JESHI la Kujenga Taifa (JKT), Kikosi cha 842 KJ Mlale kilichopo
wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kimekabidhi madawati 1,074 kukabiliana
na upungufu katika jimbo la Peramiho na Madaba.
Madawati 534 yalikabidhiwa kwa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama na
mengine 540 yalikabidhiwa kwa Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama kwa
ajili ya halmashauri ya wilaya ya Madaba na yatasambazwa katika shule
zenye upungufu wa madawati.
Akikabidhi madawati hayo jana, Mkuu wa Kikosi cha 842 Kj, Meja
Absolomon Shaushi alisema madawati hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais
John Magufuli la kuzitaka taasisi za serikali, mashirika na watu binafsi
kusaidiana na serikali kupunguza uhaba uliopo ili watoto wasome vizuri.
Shaushi alisema kikosi kilipewa kazi ya kutengeneza madawati kwa
ajili ya kukabiliana na upungufu uliopo kwa shule za msingi na hadi sasa
kazi hiyo inaendelea vizuri kutokana na morali ya hali ya juu
waliyonayo vijana hasa ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa waathirika wa
uhaba wa madawati kwenye shule walizosoma.
Alisema kikosi kimejipanga vyema kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa
kuzingatia ubora unaotakiwa na kuziomba taasisi nyingine ambazo ziko
tayari kumuunga mkono Rais Magufuli katika suala hilo kukitumia Kikosi
cha Mlale JKT ambacho kina uwezo mkubwa katika utengenezaji wa madawati
na samani nyingine kama vile milango, meza kwa ajili ya ofisi, vitanda
na makabati.
Chanzo Na Habari Leo
0 comments:
Post a Comment