ASILIMIA 70 YA WATANZANIA KUSHIRIKI KATIKA SHUGHULI ZA KIUCHUMI. Na Ally Daud-MAELEZO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


WATANZANIA zaidi ya asilimia 70 wamepewa kipaumbele  kushiriki katika shughuli za kujenga uchumi wa nchi kufikia uchumi wa kati katika kutekeleza sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi mpaka kufikia mwaka 2020.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi(NEEC) Bi. Beng’i Issa wakati wa ufunguzi wa ripoti ya Tathimini  ya Sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambao umefanyika leo jijini Dar es salaam.
“Tunataka kufikia 2020 watanzania asilimia zaidi ya 70 waweze kushiriki katika shughuli za kiuchumi ili kufikia katika uchumi wa kati ili kutekeleza sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini” amesema Bi. Issa.
Aidha Bi.Issa amesema kuwa watanzania wanatakiwa washiriki katika shughuli za kiuchumi na wasitegemee zaidi wawekezaji kutoka nje ili kuifanya Tanzania iendelee kiuchumi kutoka ngazi ya mmojammoja  hadi kufikia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa Meneja wa Utafiti na ufatiliaji wa Sera hiyo kutoka NEEC Bi. Frola Kajela amesema kuwa Serikali imeandaa sera hiyo ili kuwezesha watanzania kutumia rasilimiali zilizopo katika kuinua uchumi wa nchi na kuweza kumilikiwa na watanzania wenyewe.
“Sera hii inalenga zaidi kwa watanzania kumiliki uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini ili kujishughulisha katika kuleta maendeleo ya nchi kwa jamii na taifa kwa ujumla mpaka kufikia 2020” alisema Bi. Kajela.
Aidha Bi. Kajela amesema kuwa sera hiyo inafanyiwa maboresho ili kuweza kuwafikia watanzania wote katika kuelewa na kumiliki uchumi kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza  mpango wa serikali uliyowekwa kuhakikisha watanzania wanajiinua kiuchumi.
Mwisho.

Mchakato wa uandaaji wa sera ya Filamu wawavutia wasanii wa filamu nchini


Na: Genofeva Matemu - WHUSM
Wadau wa tasnia ya filamu nchini wameipongeza Serikali kuwashirikisha katika mchakato wa uandaaji na ukamilishaji wa Sera ya filamu nchini.
Hayo yamesemwa na wadau mbalimbali walioshiriki katika kikao cha kupitia uchambuzi wa hali halisi ya tasnia ya filamu kwa ajili ya maandalizi ya Sera ya filamu kilichofanyika mapema wiki hii.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa sekta ya filamu hapa nchini imekuwa ikisimamiwa na kongozwa na Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 lakini kutokana na kukua kwa tasnia ya filamu ilionekena kuwa kuna uhitaji wa Sera ya Filamu itakayo kuwa dira na mwongozo katika kukuza tasnia hiyo.
Bibi. Fissoo amesema kuwa Bodi imekamilisha hatua ya uchambuzi wa hali halisi ya sekta ya filamu kwa kiasi kikubwa kwa kupitia machapisho mbalimbali pamoja na kuangaia mifano ya nchi zilizopiga hatua katika sekta ya filamu kama vile Afrika ya Kusini, Kenya, Nigeria pamoja na kuzingatia mchango mkubwa kutoka kwa wadau wenyewe ambao wamewezesha kupatikana kwa takwimu muhimu.  
Aidha Muigizaji wa filamu nchini Bw. Saidi Jangala amesema kuwa sera inayoandaliwa iweke maelekezo ya kuzingatia utengenezaji wa filamu zinazobeba historia ya Kitanzania kama vile historia ya Majimaji, pia sera hiyo ianishe mikakati mahsusi ya upatikanaji wa mitaji pamoja na kuipa kipaumbele michezo ya kuigiza kwani michezo hiyo ndiyo chachu kuu ya weledi katika uigizaji.
Naye Msanii wa filamu nchini Bw. Chiki Mchoma ameiomba kamati ya kuanda sera ya filamu kuhakikisha sera inayoandaliwa inaelekeza wadau wa filamu kuandaliwa mifumo ya elimu pamoja na kuweka misingi ya kufilisi wanaojihusisha na uharamia wa kazi zao na kuwawajibisha wanaonunua kazi zitokanazo na uharamia.  
Hata hivyo mtaalamu wa Kiswahili Pro. Hermas Mwansoko ameitaka kamati ya kuandaa sera ya filamu kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye filamu zetu kusaidia kuzitofautisha filamu za Kitanzania na zingine.

Kukamilika kwa sera ya filamu nchini kutabadilisha kabisha taswira nzima ya sekta ya filamu hapa nchini kwani itatoa dira ama mwelekeo wa tasnia. Hii itawezesha kuongezeka kwa fursa za uwekezaji katika tasnia, kuweka mwongozo kuhusu motisha na fursa za mitaji, uzalishaji wa bidhaa bora zenye kuzingatia weledi pamoja na filamu kuangaliwa kama chombo cha kukuza uchumi kwa manufaa kwa Taifa na watanzania wote.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa