CHAKULA CHASABABISHA VIFO VYA WATOTO WANNE WA FAMILIA MOJA.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusidedit Nsimeki

Iliyokuwa iwe sikukuu ya Idd el-Fitri yenye furaha na fanaka imegeuka kuwa sikukuu ya majonzi na maombolezo mazito kwa familia ya Salum Mumba mkazi wa kijiji cha Lugunga, wilayani Namtumbo baada ya kupoteza watoto wake wanne kwa mpigo kwa kile kinachosadikiwa kula chakula chenye sumu.

Mbali na watoto hao walioiacha familia katika majonzi yasioelezeka, watu wengine 13 wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Lusewa Wilayani Namtumbo na Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Ruvuma baada ya kula chakula hicho kinachodaiwa kuwa na sumu wakati wa sikukuu hiyo.


Habari zilizopatikana jana mjini Songea ambazo zilizibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusidedit Nsimeki, zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea Ijumaa wiki iliyopita majira kati ya saa 4:00 asubuhi na saa 7:00 mchana, katika kijiji hicho.

Watoto waliofariki ni Tazamio, Zidani, Ramadhani na Zahara wote watoto wa Salum Mumba, wakazi wa Kitongoji cha Tulieni B kilichopo katika Kijiji cha Ligunga.

Kamanda Nsimeki alisema siku hiyo kabla ya tukio, Salum Mumba,  alinunua samaki ambao aliwapeleka nyumbani kwake na alimkabidhi mke wake ambaye hakutaka kumtaja jina ili aandae chakula kwa ajili ya sikukuu ya Idd.

Alisema chakula kiliandaliwa na majira ya mchana wakati Mumba akiwa amekwenda msikitini kuswali, familia yake ilianza kula chakula hicho ambacho ni samaki na ugali na baada ya muda si mrefu, ghafla mtoto mmoja alianza kuumwa hali ambayo iliwafanya waanze kushtuka na kumsaidia na kwamba wakati wakimsaidia na kutaka kumpeleka katika kituo cha afya, alifariki dunia.

Alifafanua zaidi kuwa, haikuchukua muda mrefu mtoto mwingine alianza kuumwa naye baadaye alifariki dunia, wakati wamepata mshtuko, watoto wengine walifariki na kisha watu wengine 13 walianza kuumwa.

Kamanda Nsimeki alisema baada ya majirani kupata taarifa hizo waliwakimbiza katika Kituo cha Afya cha Lusewa kwa matibabu, lakini kati yao watoto sita hali zao zilikuwa ni mbaya na walihamishiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea kwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa ni Gairi Mumba, Zamoni Mumba, Fatuma Rashidi, Samidu Mumba, Asha Omary na Sharifa Mumba na watoto waliolazwa katika Kituo cha Afya cha Lusewa bado majina yao hayajapelekwa  ofisini kwake, lakini alisema kuwa hali zao zinaendelea vizuri.

Alisema polisi inamshikilia mtu mmoja ambaye hakutaka kumtaja jina ambaye atasaidia kufanikisha upelelezi wa tukio hilo.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi ya Hospitali ya Mkoa wa Ruvumaa, Dk. Benedictor Ngaiza, aliiambia NIPASHE jana mchana kuwa, juzi Ijumaa majira ya mchana alipokea wagonjwa sita kutoka Kituo cha Afya cha Lusewa wakiwa na hali mbaya baada ya kudaiwa kuwa  wamekula chakula kinachohofiwa kuwa na  sumu.

Dk. Ngaiza alisema mpaka sasa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo hali zao zinaendelea vizuri tofauti na walivyofika na kati yao wawili wanatarajiwa kuruhusiwa ambao ni Asha Omary na Sharifa Mumba.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Tulieni B, Isaya Juma, alisema tukio hilo limeleta mshtuko mkubwa kwa wakazi wa kijiji cha Lugunga na kwamba pamoja na kwamba taarifa ya tukio hilo waliipeleka polisi nao wanaendelea kumsaka muuza samaki wanaohofiwa kuwa na sumu na kwamba watatoa ushirikiano wa dhati kwa jeshi la polisi.
CHANZO: NIPASHE

Wananchi Ruvuma hawajui sheria za mazingira

Jitihada za Serikali  kutunza na kuendeleza vyanzo vya maji katika bonde la mto Ruvuma na pwani ya kusini ili kuboresha huduma 
ya maji huenda zikatatizwa na mgongano wa sheria na sera ya misitu, kilimo, ardhi na ile ya maji.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi mkoani Ruvuma umebaini kuwa wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji hawaelewi sheria za uhifadhi ardhi na sera mbalimbali ikiwepo kilimo kwanza pamoja na ile  ya wizara ya maji inayozuia kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye mabonde na  vyanzo vya maji.

Baadhi ya wakulima wa mbogamboga katika bonde la mto ruvuma,matogoro mjini Songea, wamesema wanashangazwa na 
baadhi ya viongozi kuzuia shughuli za kilimo katika bonde hilo wakati serikali  ikihimiza wakulima kujikita zaidi ktk kilimo cha umwagiliaji.

 Wamesisitiza kuwa sheria ya mazingira inayowabana kutokufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya mita 60 ili kutunza vyanzo vya maji inakwamisha utekelezaji wa sera ya kilimo kwanza hatua ambayo wamedai itaongeza umasikini kwa jamii inayotegemea kilimo cha mabondeni.

 Ofisa uhusiano wa bonde la mto Ruvuma na pwani ya kusini bw.Dickson Maganga amesema ofisi yake inatambua changamoto ya mgongano wa sera na sheria katika kuhifadhi rasilimali ya maji  ndio maana wameanzisha mpango shirikishi wa kutunza na kuendeleza rasilimali hiyo  kwa kuunda jumuiya za watumia maji katika mitaa ili kusaidia kueneza elimu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo na mabonde ya mito katika eneo hilo.

 Wakati serikali ikitekeleza miradi mbalimbali ya maji bado kumekuwepo na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mengi nchini  hali inayosababishwa na mabadilko ya tabia nchi pamoja na  shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika vyanzo vya maji zikiwepo kilimo,uchomaji 
wa mkaa na matofali,ufugaji na upasuaji wa mbao.

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa