Home » » WANANCHI MJI MBINGA WATAKIWA KUSHIRIKI MIRADI YA BOOST

WANANCHI MJI MBINGA WATAKIWA KUSHIRIKI MIRADI YA BOOST

Na Alex Nelson Malanga

Afisa Habari----Mji Mbinga

Mbinga. Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga wametakiwa kushiriki ipasavyo katika utekelezaji wa miradi ya BOOST yenye thamani ya Sh419.1 milioni kwa kutoa nguvu kazi.

Serikali kupitia mradi wa uboreshaji elimu ya awali na msingi (BOOST), imeipatia Mji Mbinga kiasi hicho cha fedha kwaajili ya ujenzi wa madarasa 15 na matundu 30 ya vyoo katika shule za msingi Beruma, Masumuni, Nazareth, Changarawe na Luhangai.

Akizungumza siku ya Ijumaa (Agosti 2) katika shule ya msingi Nazareth, Bw. Xavery Mwihava, Afisa Elimu Takwimu, Idara ya Elimu ya Awali na Msingi, Halmashauri ya Mji Mbinga, alisema kuwa nguvu za wananchi zitaokoa fedha ambazo zingetumika kuajiri vibarua.

Alisema badala ya kutafuta kibarua kufanya shughuli ndogo ndogo kama kusafisha eneo, kuchimba msingi, kusogeza maji na matofali, wananchi wanapaswa kufanya wenyewe ili pesa itakayookolewa isaidie shughuli nyingine za ujenzi.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetupatia pesa, shukrani yetu ni kwa sisi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi,” alisema Bw. Mwihava.

Bw. Mwihava aliye mwakilishi Afisa Elimu Awali na Msingi, Halmashauri ya Mji wa Mbinga, katika utambulisho wa miradi ya BOOST aliongeza: “Hii miradi ni yenu, hivyo mnapaswa kuonesha  uzalendo wa hali ya juu.|

Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kushirikiana na walimu, kamati ya shule na uongozi wa Serikali ya mtaa ili miradi itekelezwe kwa ubora zaidi.

“Inatakiwa tuimbe wimbo mmoja, haitapendeza wananchi kuwaachia walimu, kamati ya shule au serikali ya mtaa peke yao, ” alisisitiza.

Miradi ya BOOST itakayotekelezwa mwaka huu wa fedha ni ujenzi wa madarasa manne na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Changarawe (Sh106.2 milioni) na madarasa matatu na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Nazareth (Sh82.2 milioni).

Miradi mingine ni ujenzi wa madarasa matatu na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Masumuni (Sh82.2 milioni) na madarasa matatu na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Beruma (Sh82.2 milioni).

Pia mradi mwingine utakaotekelezwa ni ule wa ujenzi wa madarasa mawili ya mfano ya elimu ya awali na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Luhangai (Sh66.3 milioni).
 



0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa