Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KWA muda mrefu kabla ya kurejeshwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa yalikuwapo madai ya kupata Katiba mpya. Madai haya yaliongezeka na kupata nguvu zaidi baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi. Kwa kiasi kikubwa madai haya yalichangiwa na mapendekezo ya Tume ya Jaji Francis Nyalali ambayo, pamoja na mambo mengine, ilitamka kwamba mfumo wa vyama vingi usingeweza kustawi chini ya Katiba iliyotungwa na chama kimoja kwa lengo la kulinda maslahi yake. Pendekezo hilo halikukubaliwa na badala yake mfumo wa vyama vingi ukarejeshwa chini ya katiba ya mwaka 1977 bila maelezo wala mjadala.
Hivyo madai ya Katiba mpya yakaendelea na hatimaye kuwagawa Watanzania katika makundi matatu. Kundi la kwanza lilidai Katiba mpya. La pili lilidai kwamba hakuna haja ya jambo hili na la tatu likipendekeza marekebisho ya mambo fulani fulani katika Katiba ya mwaka 1977. Mwishowe, lakini kwa shingo upande, serikali ilianzisha mchakato wa kutunga Katiba mpya.
Hata hivyo mivutano iliendelea kati ya makundi haya na hasa kati ya wale waliotaka Katiba ya kuleta mabadiliko ya msingi na wale waliopinga mabadiliko hayo. Kwa kiasi kikubwa hali hiyo inaendelea na ndiyo ilivuruga mjadala na kusababisha mgawanyiko ndani ya Bunge Maalumu la Katiba mpaka wabunge wa Ukawa wakatoka na mchakato mzima wa kutunga katiba ukavurugika. Mgawanyiko huo umeendelea kukua mpaka Ukawa wakaamua kususia kura ya maoni na baadhi ya maaskofu kuwashauri waumini wao kupiga kura ya hapana.
Katiba ni nini?
Katiba ya nchi ina maana angalau tatu. Maana ya kwanza ni Katiba kama makubaliano ndani ya jamii husika kuhusu mambo muhimu yanayohusu maisha ya jamii hiyo na jinsi ya kuyasimamia na kuyaendesha. Mambo hayo ni pamoja na tunu (core values), mfumo wa uchumi, maadili na miiko ya jamii na viongozi wake, pamoja na upeo na dira ya jamii hiyo. Maana ya pili ni Katiba kama mkataba kati ya watawala au viongozi na watawaliwa au wananchi kuhusu mfumo wa uongozi au utawala unaowafaa.
Sura hii hujumuisha mambo kama haki za raia, mipaka ya mamlaka ya serikali, mihimili ya dola na madaraka yake ikiwamo bunge, serikali na mahakama. Maana ya ya tatu ni katiba kama sheria mama. Katika mwonekano huu katiba huweka misingi ya sheria zinazoweza kutungwa na bunge au mamlaka nyingine zisiende kinyume na masharti ya katiba; vinginevyo zinavunja katiba na hivyo kuwa batili. Katika hali halisi nyuso hizi zote za katiba huunganika katika katiba moja
Katika uzoefu wa ulimwengu kuna katiba zilizoandikwa na zile ambazo hazijaandikwa zinazotegemea historia, maamuzi ya mahakama, miswada ya Bunge na utamaduni wa ki-siasa wa nchi husika. Uingereza, kwa mfano, haina katiba kama andiko maalum ila hutegemea mkusanyiko wa maamuzi mbali mbali ya bunge, serikali na mahakama. Vile vile kuna katiba zilizotungwa kulinda maslahi ya tabaka la wachache wenye mamlaka ya kutawala na kukandamiza walio wengi. Hata hivyo katiba za kisasa katika zama za demokrasia ni katiba zinazotungwa kuweka mamlaka ya juu mikononi mwa wananchi ambao huwa na uwezo wa kudhibiti wale waliowapa madaraka. Pia katiba ya ki-demokrasia huweka misingi ya haki na usawa katika jamii kwa kuyapa maoni ya kila mwananchi uzito sawa kutegemea nguvu ya hoja na matakwa ya jamii kwa ujumla wake na kujenga uwiano kati ya maslahi ya sehemu mbali mbali ndani ya jamii. Katiba za aina hii hutungwa kwa maridhiano kwa kushirikisha jamii nzima ili kujenga udau na kuweka misingi ya wananchi kuridhia, kuipenda, kuihesimu, kuitii na kuilinda katiba hiyo. Maridhiano huzingatia maslahi ya kila sehemu ya jamii na wakati huo huo kutambua maslahi ya jamii pana. Ili Katiba iwe endelevu ni bora ipate ridhaa ya wananchi sio tu katika kuipigia kura ya maoni bali hasa katika kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa kuitunga. Kwa maana hii mchakato wa kutunga Katiba ni muhimu kuliko zao la mchakato kwa maana ya katiba yenyewe. Kwa maana hiyo vile vile kama tunataka Katiba bora na siyo bora Katiba sharti tuhakikishe kwamba mchakato ni shirikishi, jumuishi na wenye kufikia uamuzi kwa maridhiano. Ni jambo hili pekee ambalo huipa uhalali wa kisiasa na kuondoa uwezekano wa kuirekebisha kila mara. Katiba ya aina hii iliyotungwa kwa kwa maridhiano vile vile hujenga maridhiano na kuweka misingi ya maelewano na amani ndani ya jamii. Katiba ikitungwa kwa misingi ya ‘wengi wape’ hupanda mbegu ya kuibadilisha kila mara. Hii ni kwa kuwa wengi wa leo yawezekana wakawa wachache wa kesho na kwa sababu hiyo uwezekano wa kila kizazi kutaka kutunga Katiba upya utakuwa ni mkubwa! Matokeo yake ni ombwe la ki-katiba. Na hilo ndilo chimbuko la mitafaruku na migogoro isiyoisha katika nchi nyingi za ki- Afrika.
Maridhiano na changamoto zake
Kujenga maridhiano sio kitu chepesi. Inahitaji jitihada kubwa na uwezo wa kuwa na maono na upeo wa mbali, kuzingatia maslahi ya jamii ya muda mrefu, kuepuka ubinafsi na mtizamo finyu na kutetea haki za jamii kwa ujumla wake na hasa za wanyonge. Maridhiano hayajengeki kwa kugangania misimamo bali kwa kujali maslahi ya wote. Daima maslahi binafsi au ya tabaka fulani ni adui wa maridhiano. Je, maridhiano ni nini? Njia ya kutatua migogoro yenye wahusika au wadau wengi wenye maslahi yanayokinzana kwa kumshirikisha kila mdau. Maridhiano hufikiwa kwa nipe nikupe na siyo kutumia nguvu, ujanja au ghilba.
Maridhiano yana lengo la kupatanisha wadau sio kiwatenganisha. Kamwe maridhiano hayafikiwi kwa uwingi wa makundi bali kwa nguvu ya hoja zinazozingatia maslahi ya jamii kwa ujumla wake. Hivyo kwa kawaida maridhiano hayafikii maamuzi kwa kupiga kura ila kwa kufikia mwafaka.
Maridhiano huhitaji usikivu na uvumilivu wa hali ya juu, kila mhusika akitoa dukuduku zake na kila mmoja akiwasikiliza wenzake kwa kujaribu kujiweka kwenye mazingira yao.
Maridhiano hulenga kupata suluhisho linalokubalika na wote sio lile linalopendwa na wote au kundi fulani. Kila mhusika anaweza kuishi kwa matumaini chini ya suluhisho hilo.
Ni muhimu kushawishi kila mhusika ili kuepuka uwezekano wa wasioridhika kukwamisha utekelezaji wa makubaliano au kuyavunja kabisa.
Faida za maridhiano
Maridhiano yana faida kadhaa, ambazo ni pamoja na mosi, maridhiano huweka misingi imara ya kuheshimu na kufuata makubaliano; pili, maridhiano hujenga udau ndani ya nyoyo na fikra za wahusika wote wajione ni wamiliki wa makubaliano hayo; tatu, maridhiano huzaa suluhu bora kwa kuchambua, kushindanisha na kuunganisha hoja tofauti kupata yenye nguvu ya hoja; nne, maridhiano huwahakikishia wahusika wote kwamba wenzao wanajali maslahi yao na kuweka mazingira ya kuaminiana, kuheshimiana na kushirikiana katika migogoro mingine.
Tano, maridhiano hujenga mazingira ya kusikilizana na kuvumiliana katika jamii yenye mitazamo tofauti na saba; maridhiano huondoa majungu, fitina, ubabe na unafiki na badala yake kukuza ukweli, uwazi na ushawishi wa hoja hasa katika mambo ya msingi katika jamii.
Kutoka mchakato wa maridhiano hadi mpasuko
Akitangaza nia ya kuanzisha mchakato wa kutunga katiba mpya katika hotoba yake ya kufunga mwaka wa 2011 na kufungua 2012. Rais, pamoja na mengine, alisema yafuatayo: “Wananchi watapewa fursa ya kutosha ya kutoa maoni yao kwa uhuru na pawepo kuvumiliana kwa hali ya juu pale watu wanapotofautiana kwa mawazo. Pasiwepo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana wala kushinikizana. Naomba washiriki waongozwe kwa hoja badala ya jazba. Tukiwa na jazba, hasira na kushinikizana kamwe hatutaweza kutengeneza jambo jema. Na inapohusu Katiba ya nchi itakuwa hasara tupu. Haitakuwa endelevu na kulazimika kufanyiwa marekebisho mengi mwanzoni tu baada ya kutungwa.”
Hatimaye maneno haya yalitafsiriwa kama mdhumuni makuu katika sheria ya mabadiliko ya Katiba baadaye. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83(2012) – Sehemu ya pili (madhumuni) imeainisha, pamoja na mengine, masharti yafuatayo ikiagiza Tume ya Mabadiliko ya Katiba:
4(1) e – Kuweka utaratibu ambao utaruhusu wananchi kushiriki kwa uwazi na kwa mapana katika kutoa na kuwasilisha maoni yao kuhusu katiba. Na 4(1) j – Kuweka utaratibu utakaowezesha kujenga mwafaka wa ki-taifa katika masuala yenye maslahi kwa taifa wakati wa mchakato kuhusu Katiba.
Kwa tafsiri pana mchakato wa kutunga katiba mpya siyo tu ulikuwa na lengo la kuzaa katiba kama andiko ila pia ulinuia kufanikisha yafuatayo: kwanza, kupata katiba iliyotungwa kwa maoni huru ya wananchi yaliyotolewa kwa misingi ya usawa, uwazi na bila hofu au shinikizo lolote; pili, kutumia mchakato wa kutunga katiba kujenga maridhiano ya kisiasa na kijamii kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katriba, Mabaraza ya Katiba katika kila wilaya, Bunge Maalum la Katiba na hatimaye wananchi wote kupitia kura ya maoni; tatu, kufikia mwafaka wa kitaifa kuhusu mustakhabali wa muungano.
Lakini nne, ni kuweka misingi ya kujenga utamaduni wa kutii, kutetea na kuilinda katiba kwa hiari na moyo wa uzalendo na tano; kujenga tabia ya kuvumiliana katika majadiliano kwa kutegemea nguvu ya hoja badala ya kulazimisha hoja za nguvu katika kufikia uamuzi hasa wa kisiasa.
Maridhiano katika Tume na mitafaruku Bunge Maalumu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na wajumbe ambao mwanzoni mwa kazi yetu walikuwa na mitazamo na hata misimamo tofauti kuhusu mambo mengi yahusuyo katiba. Kuhusu Muungano, kwa mfano, mimi binafsi nilipendelea muundo wa serikali moja na baadhi ya Wazanzibari walipendelea Muungano wa ‘nkataba’ (mkataba) usiokuwa wa kikatiba. Lakini tangu mwanzoni wajumbe tulikubaliana kuongozwa na maoni ya wananchi kama msingi mkuu wa Katiba.
Tulijiwekea taratibu zilizosisitiza kuweka mazingira ya wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru na wengine wote (tukiwamo sisi) kuwasikiliza kwa umakini na utulivu. Mjumbe wa tume hakuruhusiwa kumwingilia mwananchi katika kutoa maoni yake ila tu pale alipotaka ufafanuzi wa jambo. Utaratibu mwingine ni kwamba tulikubaliana kufikia uamuzi kwa maridhiano. Kama kulitokea tofauti juu ya jambo lolote tulijadiliana, keelezana na kuelimishana mpaka tukakubaliana.
Mijadala hii mara nyingine ilikuwa mikali na kuzua hofu ya wajumbe kuvaana kwenye vikao. Kamwe hakukuwa na malumbano, mipasho au kejeli kama sote tulivyoshuhudia katika Bunga Maalumu. Kwa maana hiyo rasimu ya pili ilipitishwa kifungu kwa kifungu kwa maridhiano na bila mjumbe hata mmoja kutofautiana na wenzake. Hata mara moja hatukupiga kura na kuamua jambo kwa wingi au uchache wakura. Hata kama ingepigwa kura ingekuwa ya ‘ndio’ kwa asilimia moja.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya awali (Sura ya Ibara 20(3) na (4) ilimwagiza Mwenye Kiti wa Tume kuiwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalumu na kwa madhumuni ya kifungu hicho ilitamka kwamba “…Mwenyekiti na wajumbe wa Tume wanaweza kutoa ufafanuzi utakaohitajika wakati wa majadiliano katika Bunge Maalum” Kwa bahati mbaya kifungu hicho kilifutwa baada ya rasimu ya pili. Hii ndiyo ilikuwa dalili ya kwanza kwamba mchakato utavurugika kama mlivyoufuatilia. Tume ilikuwa imejiandaa sio tu kufafanua mambo lakini vilevile kusaidia kujenga maridhiano ndani ya Bunge Maalumu kama ilivyokuwa kwenye Tume. Kuondolewa kwa tume, kwa mfano, kemesababisha tafsiri potofu ya muundo wa shirikisho. Kilichopendekezwa na Tume katika hili ni kuanzisha dola la Muungano lenye mamlaka kamili juu ya serikali mbili zinazounda muungano. Kabla ya hapo Muungano umekuwa kama yatima na hivyo kukosa mamlaka ya kuutetea na kuulinda bila kukwazwa na mgongano wa maslahi. Hilo ndilo chimbuko shina la maradhi ya Muungano na ‘Kero za Muungano’ ni dalili tu za maradhi hayo. Bila kuwa na dola la Muungano hali hii itaendelea na hatimaye inaweza kuwa chanzo cha Muungano kuvunjika.
Jambo jingine lililochangia kuvurugika kwa Bunge kwa kiasi kikubwa ni hotuba ya Rais ya kuzindua Bunge hilo. Kwanza, katika hali isiyokuwa ya kawaida, badala ya Rais kuhutubia Bunge na kulizindua kwanza, zilifanyika hila za kupangua utaratibu huo wa kawaida ili Rais azungumze baada ya Mwenyekiti wa Tume ili akajibu hotuba ya Mwenyekiti na kuweka misimamo ya chama chake. Kuanzia hapo Bunge likagawanyika, wana-Ukawa wakatoka nje na mpasuko ndani ya taifa letu ukastawishwa. Hadi leo mpasuko huo unaendelea kukua. Mchakato ambao ungeziba nyufa alizoziona Mwalimu Julius Nyerere, kabla ya kifo chake sasa umezipanua.
Jambo la tatu lililovuruga mchakato lilihusu mamlaka ya Bunge Maalumu. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais aliwaambia wajumbe kama ifuatavyo: “Kile ambacho wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa msisite kufanya hivyo ili watanzania wapate katiba iliyo bora”. Kwa kutoa kauli hii Rais ki-msingi aliweka maoni ya wajumbe juu ya yale ya wananchi yaliyopokelewa na kuratibiwa na Tume kisheria na kuwasilishwa kwenye Rasimu ya pili. Wajumbe wa BMK hawakukusanya maoni ya wananchi na hawakuwa na mamlaka hiyo. Jambo hili ni kinyume cha lengo kuu la mchakato – kupata katiba iliyotungwa kwa maoni ya wananchi. Itakumbukwa kwamba jambo hili lilipelekwa mahakamani pamoja na ombi la kusimamisha bunge lakini hukumu ya Mahakama ilishindwa kuliamua kwa ubayana.
Jambo la nne lililovuruga mchakato ni kishindwa kwa mwenyekiti wa BMK kufuata dhamira na masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mjadala wene fujo, matusi, kejeli na ubaguzi ulijenga uhasama baina ya wa-Tanzania ndani na nje ya BMK. Uamuzi wote, ukiwamo wa kupitisha Katiba inayopendekezwa, ulifanyika kwa jazba, shinikizo na pengine ulaghai hasa wajumbe walipodaiwa kupiga kura wakiwa Hijja na wengine kukana kupiga kura ya ndiyo. Jambo hili la Katiba ya nchi ni jambo kubwa kiasi kwamba halistahili hata kidogo kufanya kwa mtindo ambao umejenga mgawanyiko katika jamii yetu na kutikisa maridhiano ya serikali ya kitaifa Zanzibar. Nilishangaa na kusikitika pale BMK liliposherehea kumaliza kazi kwa vifijo, gombesuku na mdundiko na miduara. Na niliduwaa zaidi pale akina mama waliposhona sare za makenzi wakisherehekea kushindwa kufikia malengo tuliyojiwekea kama taifa la kupata Katiba yenye ridhaa ya wote. Badala ya kusikitika kwa kushindwa kufikia malengo yetu tukasherehea kupata katiba kwa mgawanyiko wa Taifa letu! “Watu wa ajabu sana…” angestaajabu Mwalimu Nyerere!
Ni nini kifanyike sasa?
Hatua inayofuata ni ya Kura ya Maoni juu ya Katiba inayopendekezwa. Hadi sasa haijulikani kama kura hiyo itapigwa mwishoni mwa Aprili kama alivyotamka Rais. Mpaka sasa daftari la wapiga kura halijaboreshwa na hatua muhimu ya kulihakiki ni kama imeachwa kiasi kwamba kura itapigwa siku moja baada ya uandikishaji. Vile vile sheria imetoa muda wa elimu ya umma wa miezi miwili na kampeni ya mwezi mmoja. Yakitimizwa haya yote na kutekelezwa kwa weledi na ukamilifu kama sheria inavyoagiza, kura haiwezi kufanyika kabla ya mwezi wa Julai. Tusije tukajikuta tunatunga Katiba kwa utaratibu wa kuvunja au kupindisha sheria kwa shinikizo la ‘lazima tupate Katiba ya Kikwete’. Maslahi ya muda mfupi yasiathiri ya muda mrefu na maisha ya taifa. Kwa vyovyote vile katiba iliyotokana na mitafaruku na mchakato ulioharibika haitufai.
Kura ya maoni iahirishwe ili tujitafakari na kujipanga upya. Kama alivyosema Rais Kikwete katika hotuba yake ya kufungua mwaka wa 2012: “Tukiwa na jazba, hasira na kushinikizana kamwe hatutaweza kutengeneza jambo jema. Na inapohusu Katiba ya nchi itakuwa hasara tupu. Haitakuwa endelevu na kulazimika kufanyiwa marekebisho mengi mwanzoni tu baada ya kutungwa.”
Kwa bahati mbaya au kwa maksudi hiyo ndiyo hali halisi inayotukabili kwa sasa. Kama taifa tunahitaji busara, hekima na ujasiri wa kutambua hili na kuchukua hatua zitakazotuwezesha kurejesha utangamano katika jamii na kujipanga upya kwenye jambo la msingi kama Katiba.
Makala haya yameandikwa na Profesa Baregu ambaye alikuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, anapatikana kwa simu 0787506381.
Chanzo:Raia Mwema