PINDA ATOA AGIZO UCHAGUZI MKUU 2015

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewataka Watanzania wasikubali kuchagua viongozi wanaotafuta uongozi kwa kutumia fedha kwani zinaweza kuleta machafuko.
Alisema hayo jana wakati wa ibada maalumu ya kumsimika Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Ruvuma, Amon Mwenda kwenye kanisa hilo la Usharika wa Songea iliyohudhuriwa na mamia ya waumini na viongozi mbalimbali.
“Ndugu zangu ninawaambia kuwa msigeuze uchaguzi kuwa mtaji, bali tuzingatie taratibu na sheria za uchaguzi ambazo ndiyo mwongozo unaoweza kutusaidia.
“Ninawasihi wananchi wawe makini na viongozi wanaopenda kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Kama mtu ana nia ya kweli ya kuongoza ni kwa nini atumie fedha ili kupata nafasi ya uongozi?” alisema na kuongeza:
“Tatizo ni kwamba hata wananchi hivi sasa wanakubali kupokea kile kinachotolewa na wagombea. Atakuja huyu atakupa hiki na mwingine naye atakupa kile, lakini ujue akiingia madarakani anaanza kurudisha haraka vile alivyowagawia.”
Aliwaomba viongozi wa dini na waumini kuendelea kuliombea taifa ili Mungu aliepushe na janga la watu kupenda rushwa.
Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea mchakato wa kupata Katiba Mpya ili wajumbe wote warejee ndani ya Bunge na kuikamilisha kazi waliyoianza.
Alisema Watanzania kwa sasa hivi wanahitaji kumwomba Mungu ili waendelee kuwa na amani.
Waziri Mkuu pia aliwataka Watanzania kujikita zaidi katika kilimo ambacho kitaweza kuwakomboa na kuondoa umaskini unaowakabili.
Alisema kila mwananchi anapaswa kufanya kazi kwa bidii ili aweze kumudu maisha yake ya kila siku akitolea mfano wa shughuli za kilimo na ujasiriamali badala ya kusubiri kusaidiwa.
Waziri Pinda alisema Dayosisi mpya ya Ruvuma inapaswa kuweka mipango yakinifu ya maendeleo ambayo itaweza kuisaidia Serikali kupunguza changamoto zilizopo kwa kuanzisha miradi ya elimu, afya na shughuli mbalimbali za kijamii.
Awali, akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mwenda alisema dayosisi mpya ya Ruvuma imezaliwa katika kipindi chenye changamoto nyingi za kidunia na utandawazi ukiwamo mmomonyoko mkubwa wa maadili.
Hata hivyo, akiainisha malengo ya dayosisi hiyo ambayo anakuwa Askofu wake wa kwanza, Askofu Mwenda alisema mbali ya kufundisha neno la Mungu, dayosisi hiyo itahimiza ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na akiba ya chakula cha kutosha.
Alisema watashirikiana na Serikali na wadau wa ndani na nje kutoa huduma za kijamii hasa elimu na afya.
Aliahidi kukabiliana na changamoto za sasa ambazo alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa, mauaji ya albino, unajisi wa watoto na ubakaji wa wanawake.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa alisema Kanisa lingependa kupata viongozi ambao ni wacha Mungu.
Askofu Malasusa alisema inashangaza kuona kuna baadhi ya watu wanagombea nafasi za uongozi lakini hawana mapenzi na Mungu aliyewaumba watu anaotaka kuwaongoza
Chanzo:Mwananchi

PSPF YAZAWADIA MADAWATI 90 KWA SHULE ZA TUNDURU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mfuko wa Pensheni kwa Umma (PSPF)
Mfuko wa Pensheni kwa Umma (PSPF) umetoa msaada wa madawati 90 yenye thamani ya shilingi milioni tano kwa ajili ya kusaidia kupunguza tatizo la madawati katika baadhi ya  shule za msingi za Wilaya ya Tunduru.
 
Akikabidhi msaada huo jana, Mwakilishi wa mfuko huo Mkoa wa Ruvuma, Deogratius Njuu, alisema, PSPF ni mdau mkubwa wa elimu wamegushwa na tatizo hilo hivyo wameona wasaidiane na halmashauri hiyo ili kupunguza tatizo hilo.
 
Njuu ameongeza kuwa, mfuko huo unaamini kuwa taifa lolote lenye maendeleo lazima libebwe na elimu na ndiyo maana nao wamepanga kusaidia katika kuinua kiwango cha elimu katika maendeleo mbali mbali nchini.
 
Aidha, amewashauri kuyatunza madawati hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kuwasaidia wanafunzi wote.
 
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini, Ramo Makani, amewapongeza PSPF kwa kutoa msaada huo kwa kuwa utasaidia kupunguza tatizo la  madawati na kuwataka wadau wengine watakao sikia waige mfano mzuri na bora  uliofanywa na mfuko huo.
 
Alisema, bado halmashauri inakabiliwa na changamoto nyingi kama upungufu wa madawati ambapo watoto wa shule za msingi wanakaa chini, upungufu wa matundu ya vyoo, meza, viti pamoja na miundombinu, hivyo amewaomba watu wenye uwezo wasaidiane na halmashauri kutatua matatizo hayo. 
 
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Kenneth Haule, alisema  kuwa halmashauri hiyo ina upungufu wa madawati 4537 ili kufanikisha utoaji elimu bora kwa watoto ni muhimu kuwapo kwa miundombinu na samani za kutosha zenye viwango kwa wanafunzi na walimu.
 
Alisema, wilaya hiyo inaupungufu mkubwa wa miundombinu na samani za kielimu vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, vyoo  pamoja na madawati ambapo jitihada kubwa za kupunguza tatizo hilo kwa kushirikiana na serikali kuu na jamii husika bado zinaendelea  kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi  wanaosajiliwa kila mwaka.
 
Aidha, alisema bado wilaya ina upungufu mkubwa wa samani za shule hivyo ameomba waendelee kusaidia kila wanapopata fursa ili kuendeleza sekta ya elimu nchini.
CHANZO: NIPASHE

JK AWAHAKIKISHIA WAKULIMA BEI YA MAHINDI 500/-KWA KILO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete amewahakikishia wakulima wa zao la mahindi mkoani Ruvuma  kuwa serikali itanunua mahindi yote kwa Sh. 500 kwa kilo badala ya Sh. 450.
Alisema hayo wakati akihutubia mamia ya wakazi wa manispaa ya Songea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Majimaji mjini hapa.

Alisema kuwa mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa saba inayoongoza kwa kilimo cha zao la mahindi hivyo serikali lazima iwaunge mkono kwa kuhakikisha kuwa mahindi yote yaliyolimwa katika msimu wa mwaka huu yananunuliwa yote na fedha ya kununulia mahindi hayo lazima itapatikana.

Alisema kwa vile kwenye Ghala la Hifadhi la chakula la Taifa (NFRA) mkoani Ruvuma mahindi yamefurika, ni lazima magari ya jeshi yatumike kusafirisha mazao ili kuhakikisha kuwa yanatolewa kwenye ghala kuu na kupata nafasi ya kupokea mahindi mapya yatakayoanza kununuliwa katika msimu unaotarajiwa kuanza Agosti mosi, mwaka huu.

“Ndugu wananchi dhamira yangu ya kufanya ziara katika mkoa wenu ni kutaka kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo na kuwahamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kusukuma gurudumu la Taifa.”alisema Kikwete.

Alisema kuwa amefurahishwa na kazi iliyofanywa na wakulima pamoja na NFRA  kwa kununua na kuhifadhi mahindi vizuri na kuondoa hofu ya  kuwapo njaa Tanzania.

Akizungumzia ujenzi wa barabara za manispaa kwa kiwango cha rami, Rais Kikwete alimuagiza Waziri wa Miundombinu Dk. John Magufuli kuhakikisha barabara ya kutoka Songea Girls hadi njia panda ya Ndilimalitembo inajengwa kwa kiwango cha lami kufikia mwakani.

Aidha amemuagiza Mkuu wa Mkoa huo, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na manispaa pamoja na wenyeviti wa Halmashauri kuhakikisha kuwa shule zote za sekondari za serikali zinakuwa na maabara ili kuongeza idadi kubwa ya wanafunzi wa masomo ya sayansi .

Rais Kikwete alizindua ghala jipya la wakala wa  NFRA lenye uwezo wa kuhifadhi tani 5000, mradi wa nyumba 18 za bei nafuu za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na  ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
 
CHANZO: NIPASHE

RAIS KIKWETE AFUNGUA OFISI ZA TAKUKURU MKOA WA RUVUMA



Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kufungua rasmi jengo la ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Ruvuma jana mjini Songea.
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na kaimu Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Bibi Mary Mosha wakifunua kitambaa katika jiwe la msingi wakati wa ufunguzi wa jingo la ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma jana. Rais Kikwete yupo katika ziara ya kikazi  ya wiki moja mkoani Ruvuma
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipanda mti wa kumbukumbu wakati wa ufunguzi  rasmi wa ofisi za taasisi ya kuzuia rushwa TAKUKURU mkoa mjini Songea jana. Kushoto ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Mary Mosha. Picha na Fredy Maro, IKULU


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

RAIS KIKWETE AZINDUA RASMI NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU ZA NHC SONGEA LEO

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikata utepe kufungua rasmi nyumba zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa NHC huko Mkuzo, wilayani Songea mjini mkoani Ruvuma leo. Kutoka kushoto ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi Prof.Anna Tibaijuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Bwana David Misonge Shambwe, na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bwana Said Mwambungu.
Ris Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akifunua jiwe la msingi wakati wa ufunguzi wa nyumba zilizojengwa kwa gharama nafuu na Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) huko Mkuzo wilayani Songea mjini Mkoani Ruvuma leo.Kushoto ni kaimu Mkurugenzi wa NHC Bwana David Misonge Shambwe na wwapili kushoto ni Waziri wa Ardhi Nyumba na makazi Prof.Anna Tibaijuka. Picha na Freddy Maro.

DC TUNDURU AMPONGEZA MWEKEZAJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
MKUU wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande NalichoMKUU wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho, amempongeza Mwekezaji wa nyumba ya kulala wageni ya Peramiho, Faustin Chale kwa uwekezaji alioufanya wilayani hapo.
Alisema ujasiri wa mwekezaji huyo wa kutumia mkopo wa sh milioni 100 kwa ajili ya mradi wa nyumba hiyo ni jambo jema alilodai kuwa litapunguza adha ya malazi kwa wageni wakati wa sherehe za kimkoa na ziara za viongozi wa kitaifa.
Nalicho alisema hayo jana alipozungumza na Tanzania Daima huku akiwataka wananchi wengine kuiga mfano wa mdau huyo wa maendeleo.
Alisema mwekezaji huyo mzawa ni mtumishi wa serikali hivyo anastahili pongezi kwa aina hiyo ya uwekezaji wa gharama kwa ajili ya shughuli za maendeleo huku wengine wakiogopa kukopa na kuwekeza wilayani humo kwa madai ya miundombinu mibovu ya barabara.
Aliwataka watumishi wa serikali kutumia fursa ya kufunguka kwa barabara kutoka Mtwara kupitia Tunduru na kutoka Tunduru hadi Songea itakayojengwa kwa kiwango cha lami mapema mwaka huu kujiwekea vitega uchumi vitakavyowasaidia baada ya kustaafu.
Kwa upande wake mmiliki wa nyumba hiyo, Faustin alisema asili ya mafanikio na maendeleo yake ni kukopa hivyo amewashauri watumishi wengine nao kuandaa maisha yao kwa kuweka vitega uchumi badala ya kutegemea fedha za kiinua mgongo.
Mradi huo ulifunguliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Rachel Kassanda wakati mwenge huyo ulipopita wilayani Tunduru mwishoni mwa wiki.
Chanzo:Tanzania Daima 

MWENYEKITI WA CHADEMA KANDA YA KUSINI AJIUZULU WADHIFA WAKE



MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya  kusini  ambaye pia ni Mchungaji  wa Kanisa la Avangelisitic Assemblies of God Tanzania(EAGT),Joseph Matare  amejiuzulu nafasi yake hiyo kutokana na Kanisa lake hilo Kuagiza Wachungaji wake ambao ni Viongozi wa  Vyama vya Siasa kuachana na Nafasi zao za Kisiasa.

 Joseph Matare akizungumza na Waandishi wa habari Mjini Songea amesema kuwa ameamua kujuzulu Nafasi yake ya Uongozi wa  CHADEMA Kanda ya Kusini inayojumuisha Mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma kufuatia  Kanisa lake katika  Mkutano wake wa Kanda kuagiza Wachungaji wake wote ambao ni Viongozi wa Kisiasa kuachia nafasi zao na badala yake wasimamie Kazi ya Mungu  Katika Makanisa yao.


 ‘Kufuatia maagizo  ya Mkutano huo wa Kanisa uliofanyika Njombe nimeamua kutii na  leo tarehe 10 Julai  2014 nimeamua kujiuzulu  na  Katibu wangu Mkuu Dr Wilbroad Slaa nilimjulisha tangu tarehe 04 Juni mwaka huu’ alisema  Matare katika taarifa yake ya kujiuzulu.

 Anafafanua kuwa muda  wa Viongozi wa Kanda ulikuwa ni wa muda na wa mpito hadi  uchaguzi wa Kanda utakapopita  ambao ulipaswa kufanyika Juni 2014 na kwamba muda umeongezwa hivyo ameona aheshimu  maagizo yaliyomuweka madarakani.

 Hata hivyo Matare anasema kuwa anawatia moyo Makamanda wote wa CHADEMA  waliobaki kuendelea kupigania Nchi ili iondokane na uovu  unaotendeka sasa na kwamba Mungu atakuwa nao wale wote wanaotafuta haki kwa ajili ya Wananchi walio wengi.

 Anasema  kuwa ameondoka bila kuwa na Ugomvi na Kiongozi yeyote wa CHADEMA   hivyo wataendelea kushirikiana kutafuta  haki akiwa Mwanachama wa Kawaida na Mchungaji.

 Matare ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT  Mkuzo la Mjini Songea la Mkoani Ruvuma  amesema kuwa anatambua juhudi za Viongozi wa CHADEMA katika kupigania haki za Wananchi na Wabunge wote wa CHADEMA katika kupigania haki na kwamba ipo siku Mungu atawalipa ujira wa kazi wanayofanya.

 Anasema kuwa Mungu anatambua kazi  nzito wanayofanya Viongozi wa CHADEMA ambayo amesema ni ya kutafuta Ukombozi kamili wa Nchi na itakuwa  ni uendawazimu kubeza kazi hiyo.


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

'MSIHIFADHI WAHAMIAJI HARAMU'

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
KIONGOZI wa mbio za mwenge wa uhuru, Rachel Kassanda, amewataka Watanzania kuacha tabia ya kuwahifadhi wahamiaji haramu, kwani kwa kufanya hivyo ni kuhatarisha amani na usalama wa nchi.
Akizungumza baada ya kuzindua nyumba ya Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Ruvuma, Kassanda aliwalaumu wakazi wa maeneo mbalimbali ya mpakani mkoani hapa kwa kuiweka rehani amani na usalama wa nchi bila sababu za msingi.
Alisema uhamiaji pekee haiwezi kufanya kazi bila kushirikiana na wananchi, hivyo wanapaswa kusaidia kwa kutoa taarifa muhimu za kiuhamiaji na kuwezesha udhibiti matukio ya kihalifu.
Alisema mkoa huo ndio mapitio ya makundi ya wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Somalia wanaoelekea kusini mwa Afrika, hivyo wananchi wakitoa msaada kwa maofisa wa uhamiaji wanaweza kukomesha hali hiyo.
Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Ruvuma, Koku Lwebandiza, aliishukuru serikali kwa kuwezesha kujengwa kwa nyumba hiyo ambayo  imegharimu sh milioni 434.
Chanzo:Tanzania Daima 

OFISI YA RAIS, TUME YA MIPANGO YAKAGUA MRADI WA MAKAA YA MAWE NGAKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 Majiko maalum yanayotumia mkaa uliotokana na makaa ya mawe  kwa ajili ya kupikia majumbani.
 Viongozi na Maofisa kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango na NDC wakiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa Kampuni ya TANCOAL ndani ya mgodi wa makaa ya mawe. Kampuni ya TANCOAL ndiyo inayohusika nauchimbaji wa makaa ya mawe katika Mradi wa Mkaa ya Mawe Ngaka.
Mtaalam wa Kudhibiti Ubora, Bw. Boscow R. Mabena  akitoa maelezo namna ambavyo Coal Briquett Machine(Pichani) hutumika kubadili makaa ya mawe kutoka hali yake ya mwanzo baada ya kuchimbwa na kutengenezwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Picha na: Thomas Nyindo, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.

WAFANYABIASHARA WAKATAA KUKATWA 20

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WAFANYABIASHARA wa kampuni za ununuzi wa kahawa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Ruvuma, wamekataa kuendelea kukatwa sh 20 kwa kila kilo ya zao hilo kuchangia mfuko wa ununuzi wa dawa za kuthibiti vidung’ata.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima Jumatano, baadhi ya wafanyabiashara hao (majina yamehifadhiwa) walidai kuwa fedha zinazokatwa kwa ajili ya kuchangia mfuko huo zinatumika kwa manufaa ya wajanja wachache kwa sababu ugonjwa huo umetoweka miaka mitatu iliyopita.
Walisema fedha zilipangwa kukatwa kipindi cha dharura kwa ajili ya kulinusuru zao hilo lisishambuliwe na ugonjwa wa vidung’ata, lakini sasa wamegeuza sheria licha ya ugonjwa huo kutoweka.
“Suala linalotakiwa ni kukaa mezani kati ya halmashauri na wafanyabiashara wa kahawa badala ya kutumia ubabe kukata fedha hizo na kufanya urasimu katika utoaji wa vibali vya kununulia zao hilo kwa sisi tunaopinga suala hilo,” alisisitiza mmoja wao.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga, alisema madai ya wafanyabiashara hao hayana ukweli, badala yake ametaka makato hayo yaendelee hadi ugonjwa huo utakapotokomea kabisa huku akibainisha kwamba baadhi ya maeneo yanasumbuliwa na vidung’ata.
Chanzo;Tanzania Daima

KURASA ZA MBELE NA NYUMA NA MBELE ZA MAGAZETI YA LEO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.




 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa