MHE. POSSI: JAMII IWASHIRIKISHE WATU WENYE ULEMAVU KATIKA FURSA ZOTE ZA MAENDELEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na.Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Mhe. Dkt. Abdallah Possi ameiasa jamii kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika shughuli zote za maendeleo ili kusaidia kuwainua na kuondokana na dhana ya utegemezi na kuwakwamua kiuchumi.
Dkt.Possi ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Wilaya za Mbinga, Songea Vijijini na Nyasa mkoani Ruvuma ambapo alitembelea Shule zenye kuhudumia watu wenye mahitaji maalum za Songea Boys, Luhira, Huruma na Kituo cha Kulelea wenye ulewavu cha Peramiho Disabled Persons Action (PEDIPA) na Kituo cha kulele wazee na wenye ukoma cha Nge Wilayani Nyasa.
Katika ziara hiyo Mhe.Possi alibaini changamoto nyingi za watu wenye ulemavu na kuishauri jamii namna pekee ya kutatua changamoto wanazokabiliana nazo ni jamii kuona umuhimu wa kuwashirikisha watu hao katika mipango yote ya maendeleo.

“Halmashauri ziandae mipango ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kuweza kushiriki kikamilifu katika kujitafutia kipato na hii itasaidia kuondokana na hali ya utegemezi na kuondoa mitazamo hasi juu ya watu wenye ulemavu kuwa hawawezi” .Alisema Mhe.Possi.

Waziri Possi alisisitiza kuwa ni lazima Halmashauri ziwe na ubunifu wa miradi ya maendeleo itakayo walenga watu wenye ulemavu, “Ni vyema sasa kuwe na jitihada za makusudi za kuunda miradi maalum kwa ajili ya kuwapa nafasi za ushiriki ili kujitafutia vipato na kuyakabili mazingira yao, ikumbukwe wakina mama waliachwa nyuma kwa muda mrefu ila baada ya kupaza sauti zao tunaona sasa wanasikika hivyo hivyo iwe kwa watu wenye ulemavu” Alisitiza Dkt.Possi.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyasa Dkt.Osca Albano alisisitiza kuyapokea maelekezo yote ya Naibu Waziri Mhe.Possi kwa vitendo na kumhakikishia kuwa Wilaya yao itakuwa mstari wa mbele katika kulitekeleza hilo.
 “Sisi tunafanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Halmashauri hivyo ni vyema tukalichukua hilo kuangalia namna tunavyoweza kuliweka katika mipango yetu yote ya maendeleo ili kuwasaidia na kufikia lengo la serikali,” alisema Dkt. Albano.
Nae Katibu Tawala Wilaya ya Songea Bw. Edmund Siame aliomba halmashauri zote ziwe zinatoa mrejesho mapema juu ya maagizo yanayotolewa na viongozi wa juu huku Mwalimu Elswida Charles anayehudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum akimweleza Dkt. Possi kuwa watu wenye ulemavu wanafarijika kutokana na jitihada anazofanya kuwainua watu wenye ulemavu.

VIDEO - NAIBU WAZIRI POSSI AWAPA UKWELI WAHITIMU AJUCO SONGEA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu) Mhe. Dkt. Abdallah Possi.

VIDEO - WAKAZI WA MWENGE MSHINDO WA MUOMBA RAIS AWASAIDIE WAWEZE KULIPWA STAHIKI ZAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Baadhi ya wananchi wa kata ya MWENGEMSHINDO Manispaa ya SONGEA mkoani RUVUMA ambao maeneo yao yamechukuliwa na MAMLAKA ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) kwa kipindi cha miaka tisa iliyopita bila kuwalipa fidia yoyote, wamemuomba rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania DOKTA JOHN POMBE MAGUFULI kuingilia kati suala hilo ili waweze kupata haki yao.story kamili bonyeza hiyo video.

VIDEO- WAKULIMA WA ZAO LA KORSHO TUNDURU WANUFAIKA NA BEI MPYA YA ZAO HILO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh7m671y6bLV1959JfjkFmMXlz2n_74O1PXN1RZNGPetI9APnbo7kPPcQlteWIZe54vQy1sCiOaKXrM1P7BOWgrrX7QbDQ2T5p-2hv4r88s_MJut8o8CvTcVr3A3io2As6JNBUX6PpypD32/s1600/IMG_4156.jpg
WAKULIMA wa korosho Wilaya ya Tunduru, wameondokana na umasikini kutokana na kupata soko la uhakika baada ya Kampuni ya Namela General Trade kushinda zabuni ya kununua zao hilo wakulima kwa bei ya Sh 3,757 kwa kilo, ikizishinda kampuni nyingine saba.

Hadi kufikia Novemba 14, kulikuwa na zaidi ya tani 541 zilizoingizwa katika ghala la Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru (Tancu) ambako kampuni hiyo ilipewa kununua korosho tani 400 huku Kampuni ya Machinga iliyoshinda nafasi ya pili katika mnada huo, ikipata kibali cha kununua tani 141 kwa bei ya Sh 3,750.

Bei ya kununua mahindi yaongezwa

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Songea, imelazimika kuongeza bei ya kununulia mahindi ya wakulima mkoani Ruvuma kutokana na ushindani mkubwa, baada ya kuwepo kwa wanunuzi binafsi wengi wanaonunua mahindi kwa bei kubwa.
Kutokana na ushindani uliopo, NFRA kuanzia Novemba 7, mwaka huu ililazimika kupandisha bei ya kununua mahindi hadi kufikia Sh 580 kwa maeneo ya vijijini na Sh 600 kwa watakaoleta katika kituo kikuu cha Ruhuwiko mjini Songea.
Hayo yalisemwa na Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Majuto Chabruma, alipozungumzia kazi ya ununuzi wa mahindi katika vituo mbalimbali vilivyotengwa katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma.
Chabruma alisema mwaka huu Serikali ilituma Sh bilioni 6.4 kwa ajili ya kununua mahindi tani 12,000 za awali huku malengo ikiwa ni kununua tani 22,000 na bado wanaendelea na kazi hiyo japo hawajafikia lengo lao.
Hata hivyo, kuna ushindani mkubwa wa soko kutoka kwa watu na kampuni binafsi ambazo zimeingia mkoani Ruvuma kwa ajili ya kununua mahindi.
Chabruma alisema serikali imeona ni vyema kuongeza bei ya mahindi ili kukabiliana na ushindani wa bei iliyopo sokoni, jambo lililosababisha kupungua kwa mahindi.
Alisema bado wakala unaendelea kununua ziada ya mahindi ambayo bado ipo kwa wakulima na wauzaji wengine katika kituo cha Ruhuwiko Songea na amewashauri wakulima mkoani Ruvuma ambao bado wana mahindi nyumbani kuyauza kwa wakala huo.
Alisema hatua hiyo itaiwezesha serikali kufikia malengo yake na nchi kwa jumla iwe na akiba na kuwezesha kutoa nafaka hiyo pindi kutakapojitokeza uhaba wa chakula nchini.
Aidha, Chabruma aliwakumbusha wakulima mkoani Ruvuma kuanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo wakati huu kwani mvua za kwanza zimeshaanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, pamoja na baadhi ya mikoa mingine nchini.

SERIKALI YATENGA BILIONI 13 KUWEKA MAJI SAFI RUVUMA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge  akijibu swali Bungeni leo mjini Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho, Dodoma.

Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 13.17 katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa lengo la kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya mkoa wa Ruvuma ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata maji safi na salama.

Kiasi hicho cha fedha kimetajwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge alipokuwa akijibu swali la Mhe. Jacqueline Ngonyani (Viti Maalum) lililohoji juu ya muda ambao Serikali itapeleka majisafi na salama katika Mkoa huo.


Waziri amesema kuwa Mpango wa Utekelezaji wa Maji Vijijini ulioanza mwaka 2006/ 2007, mkoa wa Ruvuma ulipangiwa vijiji 80 na kati ya vijiji hivyo jumla ya vijiji 76 vilipata maji safi na salama.  


“Asilimia kubwa ya vijiji vilivyokuwa katika miradi hiyo vimepata maji safi na miradi iliyobakia ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji hivyo kwa mwaka huu wa fedha Ruvuma imetengewa kiasi cha fedha cha bilioni 13.17 ili changamoto ya maji safi na salama katika mkoa huo iishe kabisa”, alisema Lwenge.


Ameongeza kuwa Serikali imeendelea na mipango ya kuboresha huduma hizo katika miji ya Songea, Mbinga, Namtumbo na Tunduru iliyopo katika mkoa huo ambapo kwa mji wa Songea, mradi wa ukarabati wa chanzo cha maji cha mto Ruhila Darajani umekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6.


Amefafanua kuwa kukamilika kwa chanzo hicho mnamo mwezi Februari mwaka huu kumeongeza kiasi cha upatikanaji wa maji wa jumla ya lita milioni 6 kwa siku ambapo wakazi 164,162 wamenufaika katika Manispaa hiyo.


Aidha, Mhandisi Lwenge amebainisha kuwa kwa sasa Serikali imekamilisha usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya uboreshaji wa huduma hizo katika miji iliyopo katika mkoa huo.


“Serikali inaendelea na jitihada ya kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ambayo kwa mji wa Tunduru mradi utagharimu  Dola za Kimarekani milioni 7.3, mji wa Namtumbo ni Dola za Kimarekani 12.08, na Dola za Kimarekani 11.86 kwa ajili ya mji wa Mbinga”, alisema Mhandisi Lwenge.

Elimu yaondoa Presha kwa Wazazi Mwaka mmoja wa Serikali ya JPM

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Bijampola ni kijana aliyekuwa na bidii sana shuleni, ndoto yake ilikuwa awe rubani pindi akimaliza masomo yake ya taaluma hiyo. Kwa bahati mbaya kwa kijana huyo, wazazi wake walikosa ada ya kumsomesha, hivyo akaishia darasa la nne na ndoto yake ikaishia hapo, kwa sasa ni mtoto wa mitaani, inasikitisha. Je Bijampola angekuwa anasoma kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano ndoto yake ingezimika au ingetimia! Bila shaka ingetimia kwani Serikali hii imeamua kutoa Elimu ya Msingi bure.
Kati ya mambo ya kupongezwa na kuungwa mkono ni hili suala la ELIMU BURE. Hakika Rais John Pombe Joseph Magufuli na Serikali yake wanawajali wananchi na hasa wa kipato cha chini ambao ndio wengi. Hili nalisema bila kificho kwani kutoa elimu kuanzia awali, msingi hadi sekondari ni jambo la kushukuru sana na litafanya vipaji vingi viweze kuibukka kwani wazazi hawatashindwa kuwapeleka watoto wao shule kwa kisingizio cha kukosa ada. Hongera Mzee wa Hapa Kazi Tu.
Kwa msingi huu au mfumo huu ndoto za akina Bijampola haziwezi kufa tena ni lazima zitimie. Ni dhahiri kwamba watoto wengi walikuwa wanazagaa mitaani pasipo kwenda shule kwa sababu wazazi wao hawakuwa na uwezo wa kuwasomesha. Baada ya elimu kutolewa bure tunaona watoto wa mitaani kupungua kwa kiwango kikubwa.
Katika hotuba ya Mhe. Rais ya kufungua Bunge la 11 mnamo Novemba 20, 2015 mjini Dodoma, Dkt. Magufuli alisema yafuatayo kuhusu elimu, “Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu.  Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi.  Aidha, tutahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k. Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, kama tulivyoahidi kwenye kampeni.  Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati.  Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga mkono Benki ya walimu ili iweze kuwanufaisha zaidi”.
Wahenga husema haja ya mja hunena, muungwana ni vitendo. Usemi huu umedhihirika na Serikali ya Awamu ya Tano kutekeleza kwa vitendo yale wanayoahidi ikiwemo hili la elimu bure.
Ni ukweli usiopingika kuwa kila mwenye kuthamini utu wa Mtanzania ni lazima akubaliane na kitendo cha kiungwana kilichofanya na Serikali ya Magufuli kama Mhe. Mwenyewe anavyoinadi cha kutoa elimu bure.
Ukweli huu unadhihirishwa na Mkazi wa Mbweni ambaye ni mzazi wa watoto wawili, Bi Pelagia Mpanda anayetoa ya moyoni kuhusu elimu bure. “ Kwa kweli ninamshukuru sana Mhe. John Pombe Magufuli kwa kutoa elimu bure kwa watoto wetu, mimi nina watoto mapacha ambao nimewasomesha kwa taabu sana kuanzia chekechea hadi darasa la saba. Mamilioni ya pesa yamenitoka na si kwamba nilikuwa tajiri la hasha nimekuwa nikikopa huku na kule na fedha nyingine nikipata kwenye shughuli za ujasiriamali, lakini cha moto nilikiona.” Ameendelea kusema, “Nilivyosikia Elimu inatolewa bure hadi sekondari nilishukuru sana nikashauriana na mume wangu watoto wetu tukawapeleka sekondari ya serikali ambapo wanafanya vizuri, kwa kweli nasema Magufuli umetujali sisi watu wa hali ya chini na Mungu akulinde uendelee kutuongoza na kutusaidia,”
Mzazi huyu anaendela kusema kwa sasa hapa presha na anasomesha watoto wake kwa raha na fedha anayoipata anaielekeza kwenye miradi mingine ya maendeleo. Amemwomba Mhe. Rais atupie jicho hata kwenye shule binafsi wapunguze viwango vya ada ili wale ambao bado wanasomeshja watoto wao katika shule hizo waweze nao kupata unafuu.
Elimu bure imegusa watu wengi na kuwafurahisha, hapa Mratibu Elimu Kata ya Keko, Bi Happines Elias jijini Dar es Salaam naye anasema haya kuhusu Elimu Bure, “Kwa kweli suala la Elimu bure nimelipokea kwa mikono miwili, mimi kama mwalimu najua jinsi ambavyo wazazi wamekuwa wakiangahika na michango mbali mbali kwa ajili ya watoto wao shuleni, lakini baada ya vitu hivi kuondolewa wazazi na watoto wan amani na watoto wanafanya vizuri darasani kwa sasa kwani hawana wasi wasi wa kufukuzwa.”
Mratibu huyu ameongeza kusaema kuwa anaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kujali elimu na hasa baada ya kuondoa ada haikuishia hapo bali imetoa madawati kwa kila shule, watoto hawakai chini tena. Ameongeza kuwa yeye kipindi anafundisha aliwahi kudondoka darasani wakati akipitapita katikati ya wanafunzi katika harakati za kukwepa kuwakanyaga akadondoka chini. Hivyo kwa sasa anasema adha hiyo haipo tena na anataraji ata viwango vya ufaulu vitaongezeka kwani mazingira ya kusomea yameboreshwa.
Kuhusu furaha ya Elimu bure, binti Mariam Yahaya, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Bunju Sekondari yeye anasema suala la Elimu bure amelifurahia sana kwani baada ya kumaliza  darasa la saba hakuwa na uhakika wa kuendelea na masomo ya sekondari kwani wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumlipia ada. Hivyo anasema, “Kwa kweli nimeruha sana kuwa Serikali inatoa elimu bure, hivyo nina hakika nitaendelea na masomo yangu bila wasi wasi.”

Picha ya Wanafunzi wakiwa Darasani


Naye   Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ambaye ndiye msimamizi wa shule za msingi na sekondari nchini anafafanua jinsi serikali ilivyojipanga kugharamia elimu ya msingi, “SERIKALI inapeleka Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kugharimia elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.”
Simbachawene anabainisha kuwa katika mpango huo, Serikali itagharimia gharama zote za  mtihani wa kidato cha nne kwa wanafunzi wote, tofauti na miaka yote ambapo wanafunzi hutozwa gharama za mitihani. Anasema fedha hizo zitatolewa moja kwa moja na Serikali kupia  Baraza la Mitihani (NECTA).
“Majukumu ya Serikali kuhusu utoaji elimu bila malipo yameelezwa katika waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2015, Serikali itabeba jukumu hili. Kutokana na kuwabana mafisadi tumeweza kupata fedha za kutosha,”anasisitiza Simbachawene.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali inatoa ruzuku ya uendeshaji wa shule Sh 10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh 25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kila mwaka.
Simbachawene anaongeza kuwa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya fidia ya ada Sh 20,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya kutwa na Sh 70,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka.

Ama kweli Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha dhamira ya dhati ya kumkomboa mwanachi hasa wa kipato cha chini. Elimu Kwanza na maendeleo yanafuata. Hii inadhihirisha kuwa Serikali hii imezidi kutambua kuwa Elimu ni Ufunguo wa Maisha na ndio maana suala la elimu limepewa kipaumbele na kuingizwa kwenye mradi wa matokeo makubwa sasa (BRN)
Ni mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ambapo mengi mazuri yameonekana katika Elimu hasa ili lililowaondolea wazazi wengi adha ya mikopo ili wawapelek watoto wao shule. Heko JPM na Falsafa yako ya Hapa Kazi Tu imedhihirika kwa vitendo.
MWISHO
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa