UFINYU WA BAJETI KATIKA SEKTA YA MICHEZO UMECHANGIA KITUO CHA MICHEZO SONGEA KUSHINDWA KUENDESHA MAFUNZO KWA WANAMICHEZO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Mwandishi Maalum – Songea
 Ufinyu wa Bajeti katika sekta ya michezo umechangia kwa kiasi kikubwa kwa kituo cha Michezo cha kanda ya Kusini- Songea  kushindwa kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa  makocha, marefarii, madaktari wa michezo, uongozi na utawala  katika michezo.

Hayo yamesemwa  leo na Mkuu wa kituo hicho Eliufoo Nyambi wakati  akisoma taarifa ya kituo kwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura wakati alipotembelea kituo hicho ili kuona shughuli za michezo wanazozifanya.

Nyambi alisema miaka ya nyuma kituo hicho kimekuwa kikitoa  mafunzo ya muda mfupi  ya aina tofauti ya michezo  na kufanikiwa kupata wataalamu wa ngazi za makocha, marefa, madaktari wa michezo, utawala na uongozi wanaotoa mafunzo na huduma za kimichezo kutoka mikoa 13  na wengine kupata sifa za kujiunga na chuo cha Maendeleo ya michezo kilichopo Malya wilayani Kwimba.

“Kuanzia mwaka 2011 hadi sasa kituo hiki hakijatoa mafunzo ya michezo katika mikoa inayoihudumia ya  kanda ya Kusini ikiwa ni pamoja na upimaji wa viwanja  hii ni kutokana na ufinyu wa bajeti  uliopo”, alisema  Nyambi.

Kwa upande wake Mhe. Naibu Waziri Wambura alisema nia ya Serikali ni kuimarisha michezo ili watu wapate muda wa kucheza  kwani michezo ni afya, chanzo cha ajira, kujenga mahusiano mazuri katika jamii na Serikali kupata chanzo cha kukusanya maduhuli.

Mhe. Wambura alisema Serikali itaangalia namna ya kukiwezesha na kukiboresha kituo hicho ili kiendelee kutoa mafunzo hayo ambayo yakifanyika yatasaidia kupunguza gharama kwakuwa yanawakusanya wanamichezo wengi katika eneo moja na walimu wa michezo wanaenda kutoa mafunzo.

Naye  Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Benson Mpesya ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Songea alisema hivi sasa  mafunzo ya michezo  yanatolewa na Asasi binafsi lakini kama Kituo hicho kitatoa mafunzo itawasaidia washiriki kupata elimu ya michezo na vyeti vya ushiriki vinavyotolewa  na Serikali.

Mwaka 1980 Serikali ilianzisha vituo vya michezo viwili ambavyo ni kituo cha michezo cha Kanda ya Kaskazini kilichopo mkoani Arusha na Songea.

Kituo cha Michezo  Songea kinahudumia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Iringa , Mbeya, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Dodoma na Songwe.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa