THOMAS MASHALI KUTAFUTIWA MBABE PASAKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 Bondia Salum Nassoro akipasha na kocha wake, Maneno Abdallah katika gym yao iliyopo Mazense Midizini.

 Promota wa mchezo huo, Haruna Musa katika picha ya pamoja na bondia, Salum Nassoro.

Kampuni ya Dippo Boxing Promotion ya jijini Dar inayoongozwa na promota, Haruna Musa imeandaa pambano la Uzito wa Kati ‘Middle Weight’ kati ya bondia Salum Nassoro wa Dar na Benson Mwakyembe wa Ruvuma mchezo utakaopigwa Siku Kuu ya Pasaka, Machi 28 mwaka huu.

Pambano hilo la kukata na shoka litapigwa kwenye uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma ambapo kwa mujibu wa promota huyo alisema kuwa mshindi wa siku hiyo atazichapa na bingwa wa Afrika  ‘WBF, Thomas Mashali.

Mabondia hao ambao kila mmoja alitamba kumchapa mwenzake, waliwataka mashabiki wa ndondi kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo ili waone ladha ya ndondi ya asili.

      

BENKI YA POSTA TANZANIA YAJENGA VYOO VYENYE THAMANI YA SH. MILIONI 4.7 KATIKA SHULE YA MSINGI MAKAMBI ILIYOPO MANISPAA YA SONGEA MKOANI RUVUMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Wanafunzi wa shule ya msingi ya Makambi iliyopo Kata ya Ndilima Litembo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakifurahia vyoo vya kisasa vilivyojengwa na Benki ya Posta Tanzania.
 Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya Posta, Noves Moses akiongea kwenye mkutano katika shule hiyo muda mfupi kabla ya kuzindua vyoo hivyo. 
 Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya Posta, Noves Moses akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua vyoo vyenye matundu 14, vitakavyohudumia wanafunzi 850 katika shule ya Msingi ya Makambi, Songea Mkoa wa Ruvuma, ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 4.7 kulia ni Meneja wa Oparesheni wa tawi la Songea, Simon Mlelwa.
Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya Posta, Noves Moses akiwa kwenye picha ya pamoja na walimu wa shule hiyo pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ya mtaa.

Na Mwandishi Wetu

MENEJA mahusiano na mawasiliano wa Benki Posta Tanzania, Noves Moses amelitaka suala la elimu bure liendane na mazingira mazuri ya kimiundo mbinu kwa wanafunzi pamoja na walimu wao ili kuifanya elimu hiyo kuwa bora zaidi.

Rai hiyo aliitoa jana wakati akizindua vyoo vya kisasa vya Shule ya Msingi ya Makambi iliyopo Kata ya Ndilima Litembo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ambavyo vimejengwa na Benki hiyo kwa thamani ya shilingi Milioni 4.7 ikiwa ni sehemu ya mchango kwa jamii katika kuboresha mazingira ya elimu.

Akizindua matumizi ya vyoo hivyo vyenye matundu 14, Noves alisema kuwa jamii na taasisi mbalimbali zinatakiwa zitambue kuwa suala la elimu bure linatakiwa liendane na uboreshwaji wa mazingira ya wanafunzi na walimu wawapo shuleni hapo.

Alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wadau wa elimu kulichukulia suala la elimu bure kama kigezo cha kutokuchangia sekta hiyo na baadala yake wanadai ni kazi ya serikali pekee jambo ambalo siyo sahihi katika uboreshaji elimu.

“Suala la elimu bure lisiwe kigezo cha wadau kushindwa kuichangia sekta hiyo kwani kufanya hivyo kunapelekea baadhi ya shule kushindwa kuwa na mazingira mazuri ya watoto kujisomea pamoja na walimu wao kutokuwa na morali ya kufundisha” alisema Meneja mahusiano .

Noves alisema kuwa Benki ya Posta Tanzania inafanya kazi kwa kiwango kikubwa na serikali hivyo imetoa misaada mbalimbali ya kijamii hasa kwa upande wa afya na elimu huku katika upande wa elimu wamechangia madawati na ujenzi wa vyoo bora vya kisasa kwenye shule mbalimbali hapa nchini .

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Kanisius Ngongi awali akitoa taarifa ya shule hiyo kabla ya kukabidhiwa vyoo hivyo alisema kuwa shule hiyo ina wanafunzi 850 na matundu ya vyoo yapo 14 na kuwa vyoo vyote vina maji ya kutosha.

Ngongi aliipongeza benki hiyo alisema kuwa shule hiyo kwa sasa imeshabadilika, mazingira yamekuwa bora kwa upande wa vyoo vya wanafunzi ambavyo kwa sasa hakuna shule ndani ya Manispaa hiyo yenye vyoo kama hivyo.


Mwalimu Ngongi alisema kuwa licha ya vyoo vya wanafunzi kuwa bora lakini bado kuna changamoto ya vyoo vya walimu maana vyoo walivyokuwa wakivitumia vimeshapoteza ubora wake na kuwafanya walimu hao kupata shida mahala pa kujisitili hivyo amewaomba wadau mbalimbali waweze kuchangia kama Benki ya Posta inavyojitolea.

SERIKALI KUSAMBAZA MADAKTARI BINGWA MAENEO YA PEMBEZONI IKIWEMO MKOA WA RUVUMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

dk kigwa9Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla akitoa ufafanuzi juu ya Wizara yake kuhakikisha itapeleka Madaktari bingwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo hospitali hiyo ya Mkoa wa Ruvuma wakati wa ziara yake aliyoifanya mapema Februari 13.2016.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto mjini Songea, Dkt. Hamisi Kigwangalla baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma na kituo cha afya cha Mjimwema kilichopo mjini Songea huku akiitaka mikoa ya pembezoni ukiwemo mkoa huo wa Ruvuma kuweka mazingira ya kuwavutia madaktari bingwa kufanya kazi katika mikoa yao.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Bw. Said Mwambungu amesema kuwa mkoa huo umeridhishwa na staili ya ziara ya kushtukiza na kwamba wanajitahidi kuboresha vituo vya afya vya Mjimwema Songea, Madaba na cha wilaya ya Namtumbo ili vipandishwe hadhi kuwa hospitali za wilaya.
Pia Dk. Kigwangalla alipata wasaha wa kutembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali hiyo na kujionea utendaji wa kazi huku akitoa wito katika suala la maboresho zaidi.
Imeandaliwa na Andrew Chale wa Modewjiblog, Ruvuma.

dk kigwa4

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla (katikati) akijiandaa kuingia kukagua utendaji wa kazi na vifaa ndani ya chumba cha upasuaji cha Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma wakati wa ziara yake hiyo Februari 13.2016.

dk kigwa

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla akijiandaa kuingia kwenye chumba cha upasuaji wakati wa ziara yake hiyo, aliyoifanya mapema Februari 13.2016.

dk kigws

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigwangalla akiangalia moja ya vitanda vinavyotumika katika upasuaji hospitalini hapo ambapo hata hivyo aliambiwa changamoto kuwa baadhi ya taa za vitanda hivyo kuwa na hitilafu wakati ziara hiyo mapema Februari 13.2016. (Picha zote na Andrew Chale,modewjiblog-Songea, Ruvuma)

KILWA YAAGIZA TANI 60 ZA CHAKULA CHA NJAA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

HALMASHAURI ya Wilaya Kilwa imeagiza tani 90 za mahindi mkoani Ruvuma kwa ajili ya kaya zilizoathiriwa na mafuriko.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, Twaib Mbasha aliyasema hayo alipozungumza na wajumbe wa Baraza la Madiwani lililofanyika jana.

Alisema halmashauri imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na tatizo hilo.
“Gari liko njiani likitokea mkoani Ruvuma linalosafirisha mahindi kuletwa wilayani hapa,” alisema.
Mbasha alisema ni vigumu kuwaacha wananchi hivi hivi bila ya kutoa msaada kwao, kwani hawakutegemea kama wangepatwa na mafuriko.

Alisema juhudi nyingine zilizochukuliwa ni kuwasiliana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu ili kupata vyakula, dawa na huduma nyinginezo wanazohitaji wananchi hao.
Madiwani walisema hali si nzuri kwa kata zote, zilizopata mafuriko mwezi uliopita, kwani zinahitaji chakula na kuna hatari ya kutokea magonjwa ya milupuko.

Diwani wa Nanjilinji, Ally Yusufu alisema ekari 3,875 za mashamba ziliathiriwa na mafuriko ya Januari 22 hadi 26 mwaka huu.
Mazao ya chakula yaliyoathiriwa kwenye ekari hizo ni ekari 1,675 za mahindi, 207 mpunga, ekari 88 mtama, 144.5 muhogo, 1755 ufuta na ekari tatu za migomba.

Alisema kaya zilizoathirika ni 771 zenye watu 3,084. Watu hao hawana mahala pa kuishi na sasa wanaishi kwa majirani, marafiki, ndugu na jamaa.
CHANZO: HABARI LEO.

CCM YATAKA MAGUFULI AUNGWE MKONO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais Dk. John Magufuli.
Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma kimewataka wanachama wake kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli, katika kupambana na ufisadi na kuwabana wakwepa kodi.
 
Rai hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho, wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi, wakiwamo wanachama wa chama hicho kwenye maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM, yaliyofanyika katika kata ya Subira, mjini hapa. 
 
Mwisho alisema kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk. Magufuli, amesaidia kwa kiasi kikubwa kurudisha imani kwa Watanzania na kuifanya CCM kupendwa na kuwa na nguvu zaidi.
 
“Inashangaza kuona baadhi ya wanachama ambao waligombea nafasi mbalimbali za uongozi kipindi cha uchaguzi mkuu mwaka jana kwa bahati mbaya majina yao hayakupitishwa kwenye kura za maoni, wamekuwa mstari wa mbele katika kuikosoa serikali. Hiyo inaonyesha walivyo dhaifu na wachanga kisiasa,” alisema.
 
Kutokana na hali hiyo, alitoa onyo kali kwa wagombea hao walioshindwa na kuendeleza makundi, migogoro na kuwa mstari wa mbele katika kupinga na kukwamisha shughuli za maendeleo.
 
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Taqnzania (UWT), Kuruthum Mhagama na katibu wake, Chiku Masanja, waliwashukuru wanawake kwa kuichagua na kuipa ushindi CCM.
 
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Juma Mpeli, alisema ajenda ya uchaguzi imekwisha kilichobaki ni chama kuisimamia serikali katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ikiwamo kuhakikisha mikopo inatolewa kwa makundi ya vijana na wanawake, kufutwa kwa ushuru mdogo mdogo, kushughulikia madai ya watumishi na kuimarisha chama katika ngazi zote.
CHANZO: NIPASHE

WALIMU WATAKIWA KUCHAPA KAZI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BAADA ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini kufanya vibaya katika matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015 kwa kushika mkia mkoani Ruvuma, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Sigsbert Kaijage amewataka walimu kuongeza bidii katika ufundishaji ili kuondoa aibu hiyo kubwa.
Mbali na hilo, Kaijage aliwataka wanafunzi, walimu, wazazi na walezi wilayani humo kushirikiana ili kuinua kiwango cha taaluma kwa lengo la kufikia malengo ya Mpango maalum wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Kaijage alitoa mwito huo hivi karibuni wakati akizungumzia kufanya vibaya kwa shule za halmashauri hiyo jambo lililoitia aibu kubwa kwa kuwa ni mara ya kwanza Halmashauri ya Wilaya ya Songea kushika mkia.
Alisema iwapo kila mmoja kuanzia mtoto, mwalimu na mzazi watachukua hatua stahiki na kila mmoja kutimiza wajibu wake itasaidia kufikia kwa malengo yaliyoelekezwa na serikali badala ya jukumu hilo kuliachia serikali.
Kaijage aliwataka wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutumia muda mwingi kwa ajili ya kujisomea na kuepuka kushiriki katika vitendo vibaya vinayoweza kuchangia kukatisha ndoto za maisha yao.
 CHANZO : HABARI LEO.

WAKULIMA WA MAHINDI 'WAILILIA' SERIKALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAKULIMA wa mahindi wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali kuongeza fedha kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea ili wanunue mahindi mengi kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017.
Wakulima hao walisema kutokana na hali ya hewa ya mwaka huu, hasa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika maeneo mkoani Ruvuma, wana imani uzalishaji utakuwa mkubwa, ikilinganisha na msimu uliopita.
Walisema ni vyema sasa serikali ikaanza kutafuta fedha za kutosha kwa ajili ya maandalizi ya ununuzi wa mazao yao, kwa kuwa viongozi wa serikali wanapita kwa wakulima na kuwahamasisha waongeze juhudi, jambo lililoungwa mkono na wakulima wengi wa mkoa huo.
Mkazi wa kijiji cha Mlilayoyo, Joseph Ngonyani alisema wakulima wengi wameitikia mwito wa viongozi unaotaka kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara mashambani.
Hata hivyo, wasiwasi wao mkubwa ni kama serikali itanunua mazao yao hasa mahindi, zao ambalo ni tegemeo kubwa la kiuchumi.
Robet Mapunda wa kijiji cha Hanga alisema katika msimu wa 2013/2014 na 2015, wakulima wengi walilazimika kuuza mahindi yao kwa hasara kutokana na utaratibu uliotumika wa NFRA kuwatumia mawakala kwenda vijijini kununua mahindi kwa bei ndogo ya Sh 200 na wao kuizuia serikali kwa Sh 500 hadi 550 kwa kilo.
Aliongeza kuwa kutokana na utaratibu huo, hakuna mkulima aliyenufaika na kilimo, badala yake mawakala ndiyo walifaidika na kuwaacha wakulima wengi wakiwa masikini.
Mapunda alisema wakulima walilazimika kuuza kwa bei ya ‘kutupa’ kwa vile walishindwa kupata nafasi ya kupeleka moja kwa moja katika vituo vilivyowekwa na NFRA, kwani wachache ndiyo waliopata nafasi hiyo jambo lililowaumiza wakulima wa mahindi katika maeneo mbalimbali mkoani Ruvuma.
 CHANZO ; HABARI LEO.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa