JKT Mlale yakabidhi madawati

JESHI la Kujenga Taifa (JKT), Kikosi cha 842 KJ Mlale kilichopo wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kimekabidhi madawati 1,074 kukabiliana na upungufu katika jimbo la Peramiho na Madaba.
Madawati 534 yalikabidhiwa kwa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama na mengine 540 yalikabidhiwa kwa Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama kwa ajili ya halmashauri ya wilaya ya Madaba na yatasambazwa katika shule zenye upungufu wa madawati.
Akikabidhi madawati hayo jana, Mkuu wa Kikosi cha 842 Kj, Meja Absolomon Shaushi alisema madawati hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuzitaka taasisi za serikali, mashirika na watu binafsi kusaidiana na serikali kupunguza uhaba uliopo ili watoto wasome vizuri.
Shaushi alisema kikosi kilipewa kazi ya kutengeneza madawati kwa ajili ya kukabiliana na upungufu uliopo kwa shule za msingi na hadi sasa kazi hiyo inaendelea vizuri kutokana na morali ya hali ya juu waliyonayo vijana hasa ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa waathirika wa uhaba wa madawati kwenye shule walizosoma.
Alisema kikosi kimejipanga vyema kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa kuzingatia ubora unaotakiwa na kuziomba taasisi nyingine ambazo ziko tayari kumuunga mkono Rais Magufuli katika suala hilo kukitumia Kikosi cha Mlale JKT ambacho kina uwezo mkubwa katika utengenezaji wa madawati na samani nyingine kama vile milango, meza kwa ajili ya ofisi, vitanda na makabati.
Chanzo Na Habari Leo
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa