kwa bei nafuu kwani mkulima anaweza kununua kwa kiasi cha sh. milioni 5.5, mashine za kisasa za kupukuchulia mahindi, mashine za kupanda mpunga; na kuvunia mpunga, mashine za kuvuna ngano pamoja na pampu za kumwagilia maji ambapo matarajio yao ni kuhakikisha wanasambaza pembejeo za kilimo zikiwemo dawa,mbolea pamoja na mbegu," alisema.

Aidha, aliwashauri wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kununua vipuri vya matrekta mbali mbali ambavyo havipatikani mkoani humo kwenye kampuni hiyo.

Chanzo:Majira

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa