Home » » Serikali yaombwa kushirikiana na kampuni binafsi upimaji viwanja

Serikali yaombwa kushirikiana na kampuni binafsi upimaji viwanja

 Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeombwa kuona umuhimu wa kuchukuwa makampuni binafsi ya upimaji wa viwanja ili kuwarahisishia wananchi upatikanaji rahisi wa viwanja badala ya kutegemea halmashauri ifanye kazi hiyo peke yake, anaripoti Cresensia Kapinga, Songea.
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Namanyigu uliopo katika halmashauri ya Manispaa ya Songea Bw.Fidolin Malindisa wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye ofisi ya afisa mtendaji wa mtaa huo.
Malindisa alisema kuwa mpango wa mzuri wa serikali wa kupima viwanja kupitia makampuni binafsi umeonekana kuwa na matunda mazuri kwa wakazi wa manispaa ya Songea baada ya mtaa wake kuibua mradi wa upimaji wa viwanja 3000 ambao umekuwa na mafanikio makubwa kwa zaidi ya asilimia 75.
Alieleza zaidi kuwa kila mkazi wa mtaa huo anayehitaji kuwa na kiwanja hawezi kuwa na sababu ya kukosa kwani viwanja vilivyopimwa ni vingi na gharama yake ni ndogo tofauti na ilivyokuwa awali kwani wananchi wa mtaa wake wamehamasika kwa kiasi kikubwa na wana kiu ya kuondokana na makazi holela yaliyokuwa yanawabana hata kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.
"Nawashauri wananchi wa mitaa mingine na hata katika halmashauri zingine hapa nchini waige mfano wa mtaa wa Namanyigu ambako wananchi wamepimiwa viwanja vyao kwa gharama nafuu na itamsaidia kila mwananchi kufaidika kupitia ardhi yake mwenyewe,"alisema Malindisa.
Hata hivyo ameipongeza kampuni ya Ardhi Plan yenye makao makuu jijini Dar es Salaam kwa kufanya kazi nzuri ambayo imeonekana machoni mwa wakazi wa mtaa wa Namanyigu kwani viwanja 3000 tayari vimeshapimwa na kwa sasa hivi zinachongwa barabara kwenye maeneo ya viwanja vyote vilivyopimwa na kazi ya uchongaji itakapokamilika watamalizia kwa kupanda mawe na tayari kwa kila mwenye kiwanja atakabidhiwa eneo lake.
Aidha ameiomba halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakikisha kuwa inaunga mkono Kampuni ya Ardhi Plan kwamba kila mkazi aliyepimiwa kiwanja anapewa hati ya kiwanja mapema iwezekanavyo ili wananchi waanze haraka iwezekanavyo kujenga nyumba kwenye maeneo hayo ambayo tayari yameshapimwa

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa