Elimu yaondoa Presha kwa Wazazi Mwaka mmoja wa Serikali ya JPM

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Bijampola ni kijana aliyekuwa na bidii sana shuleni, ndoto yake ilikuwa awe rubani pindi akimaliza masomo yake ya taaluma hiyo. Kwa bahati mbaya kwa kijana huyo, wazazi wake walikosa ada ya kumsomesha, hivyo akaishia darasa la nne na ndoto yake ikaishia hapo, kwa sasa ni mtoto wa mitaani, inasikitisha. Je Bijampola angekuwa anasoma kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano ndoto yake ingezimika au ingetimia! Bila shaka ingetimia kwani Serikali hii imeamua kutoa Elimu ya Msingi bure.
Kati ya mambo ya kupongezwa na kuungwa mkono ni hili suala la ELIMU BURE. Hakika Rais John Pombe Joseph Magufuli na Serikali yake wanawajali wananchi na hasa wa kipato cha chini ambao ndio wengi. Hili nalisema bila kificho kwani kutoa elimu kuanzia awali, msingi hadi sekondari ni jambo la kushukuru sana na litafanya vipaji vingi viweze kuibukka kwani wazazi hawatashindwa kuwapeleka watoto wao shule kwa kisingizio cha kukosa ada. Hongera Mzee wa Hapa Kazi Tu.
Kwa msingi huu au mfumo huu ndoto za akina Bijampola haziwezi kufa tena ni lazima zitimie. Ni dhahiri kwamba watoto wengi walikuwa wanazagaa mitaani pasipo kwenda shule kwa sababu wazazi wao hawakuwa na uwezo wa kuwasomesha. Baada ya elimu kutolewa bure tunaona watoto wa mitaani kupungua kwa kiwango kikubwa.
Katika hotuba ya Mhe. Rais ya kufungua Bunge la 11 mnamo Novemba 20, 2015 mjini Dodoma, Dkt. Magufuli alisema yafuatayo kuhusu elimu, “Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu.  Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi.  Aidha, tutahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k. Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, kama tulivyoahidi kwenye kampeni.  Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati.  Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga mkono Benki ya walimu ili iweze kuwanufaisha zaidi”.
Wahenga husema haja ya mja hunena, muungwana ni vitendo. Usemi huu umedhihirika na Serikali ya Awamu ya Tano kutekeleza kwa vitendo yale wanayoahidi ikiwemo hili la elimu bure.
Ni ukweli usiopingika kuwa kila mwenye kuthamini utu wa Mtanzania ni lazima akubaliane na kitendo cha kiungwana kilichofanya na Serikali ya Magufuli kama Mhe. Mwenyewe anavyoinadi cha kutoa elimu bure.
Ukweli huu unadhihirishwa na Mkazi wa Mbweni ambaye ni mzazi wa watoto wawili, Bi Pelagia Mpanda anayetoa ya moyoni kuhusu elimu bure. “ Kwa kweli ninamshukuru sana Mhe. John Pombe Magufuli kwa kutoa elimu bure kwa watoto wetu, mimi nina watoto mapacha ambao nimewasomesha kwa taabu sana kuanzia chekechea hadi darasa la saba. Mamilioni ya pesa yamenitoka na si kwamba nilikuwa tajiri la hasha nimekuwa nikikopa huku na kule na fedha nyingine nikipata kwenye shughuli za ujasiriamali, lakini cha moto nilikiona.” Ameendelea kusema, “Nilivyosikia Elimu inatolewa bure hadi sekondari nilishukuru sana nikashauriana na mume wangu watoto wetu tukawapeleka sekondari ya serikali ambapo wanafanya vizuri, kwa kweli nasema Magufuli umetujali sisi watu wa hali ya chini na Mungu akulinde uendelee kutuongoza na kutusaidia,”
Mzazi huyu anaendela kusema kwa sasa hapa presha na anasomesha watoto wake kwa raha na fedha anayoipata anaielekeza kwenye miradi mingine ya maendeleo. Amemwomba Mhe. Rais atupie jicho hata kwenye shule binafsi wapunguze viwango vya ada ili wale ambao bado wanasomeshja watoto wao katika shule hizo waweze nao kupata unafuu.
Elimu bure imegusa watu wengi na kuwafurahisha, hapa Mratibu Elimu Kata ya Keko, Bi Happines Elias jijini Dar es Salaam naye anasema haya kuhusu Elimu Bure, “Kwa kweli suala la Elimu bure nimelipokea kwa mikono miwili, mimi kama mwalimu najua jinsi ambavyo wazazi wamekuwa wakiangahika na michango mbali mbali kwa ajili ya watoto wao shuleni, lakini baada ya vitu hivi kuondolewa wazazi na watoto wan amani na watoto wanafanya vizuri darasani kwa sasa kwani hawana wasi wasi wa kufukuzwa.”
Mratibu huyu ameongeza kusaema kuwa anaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kujali elimu na hasa baada ya kuondoa ada haikuishia hapo bali imetoa madawati kwa kila shule, watoto hawakai chini tena. Ameongeza kuwa yeye kipindi anafundisha aliwahi kudondoka darasani wakati akipitapita katikati ya wanafunzi katika harakati za kukwepa kuwakanyaga akadondoka chini. Hivyo kwa sasa anasema adha hiyo haipo tena na anataraji ata viwango vya ufaulu vitaongezeka kwani mazingira ya kusomea yameboreshwa.
Kuhusu furaha ya Elimu bure, binti Mariam Yahaya, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Bunju Sekondari yeye anasema suala la Elimu bure amelifurahia sana kwani baada ya kumaliza  darasa la saba hakuwa na uhakika wa kuendelea na masomo ya sekondari kwani wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumlipia ada. Hivyo anasema, “Kwa kweli nimeruha sana kuwa Serikali inatoa elimu bure, hivyo nina hakika nitaendelea na masomo yangu bila wasi wasi.”

Picha ya Wanafunzi wakiwa Darasani


Naye   Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ambaye ndiye msimamizi wa shule za msingi na sekondari nchini anafafanua jinsi serikali ilivyojipanga kugharamia elimu ya msingi, “SERIKALI inapeleka Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kugharimia elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.”
Simbachawene anabainisha kuwa katika mpango huo, Serikali itagharimia gharama zote za  mtihani wa kidato cha nne kwa wanafunzi wote, tofauti na miaka yote ambapo wanafunzi hutozwa gharama za mitihani. Anasema fedha hizo zitatolewa moja kwa moja na Serikali kupia  Baraza la Mitihani (NECTA).
“Majukumu ya Serikali kuhusu utoaji elimu bila malipo yameelezwa katika waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2015, Serikali itabeba jukumu hili. Kutokana na kuwabana mafisadi tumeweza kupata fedha za kutosha,”anasisitiza Simbachawene.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali inatoa ruzuku ya uendeshaji wa shule Sh 10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh 25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kila mwaka.
Simbachawene anaongeza kuwa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya fidia ya ada Sh 20,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya kutwa na Sh 70,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka.

Ama kweli Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha dhamira ya dhati ya kumkomboa mwanachi hasa wa kipato cha chini. Elimu Kwanza na maendeleo yanafuata. Hii inadhihirisha kuwa Serikali hii imezidi kutambua kuwa Elimu ni Ufunguo wa Maisha na ndio maana suala la elimu limepewa kipaumbele na kuingizwa kwenye mradi wa matokeo makubwa sasa (BRN)
Ni mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ambapo mengi mazuri yameonekana katika Elimu hasa ili lililowaondolea wazazi wengi adha ya mikopo ili wawapelek watoto wao shule. Heko JPM na Falsafa yako ya Hapa Kazi Tu imedhihirika kwa vitendo.
MWISHO

ASILIMIA 70 YA WATANZANIA KUSHIRIKI KATIKA SHUGHULI ZA KIUCHUMI. Na Ally Daud-MAELEZO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


WATANZANIA zaidi ya asilimia 70 wamepewa kipaumbele  kushiriki katika shughuli za kujenga uchumi wa nchi kufikia uchumi wa kati katika kutekeleza sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi mpaka kufikia mwaka 2020.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi(NEEC) Bi. Beng’i Issa wakati wa ufunguzi wa ripoti ya Tathimini  ya Sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambao umefanyika leo jijini Dar es salaam.
“Tunataka kufikia 2020 watanzania asilimia zaidi ya 70 waweze kushiriki katika shughuli za kiuchumi ili kufikia katika uchumi wa kati ili kutekeleza sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini” amesema Bi. Issa.
Aidha Bi.Issa amesema kuwa watanzania wanatakiwa washiriki katika shughuli za kiuchumi na wasitegemee zaidi wawekezaji kutoka nje ili kuifanya Tanzania iendelee kiuchumi kutoka ngazi ya mmojammoja  hadi kufikia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa Meneja wa Utafiti na ufatiliaji wa Sera hiyo kutoka NEEC Bi. Frola Kajela amesema kuwa Serikali imeandaa sera hiyo ili kuwezesha watanzania kutumia rasilimiali zilizopo katika kuinua uchumi wa nchi na kuweza kumilikiwa na watanzania wenyewe.
“Sera hii inalenga zaidi kwa watanzania kumiliki uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini ili kujishughulisha katika kuleta maendeleo ya nchi kwa jamii na taifa kwa ujumla mpaka kufikia 2020” alisema Bi. Kajela.
Aidha Bi. Kajela amesema kuwa sera hiyo inafanyiwa maboresho ili kuweza kuwafikia watanzania wote katika kuelewa na kumiliki uchumi kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza  mpango wa serikali uliyowekwa kuhakikisha watanzania wanajiinua kiuchumi.
Mwisho.

Mchakato wa uandaaji wa sera ya Filamu wawavutia wasanii wa filamu nchini


Na: Genofeva Matemu - WHUSM
Wadau wa tasnia ya filamu nchini wameipongeza Serikali kuwashirikisha katika mchakato wa uandaaji na ukamilishaji wa Sera ya filamu nchini.
Hayo yamesemwa na wadau mbalimbali walioshiriki katika kikao cha kupitia uchambuzi wa hali halisi ya tasnia ya filamu kwa ajili ya maandalizi ya Sera ya filamu kilichofanyika mapema wiki hii.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa sekta ya filamu hapa nchini imekuwa ikisimamiwa na kongozwa na Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 lakini kutokana na kukua kwa tasnia ya filamu ilionekena kuwa kuna uhitaji wa Sera ya Filamu itakayo kuwa dira na mwongozo katika kukuza tasnia hiyo.
Bibi. Fissoo amesema kuwa Bodi imekamilisha hatua ya uchambuzi wa hali halisi ya sekta ya filamu kwa kiasi kikubwa kwa kupitia machapisho mbalimbali pamoja na kuangaia mifano ya nchi zilizopiga hatua katika sekta ya filamu kama vile Afrika ya Kusini, Kenya, Nigeria pamoja na kuzingatia mchango mkubwa kutoka kwa wadau wenyewe ambao wamewezesha kupatikana kwa takwimu muhimu.  
Aidha Muigizaji wa filamu nchini Bw. Saidi Jangala amesema kuwa sera inayoandaliwa iweke maelekezo ya kuzingatia utengenezaji wa filamu zinazobeba historia ya Kitanzania kama vile historia ya Majimaji, pia sera hiyo ianishe mikakati mahsusi ya upatikanaji wa mitaji pamoja na kuipa kipaumbele michezo ya kuigiza kwani michezo hiyo ndiyo chachu kuu ya weledi katika uigizaji.
Naye Msanii wa filamu nchini Bw. Chiki Mchoma ameiomba kamati ya kuanda sera ya filamu kuhakikisha sera inayoandaliwa inaelekeza wadau wa filamu kuandaliwa mifumo ya elimu pamoja na kuweka misingi ya kufilisi wanaojihusisha na uharamia wa kazi zao na kuwawajibisha wanaonunua kazi zitokanazo na uharamia.  
Hata hivyo mtaalamu wa Kiswahili Pro. Hermas Mwansoko ameitaka kamati ya kuandaa sera ya filamu kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye filamu zetu kusaidia kuzitofautisha filamu za Kitanzania na zingine.

Kukamilika kwa sera ya filamu nchini kutabadilisha kabisha taswira nzima ya sekta ya filamu hapa nchini kwani itatoa dira ama mwelekeo wa tasnia. Hii itawezesha kuongezeka kwa fursa za uwekezaji katika tasnia, kuweka mwongozo kuhusu motisha na fursa za mitaji, uzalishaji wa bidhaa bora zenye kuzingatia weledi pamoja na filamu kuangaliwa kama chombo cha kukuza uchumi kwa manufaa kwa Taifa na watanzania wote.

Serikali kuendelea kuagiza dawa ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa nchini

 
Na. Lilian Lundo – MAELEZO

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikishirikiana na Bohari Kuu ya  Dawa (MSD) inaendelea kuagiza dawa ili kuhakikisha zinapatikana muda wote.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt.  Mpoki Ulisubisya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa dawa nchini.

“Kumekuwepo na taarifa zisizo na ukweli zilizotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali inayofuatilia masuala ya afya nchini kwamba MSD inaupungufu mkubwa wa dawa ambapo taarifa hiyo inasema kuwa kuna makopo 173 ya dawa za  paracetamol nchi nzima, taarifa ambazo hazina ukweli wowote” alifafanua Dkt. Ulisubisya

Aidha ameeleza kuwa MSD imepokea makopo 10,000 ya vidonge vya paracetamol na kusambazwa katika vituo vyote vya kutoa huduma za afya nchi nzima.

Vile vile alisema kuwa MSD imesaini mkataba na mtengenezaji wa ndani kwa ajili ya kutengeneza makopo 138,000 ya dawa za  paracetamol yenye ujazo wa vidonge 1,000 ambazo zitaanza kupokelewa wiki ya kwanza ya mwezi Octoba mwaka huu na kusambazwa katika vituo vinavyotoa huduma za Afya nchini.

Hata hivyo alibainisha kuwa antibiotics na dawa za kupunguza maumivu (Ciprofloxacin, Ceftriaxone, Diclofenac, Co-trimoxazole, Amoxycyline, Doxycycline na Metronidazole) ambapo zilikuwa zikihitajika zaidi zimeshapokelewa na MSD na kupelekwa katika kanda zote za MSD kwa ajili ya kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Aliendelea kwa kusema kuwa, dawa za Miradi Msonge ambazo zinatibu na kuzuia magonjwa ya Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu, Ukoma, Kichaa cha Mbwa, Uzazi wa Mpango na chanjo mbalimbali zipo za kutosha kwenye Bohari.

Pia amesema kwa chanjo ambazo ziliripotiwa kutokuwepo zinatarajia kuwasili nchini kuanzia  Octoba 2, 2016, ambapo kwa wale waliotakiwa kupata chanjo hizo lakini hawakupata kutokana na ukosefu huo watataarifiwa ili kuweza kufika kwenye vituo vya afya na kupata chanjo hizo.

Akielezea juu ya hali ya upatikanaji wa dawa nchini Dkt. Ulisubisya alisema kuwa, kwa sasa upatikanaji wa dawa nchi ni asilimia 53 ambapo katika aina 135 za dawa muhimu, aina 71 za dawa hizo zinapatikana ghalani na nyingine zipo kwenye vituo vya kutolea huduma.

Dkt. Ulisubisya alisema kuwa hali ya upatikanaji wa dawa itaimarika zaidi Octoba mwaka huu ambapo Serikali inategemea kupokea kiasi kikubwa cha dawa pamoja na chanjo.
 
Mwisho
 

Watumishi wameaswa kuwasilisha nyaraka zao mapema kabla ya muda wa kustaafu.



Na Eleuteri Mangi- MAELEZO

Serikali katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti 2016 imefanikiwa kulipa jumla ya sh. bilioni 511.86 ikiwa ni malimbikizo ya mwajiri kwa watumishi waliostaafu.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mary Chatanda Mbunge wa Korogwe Mjini aliyehoji kuhusu changamoto inayowakabili wastaafu ya kucheleweshewa mafao yao na Mfuko wa pensheni wa PSPF katika mwaka wa fedha 2015/2016.

“Kucheleweshwa kwa malipo ya wastaafuhakutokani na Serikali, isipokuwa waajiri ndio baadhi ya nyaraka zinazohusika ili kuaandaa malipo ya wastaafu hao alisema Dkt. Kijaji.

Naibu Waziri Dkt. Kijaji amesema kuwa nyaraka zinazomhusu mtumishi ziwasilishwe ndani ya muda wa miezi mitatu hadi sita kabla ya muda wa kustaafu ili malipo yake yaweze kuandaliwa kwa wakati na kupata stahili zao ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Aidha, jumla ya sh. bilioni 83.25 zimelipwa ikiwa ni malipo ya deni kabla ya mwaka 1999 hali inayoonesha kuwa Serikali inaendelea kulipa malimbikizo ya madai ya wastaafu na mafao mengine yanayotolewa na Mfuko huo ili waweze kuendesha maisha yao baada ya kustaafu.

Katika kipindi cha mwezi Januari hadi Julai 2016 Mfuko umelipa mafao ya pensheni ya mwezi kwa kiasi cha sh. bilioni 117 ambapo kwa sasa mfuko huo unaendelea kulipa malimbikizo ya mafao ya mkupuo kwa wastaafu wapya na mafao mengine.

Katika kudhihirisha dhamira hiyo ya kulipa mafao ya wastaafu, Dkt. Kijaji amesema kuwa tangu Julai 2015 bodi za mifuko ya hifadhi za jamii zinaendelea kufanyia kazi mafao ya wastaafu na kuwalipa stahili zao kwa asilimia 50 kulingana na maelekezo ya Serikali.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Muhagama ameliarifu Bunge kuwa mfumo na sheria vimeunganishwa na kutoa fursa kwa mtumishi anapohama kutoka ajira moja kwenda nyingine anaruhusiwa kuhama kutoka mfuko moja kwenda mfuko mwingine. 

MAHENGE AAGIZA KILA KATA KUJENGA ZAHANATI MOJA YA KIJIJI


Na Godfriend Mbuya
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr. Binilith Mahenge amesema ameagiza kila kata kujenga zahati moja kwenye kijiji kimoja kila mwaka ili kurahisishia wananchi kupat huduma za afya na kuepuka adhan ya kutembea umbali mrefu tutafuta huduma.

Akizungumza na East Afrika Radio katika  kipindi cha SUPAMIX  Mahenge amesema kama kata ina vijiji vinne basi ndani ya miaka minne itakuwa na zahati kila kijiji, huku akisisitiza kuwa serikali ya mkoa imejipanga vizuri kuhakikisha inatatua matatizo makubwa matatu  suala la elimu, maji na afya.

“Wananchi wanatumia muda mwingi kwenda kwenye maji, wanachukua muda mwingi kwenda kwenye vituo vya afya pia muda mwingi watoto kwenda shuleni hivyo muda mwingi wa kufanya kazi kama ilivyo adhma ya serikali ya ‘Hapa Kazi Tu’ unatumika katika kupata huduma za kijamii jambo ambalo tunataka kuondokana nalo kwa kuelekeza nguvu zetu katika maeneo hayo”- Amesema Mahenge.
Aidha kuhusu namna serikali ya mkoa wake inavyosaidi vijana na wanawake Mkuu huyo wa Mkoa amesema agizo la serikali katika Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 5% kwa wanawake na 5% kwa vijana linafanyiwa kazi hivyo makundi hayo yajiunge katika vikundi ili kuweza kupata fedha hizo.

DC TUNDURU JUMA HOMERA AWATIA MBARONI VIONGOZI 4 KWA TUHUMA ZA KUUZA VIWANJA.


Askari akiwa amewakamata Viongozi wawili wa Serikali ya Kijiji waliokuwa wakituhumiwa kwa ubadhirifu wa viwanja.

Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Ndugu Japhet Muogopeni Mnyagala akizungumza mbele ya Wananchi .


Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera akizungumza na Wananchi wa Vitongoji vya FrankWeston na Umoja vilivyokumbwa na mgogoro wa ardhi.
Mkuu wa Wilaya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera akimuagiza Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Ndugu Japhet Muogopeni Mnyagala kuchukua hatua stahiki kuhusiana na mgogoro wa Ardhi ndani ya Wilaya hiyo.


Wananchi wakimsikiza kwa makini Mhe DC. Juma Zuberi Homera .
 
Mkuu wa Wilaya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera, amewatia mbaroni Viongozi wanne wa Serikali ya vijiji kwa kosa la usimamizi mbovu wa ardhi katika Vitongoji vya Umoja na Frank Weston katika kata ya Nanjoka Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.

Akisoma taarifa mbele ya Mkuu wa Wilaya Bw. Yahaya Issa Abdallah alimueleza DC. Homera kuwa Vitongoji vya Umoja na Frank Weston vimekumbwa na mgogoro wa ardhi kati ya Wenyeji, Wageni na Wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya Tunduru kwa muda mrefu.

Aidha Serikali kupitia Idara ya Ardhi na Maliasili Wilaya, iliwapimia ardhi Wananchi toka 11/08/2014 lakini ikabainika kuwa mpaka  30/06/2016 bado Wananchi hawakupewa maeneo yao na kuna baadhi ya Wafanyakazi wa Halmashauri pamoja na Wageni wapo kwenye orodha ya Wananchi wanaopaswa kugawiwa Viwanja.

Akihutubia kwenye mkutano huo wa hadhara, uliyofanyika katika Shule ya Msingi Umoja, DC Homera aliwaeleza Wananchi kuwa wasiwe na shaka,kwa sababu Serikali ipo upande wao na hakuna atakaye dhurumiwa haki yake, alisema “Namtaka Mhasibu wa Ardhi na Maliasili alete orodha ya waliolipia Ardhi maeneo ambayo siyo ya wakazi, na ambao ni Watumishi wa Halmashauri wafutwe kwenye orodha hiyo na warejeshewe fedha zao”.

Mfano, kuna baadhi ya watumishi wa Idara ya Ardhi na Maliasili,ambao wamefanya ujanja ujanja kinyume cha sheria kwa kuwaweka watoto wao kwenye orodha,na majina yao yameorodheshwa hapa,hivyo hatua za kisheria na taratibu zitafanyika kuondoa huu mgongano ambao umejitokeza katika hili pia. 
 Kama vile haitoshi ikabainika kuwa kuna kuna baadhi ya Viongozi walikusanya fedha  za wananchi  wapatao 522 na kutowapa risiti,jambo amablo ni hujuma za wazi kabisa  za kuikosesha Halmashauri ya Tunduru Mapato na kupelekea fedha kuwa mikononi mwa wajanja wachache.

Aidha aliwataka Wafanyakazi wa Idara ya Ardhi na Maliasili kujieleza ni kwa nini wamewagawia watu ardhi ambao sio wakazi? kwa nini wamefanya udanganyifu wa kuwa milikisha ardhi Watumishi wa Halmashauri kwa njia za rushwa? na kwa nini wananchi zaidi ya 522 hawajapewa maeneo yao kwa zaidi ya Miaka Miwili?

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Wilaya ndg. Japhet Muogopeni Mnyagala alikiri kufanya kosa,lakini pia alimuakikishia Mkuu wa Wilaya ndani ya wiki moja wananchi wataanza kugawiwa viwanja na zoezi hilo litaanza Kesho (leo).

Mkuu wa wilaya aliwaagiza askari wakamate viongozi walio kuwa wasimamizi wa upimaji wa maeneo katika vitongoji vya Umoja na Frank Weston ambao ni Mohammed Dumsala, Matola Limelime, Halid Daud na Tekla Damas.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa