TUME YA MIPANGO YATEMBELEA BANDARI YA MBABA BAY


Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja (katikati) akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa madini ya Shaba. Wengine kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) Mhandisi Dominick Rwekaza, Kamishna Msaidizi wa Madini na Ukaguzi wa Migodi, Ally Samaje, Kaimu Kamishna Msaidizi sehemu ya Uongezaji Thamani Madini, Latifa Mtoro na Mwakilishi wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA), John Mvumula.
Mfanyabiashara wa madini ya Shaba kutoka Kanda ya Kati Doreen Kisia, akisistiza jambo wakati akichangia hoja katika mkutano huo.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, akiongea jambo wakati akichangia mada kuhusu madini ya Shaba.
Kamishna Msaidizi wa Madini na Ukaguzi wa Migodi, Ally Samaje, akisalimiana na baadhi ya wadau wa madini ya Shaba waliohudhuria mkutano huo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) Mhandisi Dominick Rwekaza, (kulia) akiongea jambo wakati wa mkutano huo.
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja (katikati) katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa wadau wa madini ya Shaba ambao umewajumuisha wafanyabiashara wa madini ya Shaba, wachimbaji wadogo, viwanda vya kuyeyusha madini ya Shaba, Makamishna Wasaidizi wa Madini kutoka Kanda mbalimbali nchini pamoja na baadhi ya Maafisa Madini Wakaazi.

Wizara ya Nishati na Madini imekutana na wadau wa madini ya Shaba katika mkutano wa siku mbili ulioanza tarehe 24- 25 Novemba, 2014 na kuwashirikisha wafanyabiashara wa madini hayo, wachimbaji wadogo, viwanda vya kuyeyusha madini ya Shaba, Makamishana Wasaidizi wa Madini kutoka Kanda mbalimbali nchini pamoja na baadhi ya Maafisa Madini Wakaazi.

Akifungua mkutano huo, unaolenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ndogo ya madini ya Shaba na namna ya kuyaongezea thamani madini hayo, Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja amewataka wachimbaji wadogo nchini kutumia fursa zinazotolewa na Wizara ya Nishati na Madini ikiwemo kupata ruzuku ili waweze kuendeleza shughuli za uchimbaji wa madini jambo ambalo litasaidia kuyaongezea thamani madini hayo.

Aidha, Kamishna Masanja ametumia fursa hiyo, kuwataka wachimbaji na wafanyabiashara kuacha kufanya biashara kinyume na sheria na taratibu kwa kuwa jambo hilo linaikosesha Serikali mapato ikiwemo kuchangia madini hayo kutokupata thamani halisi.

Vilevile Kamishna Masanja ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kuzuia usafirishaji madini ghafi ya Shaba na kueleza kuwa, “Haturuhusu madini ghafi ya shaba kutoka nje, tunataka yatoke yakiwa tayari ni madini, kwasababu kuna zaidi ya shaba hivyo tunapoteza, tunataka kuyaongeza thamani madini yetu hapa hapa nchini”, alisisitiza Masanja.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

KAMPUNI YA MABATI YA ALAF YATOA MSAADA WA MABATI KWA AJILI YA UJENZI WA MAABARA ZA SHULE ZA SEKONDARI WILAYA YA MBEYA.


 Meneja wa Kampuni ya ALAF Tawi la Mbeya, Greyson Mwakasege akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya kabla ya kumkabidhi msaada wa mabati 384 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa maabara.
 Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King, akitoa shukrani kwa kampuni ya ALAF  kwa kujitolea mabati kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari za Wilaya ya Mbeya.
  Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King na Meneja wa ALAF tawi la Mbeya, Greyson Mwakasege wakikabidhiana mabati 284 kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za Kata.
 Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King akiwaonesha waandishi wa habari(hawapo pichani) msaada wa mabati aliyokabidhiwa na Kampuni ya ALAF .
 Meneja wa ALAF tawi la Mbeya, Greyson Mwakasege akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Mbeya bidhaa zingine zinazozalishwa katika kiwanda cha Mbeya.

 Fundi umeme na mtaalamu wa Mashine wa Kiwanda cha kuzalisha mabati, Himid Mwenzegule akiendelea kuendesha mitambo ya mashine ya kuzalisha mabati kiwandani hapo.
 Mashine ya kuzalisha mabati ya migongo ya kawaida aina ya Corrugator ikiendelea na kazi.
 Mashine ya kuzalisha mabati ya migongo mikubwa aina ya IT.
 Mashine ya kuzalisha vigae aina ya Versa Tile
 Mabati aina ya Simba Dumu yaliyozalishwa kiwandani hapo.
 Baadhi ya mabati yaliyozalishwa kiwandani hapo yakiingizwa kwenye Roli tayari kuelekea sokoni kwa wateja.


KAMPUNI ya mabati ya ALAF imetoa  msaada wa mabati 384 kwa ajili ya ujenzi wa maabara za shule za Sekondari za Wilaya ya Mbeya zenye thamani ya shilingi Milioni 7.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King,Meneja wa Tawi la Mbeya Greyson Mwakasege, alisema walipokea maombi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa maabara katika Shule za Kata.
Alisema walikubaliana na ombi hilo na kuona ni vema kusaidia Bandle 32 sawa na mabati 384 yenye thamani ya Shilingi Milioni 7 baada ya mabati hayo kuanza kuzalishwa katika Kiwanda cha Mbeya ambacho pia kinahudumia Mikoa ya Ruvuma, Katavi, Rukwa,Njombe, Iringa na Mbeya.
Alisema ni matarajio yao ya kuendelea kusaidia maeneo mengine kama mchango wa Kampuni kwa jamii inayowazunguka pamoja na kuthamini wateja wake ambao hupata huduma kutoka katika kiwanda cha Mbeya.
Mwakasege aliongeza kuwa katika Kiwanda cha Mbeya kina mashine tatu ambazo ni Mashine aina ya IT inayotengeneza mabati ya migongo mikubwa, Mashine aina ya Corrugator inayozalisha mabati yenye migongo ya kawaida midogo pamoja na mashine aina ya Versa Tile inayozalisha vigae aina ya Versa.
Alizitaja bidhaa zingine zinazopatikana kuwa ni pamoja na Bati za Afrika kusini na vigae vyenye rangi za Bluu, Kijani na Nyekundu,Nondo kutoka Uturuki, Black Pipe, Z parlin na Hollow section.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigallah King, mbali na kutoa shukrani kwa Kampuni ya ALAF  kwa msaada wa mabati pia alitoa wito kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Mbeya kujenga utamaduni wa kuchangia shughuli za maendeleo ya Wilaya.
Alisema mabati hayo yatasaidia katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Galijembe ambayo imeteuliwa na Wilaya kuwa Shule ya Bweni ya wasichana kutokana na ujenzi wa maabara kukamilika kwa asilimia kubwa.
Alisema lengo la kuiteua shule ya Galijembe kuwa shule ya Wasichana ya bweni ya Wilaya ni kuwaondolea adha watoto wa kike ambao asilimia kubwa wanaumri mdogo kwenda uaraiani kupanga vyumba baada ya kufaulu kujiunga na sekondari.
Alisema wasichana wanapata madhara makubwa wakiwa wamepanga kwenye nyumba uaraiani yakiwemo Mimba za utotoni na magonjwa ikiwa ni pamoja na kupunguza hali ya ufaulu darasani kutokana na mazingira hivyo Wilaya ya Mbeya imejipanga kuhakikisha hilo linaondoka.



Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SOMA HAPA-NANI ANACHEZESHA NGOMA YA ESCROW NA IPTL?




Kwa muda sasa kumekuwapo na tuhuma zinazohusu "wizi" wa fedha za akaunti ya escrow iliyofunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2006. Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha zilizokuwa zikilipwa na Shirika la Umeme Tanzania {TANESCO} kwa kampuni ya kufua umeme ya IPTL. Chimbuko la akaunti hiyo ni mgogoro wa tozo hiyo kwamba iligubikwa na utata baada ya kudaiwa kwamba Tanesco ilikuwa ikitozwa fedha nyingi kuliko inavyostahili.
           
Tuhuma za huo "wizi" hata hivyo hazikuishia tu kwa wahusika wakuu yaani makampuni ya umeme, bali zimetiririshwa hadi kwa watu binafsi ambao kimsingi hawana uhusiano wowote na mgogoro huo wa malipo na wala kuhusika kwa njia yoyote na hicho kinachodaiwa kwamba ni uporaji wa fedha za akaunti hiyo ya Escrow. 

Akaunti Escrow ni akaunti ya amana ambayo inawekwa chini ya uangalizi wa mtu wa tatu ili huyo mwangalizi aikabidhi kwa mlengwa pale tu masharti kadhaa yatakapokuwa yamekamilishwa. Hivyo basi akaunti hiyo maalum ya amana ilifunguliwa na kuwekwa chini ya Benki Kuu kama wakala anayesubiria kutekelezwa kwa masharti maalumu ili aikabidhi kwa wenye kumiliki fedha hizo watakapomaliza tofauti zao.
          
Ni vizuri kuliangalia suala hili la akaunti maalum ya amana kwa namna ambayo itawafanya wale wenye kiu ya kutaka kujua ukweli kukidhi hamu yao. 

Fedha iliyokuwa ikiwekwa katika akaunti hiyo ni tozo ya uwezo wa mitambo ya kufua umeme ambayo kampuni ya IPTL ilikuwa ikiitoza Tanesco. Baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kupunguza tozo ya IPTL kutoka USD 3.6million kila mwezi mpaka USD 2.6million kila mwezi baadaye TANESCO ilishauriwa vibaya na wanasheria kwamba tozo hiyo bado ni kubwa kuliko mkataba baina ya IPTL na TANESCO Mei 26, 1995 unavyo eleza.
          
Ubishani uliozuka kati ya mtoa huduma ya umeme yaani IPTL na mtumia huduma ya umeme yaani Tanesco ndio uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti hiyo maalum ya amana yaani escrow account katika Benki Kuu ya Tanzania {BoT} kama njia salama ya kutunza fedha hizo hadi mgogoro utakapokuwa umetatuliwa. 

Ni muhimu kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba mtoa huduma yaani IPTL hasitishi kufua umeme na mtumiaji wa umeme yaani Tanesco naye hakosi umeme wa kuuza kwa walaji wake. Hiyo ni busara ya kibiashara. Fedha hizo zililipwa katika akaunti hiyo maalum kutokana na hati za madai au ankara kutoka kwa mtoa huduma na si vinginevyo.
          
Kitu kimoja kilichojitokeza wazi ni kwamba suala la akaunti hiyo maalum limekuwa likibeba sura mpya kila kukicha na la kusikitisha zaidi ni kwamba vyombo vya habari vilivyo vingi ama vimekuwa vikipotosha kwa makusudi au kwa kutokuelewa mada yenyewe ipasavyo. Vipo vyombo vya habari kwa mfano ambavyo vimedai kwamba "Benki ya Standard Chartered ndiyo mmiliki wa mitambo ya IPTL baada ya kupewa mamlaka hayo na mahakama - Deed of Assignment- inayoiruhusu kuchukua na kumiliki mali za IPTL kutokana na kushindwa kulipa mkopo.

Aidha kwa mujibu wa gazeti la Mawio la Alhamisi Novemba 20-26, 2014 mkataba huo uliipatia benki ya SCB haki za IPTL ndani ya mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na kumiliki mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL.
          
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Mawio Benki ya Standard Chartered inaidai Tanesco dola za Marekani 258.7 milioni kama deni linalotokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na dola za Marekani 138 milioni zinazotokana na mkopo pamoja na riba. Kwa mujibu wa uchambuzi wa Mawio madai hayo ni halali kwa mujibu wa sheria.
          
 Kwa mujibu wa gazeti hilo "nyaraka za serikali zinaonesha kuwa PAP iliamuriwa kulipa wadai wote wa IPTL lakini haikuilipa Benki ya Standard Charted ambayo inajitangaza kuwa ni moja ya wadai.
         
Ni vyema na busara kuanza uchambuzi huu kwa kufanya nukuu hiyo muhimu sana kutoka katika gazeti la kila wiki la Mawio kwa sababu inatusaidia kuonyesha waziwazi kwamba hiki kinachodaiwa kwamba ni kashfa ya fedha za Escrow kina sura nyingi sana kulingana na maslahi yanayolengwa kutetewa. 

Katika muktadha huu ni wazi kwamba anayetetewa hapa ni Benki ya Standard Chartered ambayo inadaiwa kwamba ndiyo yenye haki ya kulipwa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow na kwa mantiki hiyo imeishitaki Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Uingereza.
          
Deni linalodaiwa kwamba Tanesco inadaiwa na Standard Chartered la dola za Marekani linatokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na nyingine ni mkopo na riba. Inashangaza kwamba Tanesco inawezaje kudaiwa na Benki ya Standard Chartered wakati aliyezalisha umeme ni IPTL? Abrakadabra hiyo ndiyo inayomfanya ye yote yule mwenye akili timamu kutambua kwamba kuna mchezo wa kiini macho unaochezwa na benki hiyo dhidi ya Tanzania.
         
Ni wazi kabisa kwamba benki hiyo inalazimisha kuwapo na mgogoro wa kuhusu akaunti ya Escrow kwa lengo moja tu nalo ni kuhakikisha kwamba wanapata nafasi ya kukwapua hizo fedha wanazodai kwamba sio halali kuchukuliwa na IPTL. Kwamba zikichukuliwa na Benki ya Standard Chartered ambayo haijazalisha umeme wala kuwa na ushahidi wowote wa kushiriki katika kuzalisha umeme ni halali kabisa na zikichukuliwa na IPTL ambayo imezalisha umeme na inayo mikataba ya kuuziana umeme na Tanesco si sahihi, ni wizi, ni ujambazi ni hila na kashfa. Hii inahitaji maelezo zaidi kushinda haya yanayotolewa hivi sasa.
          
Ukweli wa mambo ni kwamba mazungumzo kuhusu fedha za Escrow na hususan habari za kujaribu kuonyesha kwamba umiliki wake ni batili una lengo moja tu nalo ni kuandaa mazingira kwa ajili ya Benki ya Standard Chartered hatimaye kuzichukua fedha hizo kwa kutumia kigezo cha kwamba imemilikishwa mitambo ya IPTL na kwamba ndiyo iliyokuwa na haki ya kulipwa tozo ya uzalishaji umeme na si kampuni nyingine yoyote. Hivyo ndivyo kampuni hiyo inavyodai katika kesi iliyofungua dhidi ya Serikali ya Tanzania huko Uingereza.
          
Benki ya Standard Chartered inatumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha inafikia lengo lake la kukwapua fedha za kigeni si chini ya dola milioni 200 kutoka kwa serikali ya Tanzania. Moja ya njia inayotumia ni propaganda ambayo hupenyezwa katika vyombo vya habari kwa kutumia majukwaa mbalimbali. 

Moja ya njia zinazotumika ni kujaribu kuufanya umma uamini kwamba fedha zilizotoka katika ufungaji wa akaunti hiyo ya Escrow zimeibwa na kwamba wahusika katika huo wizi ni pamoja na viongozi kadhaa wa Serikali.
          
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba kuhusishwa kwa watu hao kunafanyika bila hata ya kuwataka wajieleze kama wanaelewa kile wanachotuhumiwa nacho. Wafadhili wa propaganda hizo hawakubali kujitokeza hadharani moja kwa moja kwa kuhofia kuumbuliwa. Matukio huchukuliwa si kwa ujumla wake bali upande mmoja na kuyatangaza kwa namna ya kukidhi matakwa na matarajio yao tu.
          
Tumezoea kuambiwa kwamba wakati suala linapokuwa mahakamani kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi basi si sahihi kuendelea kulijadili kwenye vyombo vya habari kwani kwa kufanya hivyo ni sawa kabisa na kuingilia uhuru wa mahakama. Ni wazi kwamba hata suala linapokuwa katika uchunguzi au upelelezi uwe kwa kutumia tume maalum au makachero basi ni muhali kulizungumzia hadharani na kuwatuhumu na hata kuwahukumu watu kwa ujasiri usio na kikomo kwamba ni wezi au mafisadi au wakumbatiaji wa madhila hayo yote. Hili linafanyika kila siku kupitia vyombo vya habari na chimbuko lake ni baadhi ya wabunge na wanasiasa ambao hufanya hivyo huku wakitumia kila aina ya takwimu za kweli na za kughushi au kubuni tu kichwani.
         
Nini kinachowafanya au kuwapa jeuri hawa watu wanaowatuhumu na kuwahukumu wengine bila ya kujali kwamba hilo halitakiwi wala kupaswa kufanyika bila ya kupitia katika vyombo vya sheria ili kutoka fursa kwa wengine kujitetea? Swali hilo linastahili kujibiwa kwa umakini mkubwa ili kubaini kama kweli hao wanaodai kwamba wanapigania haki ya kiuchumi ya Watanzania ni kweli wanafanya hivyo kwa dhati ya moyo wao kabisa bila ya kuwa na nia nyingine iliyojificha ambayo hawathubutu kuiweka hadharani kwani kwa kufanya hivyo watageuka viroja. 

Pamoja na kwamba kuna kesi mahakamani dhidi ya Serikali ya Tanzania ni wazi kwamba ukiwauliza Standard Chartered kilichowapeleka mahakamani wanasema kwamba wanaionea nchi yetu huruma, Hata hivyo, kamwe hakuna atayekuambia kwamba amekuja hapa kwa ajili ya kujaribu bahati yake kama wanaweza kufanya mbinu wakatengeneza fedha ya bure. Ili kufanikisha malengo yao tuhuma hurushwa kwa yeyote na popote. Ili kufanikisha malengo hayo mtu yeyote yule aweza kuunganishwa katika lolote lile ili kufikia lengo.
          
Ni kwa utaratibu huo huo ndio tunashuhudia jinsi jitihada za Profesa Anna Tibaijuka za kuendeleza mtoto wa kike kielimu zinavyopakwa matope na kukejeliwa mno kwa sababu tu ameomba msaada mahali na akaupata. 

Tujiulize inakuwaje wanasiasa wetu wanathubutu kumhukumu Profesa Tibaijuka na kumuita kila aina ya majina machafu. Ametuhumiwa kwamba ni mwizi eti kwa sababu aliomba msaada kwa ajili ya shule ya Babro Johansson ambayo ni kwa madhumuni ya kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu. 

Profesa Tibaijuka aliomba msaada kwa barua rasmi miaka kadhaa iliyopita na kampuni hiyo haikuweza kumsaidia mapema kutokana na ukata na ni hivi majuzi hali ilipokuwa njema ndipo ikatoa msaada huo.
         
La kustaajabisha ni kwamba msaada huo haukuwa ni siri na ulitolewa kwa uwazi mkubwa bila ya kificho. Sasa huo ujambazi wa Profesa Tibaijuka umetokea wapi? Kosa lake ni kupatiwa fedha alizoomba kwa ajili ya kuisaidia shule ambayo aliianzisha?
          
Tunajiuliza hapa, baada ya VIP kuuza hisa zake kwa PAP na kulipwa na PAP stahili yake, ilifanya kosa gani kutoa msaada kwa shule ya Babro Johansson?
          
Mahitaji na umuhimu wa elimu yanajulikana. Viongozi wanahimiza kila leo umuhimu wa Watanzania kubadilika kuchangia Maendeleo ya Elimu badala ya harusi na sherehe nyinginezo. Leo hii anatokea Mtanzania anaomba msaada wa kuendeleza elimu na anapatikana Mtanzania anakubali kuchangia vizuri maendeleo ya elimu, wawili hawa baadhi ya wanaojiita viongozi wa siasa tena wenye kutaka kuchukua madaraka ya juu kuiongoza nchi, wanalalamika na hata kutamani kutoa roho ya mtu! Watanzania tuzipime dhamira zao. Ni wadanganyifu wasio na uelewa halisi wa matatizo na vipaumbele vya taifa na hivyo kukosa dhamira thabiti ya kuyashughulikia. Wanasukumwa zaidi na tamaa zao binafsi. 
          
Kwa wanaong'ang'ania kudai damu za baadhi ya watu kutokana na hukumu ambayo wao wameipitisha baada ya kufanya kila kitu wao ikiwa ni pamoja na kutuhumu, kupeleleza, kufungua mashitaka, kusikiliza kesi na hatimaye kuhukumu na sasa kutaka kukaza hukumu kwa njia yoyote ile hakuna jambo zuri na jema kama kufanya kile wanachotaka wao yaani kukubali kwamba fedha zote katika akaunti maalum ya escrow ni za serikali na kwamba lazima zirudi serikalini. 

Hata hivyo, wakubwa hao hawataki kurudi nyuma na kujiuliza ni kwa njia gani fedha hizo zimeingia katika akaunti hiyo. Aidha, hawataki kujiuliza kwamba kama Tanesco ndio ilikuwa ikitumbukiza fedha katika akaunti hiyo, ilikuwa ikifanya hivyo kwa kutumia vigezo gani. Swali linguine la kujiuliza, je Serikali hutunza pesa zake kwenye Account zake Benki Kuu au kwenye Escrow Account?
         
Hawaoni mantiki ya kutulia na kujibu swali la msingi kwamba kama Tanesco ingelikuwa inatumbukiza fedha katika akaunti hiyo kwa ajili ya kugharamia tozo la uwezo wa mitambo kuzalisha umeme sasa inakuwaje fedha hizo zirudi tena Tanesco? Ni maswali ambayo wanaojiamini kwamba ukweli wanao wao tu hawataki kuyajibu hata kidogo kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaumaliza utamu wa mchezo wao wa kuigiza. 

Fedha hizo zinatakiwa zirudi Tanesco ili Benki ya Standard Chartered izichukue kwa madai kwamba ndiye mmiliki halali wa IPTL na kwamba kuna deni kama ilivyoainishwa awali katika makala haya.
          
Kutokana na ufafanuzi huo hapo juu ni wazi basi kwamba Tanesco ilikuwa ikilipia gharama za huduma ambayo ilikuwa inaipata kutoka kwa IPTL. Hilo halina ubishi.
          
Lakini pia suala lingine ambalo sasa halina ubishi japo halisemwi makusudi kwa sababu za upotoshaji ni kwamba katika makampuni yote ambayo yanauzia umeme TANESCO, IPTL ndiyo kampuni pekee inayotoza kiwango kidogo cha malipo ya uwekezaji (capacity charges). Suala la kujiuliza hapa ni inawezekanaje IPTL ambayo inatoza kiwango kidogo cha capacity charges ionekane “kuiibia” Serikali kwa kulipwa halali yake wakati makampuni mengine yanatoza capacity charges kwa kiwango cha juu zaidi ya IPTL na hakuna malalamiko.
       Swali la kujiuliza ni kwamba ni kitu gani kinachowasukuma watuhumu kutafuta kila njia ya kuonyesha kwamba kuna hitilafu kubwa sana kwa namna ambavyo suala la akaunti hiyo lilivyohitimishwa?
         
Ukifuatilia kwa karibu na umakini jinsi ambavyo tuhuma zimekuwa zikitolewa ni kwamba kinacholengwa ni fedha zilizokuwa katika akaunti maalumu ambazo ni tozo ya uwezo wa ufuaji wa umeme. Fedha hizo zinagombewa na Benki ya Standard Chartered ambayo ina matawi yake hapa nchini. 

Benki hiyo inatumia kila njia kujaribu kuonesha kwamba fedha zilizokuwapo katika akaunti ya Escrow ni fedha ya Serikali. Kwa mantiki hiyo inachojaribu kufanya Benki hiyo ni kuonyesha kwamba fedha akaunti ya escrow si kwa ajili ya kulipia gharama za uwezo wa mitambo kufua umeme la hasha. Bali ni fedha za Tanesco na kamwe hakuna anayestahili kuzipunguza kwa njia yoyote ile.
          
Cha kushangaza, hata hivyo, ni kwamba benki hiyo, inayodai kuwa iliikopesha fedha IPTL, katika madai yake yaliyopo mahakamani, inadai kuwa yenyewe ndiyo ilistahili kupata fedha zilizokuwa kwenye escrow account! Swali hapa ni je, hiyo asasi ndiyo Serikali? Je, fedha zilizokuwa kwenye escrow account zinakuwa za Serikali na siyo IPTL kwa sababu benki hiyo  haijalipwa?
       
Jitihada za kutaka kuhalalisha kwamba fedha hizo ni mali ya Tanesco na kwamba haziwezi kumegwa hata kidogo zinafanywa na Benki ya Standard Chartered ambayo inataka kutengeneza mazingira ya kuchota fedha kutoka Tanesco kwa madai kwamba ndiyo inayostahili kuwa mlipwaji wa fedha hizo kutokana na deni ambalo kwa mujibu wa madai yao ndio walioikopesha IPTL fedha kwa ajili ya mradi huo wa umeme.
          
Mchezo ambao benki hiyo inafanya hapa nchini ni kuhakikisha kwamba vyombo vya habari vinaandika habari za kuigonganisha serikali na wananchi kwamba Serikali ni ya mafisadi na inayokumbatia ufisadi, na haina ubavu wowote wa kupambana na rushwa. Aidha, asasi hiyo imevirubuni baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari kwamba Mahakama za Tanzania haziaminiki na zinakumbatia ufisadi na kwamba zimekubuhu kwa rushwa.
          
Cha kushangaza, tuhuma hizi za rushwa kwa Mahakama za Tanzania zinakuja muda mfupi tu baada ya benki ya Standard Chartered kuiambia mahakama New York, nchini Marekani iliposhitakiwa na VIP kuwa Mahakama za Tanzania ndizo zenye uwezo wa kusikiliza na kutatua migogoro ya IPTL.
          
Mchezo ambao Standard Chartered Bank inaufanya ni kutumia vyombo vya habari kutoa habari zisizo za kweli na za upotoshi ili kuwachochea watu dhidi ya Serikali yao kutokana na nini kinaendelea ndani ya IPTL.  Mambo mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusiana na Mahakama na watendaji wa Serikali kula rushwa.  Madhumuni ya kufanya hivyo ni kutaka kuonyesha kwamba nchini Tanzania haki haiwezi kutendeka.
         
Madai hayo yote, yanatokea wakati Standard Chartered Bank imefungua kesi London, kwa kisingizio kwamba Mahakama za Tanzania haziwezi kutenda haki  
          
Kwa vipi Standard Chartered Bank inatoa madai kulipwa dola za kimarekani 208 milioni kutoka TANESCO (katika kesi ilivyofunguliwa Mahakama ya usuluhishi (ICSID)) kwa mkopo wa dola milioni 84 kwa IPTL, wakati Serikali ya Tanzania na TANESCO tayari walikwishalipa takribani dola 200 milioni kwa IPTL kufikia mwaka 2006.  Kiasi hicho kingelitosha kulipia mkopo uliokuwa umechukuliwa na kulipa gawiwo kwa VIP na MECHMAR.  Mpaka mwaka 2013 VIP ilikuwa haijalipwa hata senti moja kwa jina lolote.
         
Kampuni ya Mechmar ilitumia fedha zilizodaiwa na IPTL kutoka Serikali ya Tanzania na TANESCO kwa kujilipa yenyewe na Kampuni ya Wartsila madeni hewa (kwa makubaliano na benki ya Danaharta na baadaye Standard Chartered Bank (Hong Kong) Ltd.
         

Standard Chartered Bank (Hong Kong) Ltd inajaribu kutekeleza mpango haramu dhidi ya IPTL kwa kutumia dhamana ya Serikali ya Tanzania na hivyo Serikali ina sababu za kutaka Standard Chartered Bank ithibitishe kama inaidai IPTL.

          Mpaka sasa ukweli ni kwamba Standard Chartered Bank imekwepa kutoa ushahidi kuwa ina madai yoyote dhidi ya IPTL na kwa sababu hiyo na zingine VIP na IPTL/PAP wameifungulia kesi za madai ya fidia na hasara ya TZS 787bilioni na USD 3bilioni katika Mahakama Kuu ya Tanzania. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MAHAKAMA YAAMURU MAITI IFUKULIWE

MGOGORO wakugombea Mwili wa mzee Cleophas Senga (80) Mkazi wa Chanji, Wilayani hapa, mkoani Rukwa, umechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi kufukua maiti ya mzee huyo kwa amri ya Mahakama na kuihifadhi katika hospitali ya hospitali ya Mkoa wa Rukwa.
Maiti hiyo ilifukuliwa jana, majira ya saa 4:40 asubuhi katika makaburi ya Mandela, huku baadhi ya mitaa mjini hapa ikisimamisha huduma za biashara kwa muda wakati umati wa watu ukiwa umejitokeza kushuhudia tukio hilo.
Baadhi ya akinamama waliojitokeza kushuhudia zoezi la ufukuaji wa maiti hiyo waliangua kilio baada ya kuona maiti ikitolewa kaburini na kuingizwa katika gari la polisi aina ya Toyota Landcruiser lenye namba za usajili PT 1275.
Akiongea na mwandishi wa habari, mdogo wa marehemu, Dominiki Senga, alisema mgogoro huo umetokana na mke wanne wa marehemu huyo.
“Wakati marehemu alipostaafu kazi ya udaktari alijenga nyumba Chanji na kufungua duka la dawa akawa anaishi na baadhi ya watoto wa mke mkubwa ambaye nae alikuwa ameshaolewa na mume mwingine na kuwaacha watoto kwa baba yao,”alisema.
Dominiki alisema marehemu alianza kuumwa miezi mitatu iliyopita ndipo kabla mauti hayajamkuta.
Alisema tangu mzee amefariki Novemba 7, mwaka huu wamekuwa wakivutana ambapo mke mdogo wa marehemu na mtoto wake wa kiume wanataka wao ndio wamzike marehemu kwa madai kuwa walikuwa wakimuuguza na wadogo zake na wanandugu pamoja na familia ya mke mkubwa wakitaka ukoo ukamzike marehemu kwa taratibu za kiukoo.
Mvutano huo uliwafikisha wanandugu mahakamani kuomba msaada wa kisheria juu ya nani mwenye haki ya kumzika marehemu.
“Kinachoshangaza tukiwa mahakamani mke mdogo wa marehemu na mwanae anayeitwa Cleophas Senga waliuchukua mwili wa marehemu mochwari na kwenda kuzika katika makaburi ya mandela mjini,”alisema.
Alisema waliamua kumueleza hakimu ndipo akatoa amri ya kufukua mwili wa marehemu na kuuhifadhi mpaka Mahakama itakapotoa uamuzi juu nani anapaswa kumzika mzee huyo.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MAJEMBE WAILALAMIKIA MANISPAA YA SONGEA

KAMPUNI ya Majembe Auction Mart imeilalamikia halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kwamba haijatoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya ulipaji wa ushuru (Service Levy), kabla kampuni hiyo haijaanza kazi ya ukusanyaji.
Majembe Auction Mart imeingia mkataba na manispaa hiyo kuwa wakala wake wa ukusanyaji ushuru.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Majembe Auction Mart Nyanda za Juu Kusini, Nelson Mwasomola, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, baada ya wafanyabiashara wa manispaa ya Songea kuituhumu kampuni hiyo kuwa wanatumia nguvu katika ukusanyaji wa ushuru ambao wenyewe hawajapewa elimu juu ya ulipaji huo.
Mwasomola, alisema kuwa wafanyabiashara wana haki ya kulalamika, kwa sababu halmashauri ilitakiwa iitishe mkutano wa kuwatambulisha kabla ya kuanza kazi jambo ambalo halijafanywa tangu Julai Mosi mwaka huu waliposhinda zabuni hiyo.
Aliongeza kuwa, kitendo cha kutokutoa elimu kwa wakati kimesababisha Majembe kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kukataa kulipa ushuru, jambo linalosababisha malumbano kati ya wafanyabiashara na vijana wa kampuni hiyo.
"Sisi tuliiandikia barua halmashauri yenye kumbukumbu namba MAM/MNS/GC/10 ya tarehe 17 mwezi wa kumi mwaka huu, tukiitaka manispaa iitishe mkutano wa wafanyabiashara itutambulishe kwao na pia iwaelimishe juu ya sheria mpya ya ushuru wa ‘Service Levy’ ambao ulikuwa unatozwa kwa makampuni tu,” alisema.
Alifafanua kuwa, baada ya halmashauri kushindwa kutoa elimu hiyo wameanza kubandika matangazo ya ufafanuzi na kuwaelimisha zaidi wafanyabiashara na kwamba, hadi sasa hawajaanza rasmi kukusanya ushuru wakisubiri zoezi hilo kukamilika.
Aidha, alisema wamepewa orodha ya wafanyabiashara 2,836 na viwango wanavyotakiwa kulipa, ambako nusu yao imebainika kuwa hawana leseni za biashara wala vibanda vyao havina namba, jambo ambalo linawafanya wakwepe kulipa ushuru.
Hata hivyo, alisema ushuru unaolalamikiwa ni mdogo ambao mfanyabiashara anatakiwa kulipa kati ya sh 300 hadi 500 kwa siku na wengine wanalipa senti 50 kwa siku na kwamba, baadhi yao hawana uwazi katika biashara zao hali inayosababisha halmashauri kukosa mapato.
Wafanyabiashara hivi karibuni waliilalamikia kampuni hiyo wakati wa mkutano wao uliofanyika ukumbi wa Familia Bombambili kuwa, kampuni hiyo inatumia nguvu katika ukusanyaji wa ushuru, hali inayosababisha ugomvi wa kutokuelewana.
Inadaiwa kuwa Lazaro Mahenge, muuzaji katika duka moja eneo la Sovi hoteli alipigwa kwa kile kilichoelezwa alikataa kulipa ushuru.
Akijibu tuhuma hizo, Mwasomola alikataa kufanya tukio hilo, isipokuwa kijana huyo alikuwa anamshawishi mmoja wa wafanyabiashara aliyekuwa anaelimishwa juu ya ulipaji wa ushuru kuwa asikubali kuzungumza na watoza ushuru.


Mwasomola, alidai kuwa alichaniwa nyaraka za serikali hivyo katika harakati za kutaka kuziokoa, alimsukuma na sio kumpiga.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WANASHERIA MWANZA WAIFAGILIA WINDHOEK WASEMA NI BORA KWA AFYA

 Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea, Fr James Rugemalira akizungumza katika hafla fupi iliyowashirikisha baadhi ya wanasheria wa jiji la Mwanza kujadili bia za windhoek pamoja na maendeleo ya jiji hilo. Halfa hiyo ilikwenda sanjari na kila mgeni mualikwa kuchangia mada.
 Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea, Fr James Rugemalira (katikati), akizungumza katika hafla hiyo. Kulia ni Mmiliki wa  The Joint Pub iliyopo Isamilo jijini Mwanza.
 Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea, Fr James Rugemalira (kulia), akisisitiza jambo  katika hafla hiyo. Kulia ni Mmiliki wa  The Joint Pub, iliyopo Isamilo jijini Mwanza. (Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
 Hafla ikiendelea.
 Mdau wa Windhoek jijini humo naye alikuwepo 
kwenye hafla hiyo.
 Wanasheria wa jiji la Mwanza wakiwa kwenye hafla hiyo.
 Mwanasheria Mtalemwa (wa pili kushoto), akiwa na wanasheria wenzake  wakifurahia Windhoek.
Kikao na hafla vikiendelea.

Dotto Mwaibale

BAADHI ya Wanasheria wa jiji la Mwanza wamesema unywaji wa bia ya Windhoek utasaidia kujenga afya za wanywaji kwani imetengenezwa kwa ubora wa juu ukilinganisha na bia zingine.

Wanasheria hao waliyabainisha hayo jijini Mwanza katika hafla fupi iliyoandaliwa na Kampuni ya Bia ya Mabibo kwa ajili ya kujua changamoto mbalimbali kutokana na soko la bia za Windhoek na Windhoek Draught na kupata maoni ya wadau wa vinywaji hivyo  iliyofanyika jijini humo mwishoni mwa wiki.

Mmoja wa wanasheria hao,   alisema kwa muda mrefu na familia yake amekuwa akitumia Windhoek na ajawahi kupata shida yoyote  kwani inachangamsha akili tofauti na bia zingine.

Bia hii haiwezi kumfanya mtumiaji ajisikie vibaya hata akinywa kiasi kikubwa na ndio maana mimi na wenzangu tunatumia bia hizi za windhoek.


"Iwapo tutajenga tabia ya kunywa bia hii hakika utafanya kazi zetu kwa uhakika hata tukiwa makazini kwani haitoi harufu mdomo na kulewesha ni vizuri  tukaiunga mkono Kampuni ya Mabibo Bia " alisema Mwanasheria huyo.

Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea, Fr James Rugemalira aliwaomba wanamwanza kuiunga mkono Kampuni ya Mabibo Bia kwa kununua vinywaji vyake kwani mpango wa kampuni hiyo ni kujenga kiwanda ambapo kitakuza uchumi wa mkoa wa Mwanza na kutoa ajira kwa vijana.

"Hatuwezi kukamilisha ndoto zetu za kujenga kiwanda bila ya nyinyi kutuunga na kupata mrejesho mzuri wa mauzo ya bidhaa zetu tuungeni mkono kwa kununua Windhoek Lager na Windhoek Draught zenye namba ya MB66 ubavuni ambazo ndizo halali katika soko la Tanzania na si vinginevyo" alisema Fr James. (Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MWANZA WAIKUBALI WINDHOEK WAFURAHIA MPANGO WA KIWANDA CHA MABIBO BIA WA KUJENGA KIWANDA



Chupa za Windhoek zinavyoonekana.
 Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea, Fr James Rugemalira akizungumza na wadau na wanahabari wa jiji la Mwanza wakati wa Promosheni ya Bia za Windhoek iliyofanyika leo usiku katika Hoteli ya Villa Park Resort jijini humo.
 Mshauri Mkuu wa Fr James Rugemalira, Aniki Kashasha akizungumza na wadau wa jiji la Mwanza pamoja na wanahabari kuhusu bia za windhoek Lager na Windhoek Draught.
  Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea, Fr James Rugemalira (katikati), akiwa amekaa na viongozi mbalimbali meza kuu. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni inayosambaza Gas ya Oryx jijini Mwanza ya Top Kihanja Co Ltd, Christopher Kilaja, Mshauri Mkuu wa Fr James Rugemalira, Aniki Kashasha, Fr James Rugemalira, Mwanasheria Tamy Henry na Michael Thomas ambaye pia na Mwanasheria. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
 Mwanahabari wa Kituo cha Televisheni cha Star TV, Yvone Kamuntu akiuliza swali katika promosheni hiyo.
 Mdau wa Windhoek Mertus Rutashobwa naye alikuwa ni miongoni mwa waalikwa waliopata fursa ya kuizungumzia bia ya Windhoek.
Ofisa Mipango wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Victor Maleko akizungumza katika promosheni hiyo kwa niaba ya wanahabari wa mkoa wa Mwanza.




 Wanahabari wakiwa kwenye promosheni hiyo.
 Wageni waalikwa wakiwa kwenye promosheni hiyo.
 Hapa wadau wa Windhoek wakibadilishana mawazo.


 Warembo hao walikuwepo kupata Windhek katika promosheni hiyo.
 Wanahabari wakichukua taarifa mbalimbali katika 
promosheni hiyo.
 Majadiliano yakiendelea.




 Wadau wakiendelea kupata Windhoek.
 Wadau wa Windhoek ndani ya Villa Park Resort 
katika promosheni hiyo.
 Hapa shughuli imepamba moto waalikwa wakimsikiliza Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea, Fr.James Rugemalira.

Dotto Mwaibale

WAKAZI wa jiji la Mwanza na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa, wamefurahishwa na uwekezaji unaotarajiwa kufanywa na Kampuni ya Bia ya Mabibo (MBL) kwa ajili ya kujenga kiwanda cha bia za Windhoek.

Wakizungumza katika promosheni iliyoandaliwa na kampuni hiyo jijini Mwanza juzi katika  ukumbi wa Villa Park Resort, wanachi hao walionesha kuguswa na uwekezaji huo na kushauri kijengwe kiwanda hicho jijini Mwanza.

Walisema kujengwa kwa kiwanda hicho kutachochea kasi ya maendeleo  ya kiuchumi na kuongeza ajira kwa vijana wa Kanda ya Ziwa.

Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea, Fr James Rugemalira alisema lengo la kufika Mwanza ni kupata mawazo mapya na ushauri wa nini kifanyike katika uwekezaji huo jijini humo.



“Tumeamua tuje Mwanza na kuomba ushirikiano wenu na rai yangu ni kupata maoni yenu ili tukipata fursa tuwe na viwanda vidogo vidogo,lakini si sawa na Tanzania Breweries (TBL),maana hatuwezi kushindana nao,” alisema Rugemalira.

Alisema ushindani wa haki ni lazima kila mtu apate haki ya kushinda,na wataka waweke misingi hiyo kwanza katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Mbeya na Mtwara kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo.

Aliwataka wananchi wa kanda ya ziwa kuwaonesha  na kuwaunga mkono ili wazalishe kinywaji cha windhoek Mwanza badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi kama ilivyo sasa,ambapo kinywaji hicho kinagizwa kutoka nchini Namibia.

“Mtu anaweza kunipa ushauri au akaniamuru atakavyo ili nijitambue na ni vema kukubaliana na ushindani  bila hivyo hatuwezi kupata maendeleo na malengo ya kampuni yetu ni kushirikiana na serikali kukabiliana na uhaba wa ajira kwa Watanzania kwa kujenga viwanda hivyo ”alisema Rugemalira.

Meneja Masoko wa Kampuni ya Mabibo Bia (MBL), Kanda ya Ziwa, Godfrey Mwangungulu alisema Bia ya Windhoek imewahi kushinda medali za juu saba  kwa ubora Barani Afrika tangu ianze kuzalishwa mwaka 1920.

"Bia ya Windhoek ilishinda tuzo hizo mfufulizo kuanzia mwaka 2007, 2008, 2009,2010,2011,2012  na 2013. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa