Home » » MBINGA YANUIA KUPUNGUZA AU KUONDOKANA NA UTEGEMEZI

MBINGA YANUIA KUPUNGUZA AU KUONDOKANA NA UTEGEMEZI

Mbinga. Ifikapo 2050, Wilaya ya Mbinga ina shauku ya kujiona inapunguza au inaondokana kabisa na utegemezi kutoka Serikali Kuu linapokuja suala la utekelezaji wa bajeti yake.

Shauku hii ilioneshwa siku chache zilizopita wakati wa mkutano uliowaleta pamoja wadau mbalimbali kutoa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025-2050.  

Kwa mwaka huu wa fedha (2024/25) mchango wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga ni asilimia 10.4 ya bajeti nzima ya Sh31.6 billion.

Tafsiri yake ni kuwa utegemezi kwa Serikali kuu ni asilimia 89.6.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mapato ya ndani yanachangia asilimia 17.5 ya bajeti nzima ya Sh48.1 billion.

Hii inamaanisha kuwa utegemezi wake kwa Serikali kuu ni asilimia 82.5.

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Kisare Matiku Makori alisema kuwa ufanisi katika ukusanyaji mapato ya ndani kwa Halmashauri za Mji wa Mbinga na Wilaya ya Mbinga utachochea utoaji huduma bora kwa wananchi.

“Lazima tuzitumie vizuri fursa tulizonazo kama tunataka kuongeza mapato yetu ya ndani,” alisema Mhe. Makori huku akitolea mfano wa madhari nzuri za Wilaya ya Mbinga jinsi zinavyoweza kuwa kivutio cha watalii.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Stuart Kuziwa alielezea haja ya kuendelea kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi.

“Tunapaswa kuja na mikakati itakayowapa wananchi na wawekezaji ujasiri wa kuwekeza katika maeneo mbalimbali na hivyo kuongeza makusanyo ya Halmashauri,” alisema Bw. Kuziwa.



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Bw. Joseph Rwiza alisema kuna haja ya wao kupunguza utegemezi kutoka Serikali kuu.

“Kwetu sisi tunaona suluhisho la kupunguza utegemezi kutoka Serikali kuu ni kutengeneza mazingira rafiki ya kuwa na uchumi jumuishi,” alisema Bw. Rwiza.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga John Ndimbo alisema kama Mbinga inataka kusimama yenyewe lazima ihakikishe inatumia ipasavyo rasilimali zake asilia.

“Tunapaswa kutumia ipasavyo fursa tulizonazo kama tunataka tusiwe wategemezi kwa Serikali kuu,” alishauri Askofu Ndimbo.
 



0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa