Serikali kuendelea kuagiza dawa ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa nchini

 
Na. Lilian Lundo – MAELEZO

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikishirikiana na Bohari Kuu ya  Dawa (MSD) inaendelea kuagiza dawa ili kuhakikisha zinapatikana muda wote.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt.  Mpoki Ulisubisya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa dawa nchini.

“Kumekuwepo na taarifa zisizo na ukweli zilizotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali inayofuatilia masuala ya afya nchini kwamba MSD inaupungufu mkubwa wa dawa ambapo taarifa hiyo inasema kuwa kuna makopo 173 ya dawa za  paracetamol nchi nzima, taarifa ambazo hazina ukweli wowote” alifafanua Dkt. Ulisubisya

Aidha ameeleza kuwa MSD imepokea makopo 10,000 ya vidonge vya paracetamol na kusambazwa katika vituo vyote vya kutoa huduma za afya nchi nzima.

Vile vile alisema kuwa MSD imesaini mkataba na mtengenezaji wa ndani kwa ajili ya kutengeneza makopo 138,000 ya dawa za  paracetamol yenye ujazo wa vidonge 1,000 ambazo zitaanza kupokelewa wiki ya kwanza ya mwezi Octoba mwaka huu na kusambazwa katika vituo vinavyotoa huduma za Afya nchini.

Hata hivyo alibainisha kuwa antibiotics na dawa za kupunguza maumivu (Ciprofloxacin, Ceftriaxone, Diclofenac, Co-trimoxazole, Amoxycyline, Doxycycline na Metronidazole) ambapo zilikuwa zikihitajika zaidi zimeshapokelewa na MSD na kupelekwa katika kanda zote za MSD kwa ajili ya kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Aliendelea kwa kusema kuwa, dawa za Miradi Msonge ambazo zinatibu na kuzuia magonjwa ya Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu, Ukoma, Kichaa cha Mbwa, Uzazi wa Mpango na chanjo mbalimbali zipo za kutosha kwenye Bohari.

Pia amesema kwa chanjo ambazo ziliripotiwa kutokuwepo zinatarajia kuwasili nchini kuanzia  Octoba 2, 2016, ambapo kwa wale waliotakiwa kupata chanjo hizo lakini hawakupata kutokana na ukosefu huo watataarifiwa ili kuweza kufika kwenye vituo vya afya na kupata chanjo hizo.

Akielezea juu ya hali ya upatikanaji wa dawa nchini Dkt. Ulisubisya alisema kuwa, kwa sasa upatikanaji wa dawa nchi ni asilimia 53 ambapo katika aina 135 za dawa muhimu, aina 71 za dawa hizo zinapatikana ghalani na nyingine zipo kwenye vituo vya kutolea huduma.

Dkt. Ulisubisya alisema kuwa hali ya upatikanaji wa dawa itaimarika zaidi Octoba mwaka huu ambapo Serikali inategemea kupokea kiasi kikubwa cha dawa pamoja na chanjo.
 
Mwisho
 

Watumishi wameaswa kuwasilisha nyaraka zao mapema kabla ya muda wa kustaafu.



Na Eleuteri Mangi- MAELEZO

Serikali katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti 2016 imefanikiwa kulipa jumla ya sh. bilioni 511.86 ikiwa ni malimbikizo ya mwajiri kwa watumishi waliostaafu.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mary Chatanda Mbunge wa Korogwe Mjini aliyehoji kuhusu changamoto inayowakabili wastaafu ya kucheleweshewa mafao yao na Mfuko wa pensheni wa PSPF katika mwaka wa fedha 2015/2016.

“Kucheleweshwa kwa malipo ya wastaafuhakutokani na Serikali, isipokuwa waajiri ndio baadhi ya nyaraka zinazohusika ili kuaandaa malipo ya wastaafu hao alisema Dkt. Kijaji.

Naibu Waziri Dkt. Kijaji amesema kuwa nyaraka zinazomhusu mtumishi ziwasilishwe ndani ya muda wa miezi mitatu hadi sita kabla ya muda wa kustaafu ili malipo yake yaweze kuandaliwa kwa wakati na kupata stahili zao ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Aidha, jumla ya sh. bilioni 83.25 zimelipwa ikiwa ni malipo ya deni kabla ya mwaka 1999 hali inayoonesha kuwa Serikali inaendelea kulipa malimbikizo ya madai ya wastaafu na mafao mengine yanayotolewa na Mfuko huo ili waweze kuendesha maisha yao baada ya kustaafu.

Katika kipindi cha mwezi Januari hadi Julai 2016 Mfuko umelipa mafao ya pensheni ya mwezi kwa kiasi cha sh. bilioni 117 ambapo kwa sasa mfuko huo unaendelea kulipa malimbikizo ya mafao ya mkupuo kwa wastaafu wapya na mafao mengine.

Katika kudhihirisha dhamira hiyo ya kulipa mafao ya wastaafu, Dkt. Kijaji amesema kuwa tangu Julai 2015 bodi za mifuko ya hifadhi za jamii zinaendelea kufanyia kazi mafao ya wastaafu na kuwalipa stahili zao kwa asilimia 50 kulingana na maelekezo ya Serikali.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Muhagama ameliarifu Bunge kuwa mfumo na sheria vimeunganishwa na kutoa fursa kwa mtumishi anapohama kutoka ajira moja kwenda nyingine anaruhusiwa kuhama kutoka mfuko moja kwenda mfuko mwingine. 
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa