Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan afunga Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa, Songea Mkoani Ruvuma


















RAIS SAMIA ATEMBELEA MAKUMBUSHO YA VITA VYA MAJIMAJI, SONGEA MKOANI RUVUMA






Matukio mbalimbali wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotembelea Makumbusho ya Vita vya Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 23 Septemba, 2024. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Makumbusho ya Vita vya Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 23 Septemba, 2024.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi wakati akielekea Songea mjini wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Ruvuma tarehe 23 Septemba, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiweka shada la maua katika kaburi la pamoja la Mashujaa wa Vita vya Majimaji walionyongwa na Wajerumani tarehe 27/02/1906 wakati wa Vita hivyo mjini Songea. Rais Dkt. Samia ameanza ziara ya kikazi mkoani Ruvuma ambapo atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoka kwenye moja ya nyumba ya utamaduni wa asili ya Wangoni iliyopo katika Makumbusho ya Vita vya Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 23 Septemba, 2024.

Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aanza Ziara ya Kikazi Mkoani Ruvuma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Songea kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma tarehe 23 Septemba, 2024.

MBINGA YANUIA KUPUNGUZA AU KUONDOKANA NA UTEGEMEZI

Mbinga. Ifikapo 2050, Wilaya ya Mbinga ina shauku ya kujiona inapunguza au inaondokana kabisa na utegemezi kutoka Serikali Kuu linapokuja suala la utekelezaji wa bajeti yake.

Shauku hii ilioneshwa siku chache zilizopita wakati wa mkutano uliowaleta pamoja wadau mbalimbali kutoa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025-2050.  

Kwa mwaka huu wa fedha (2024/25) mchango wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga ni asilimia 10.4 ya bajeti nzima ya Sh31.6 billion.

Tafsiri yake ni kuwa utegemezi kwa Serikali kuu ni asilimia 89.6.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mapato ya ndani yanachangia asilimia 17.5 ya bajeti nzima ya Sh48.1 billion.

Hii inamaanisha kuwa utegemezi wake kwa Serikali kuu ni asilimia 82.5.

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Kisare Matiku Makori alisema kuwa ufanisi katika ukusanyaji mapato ya ndani kwa Halmashauri za Mji wa Mbinga na Wilaya ya Mbinga utachochea utoaji huduma bora kwa wananchi.

“Lazima tuzitumie vizuri fursa tulizonazo kama tunataka kuongeza mapato yetu ya ndani,” alisema Mhe. Makori huku akitolea mfano wa madhari nzuri za Wilaya ya Mbinga jinsi zinavyoweza kuwa kivutio cha watalii.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Stuart Kuziwa alielezea haja ya kuendelea kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi.

“Tunapaswa kuja na mikakati itakayowapa wananchi na wawekezaji ujasiri wa kuwekeza katika maeneo mbalimbali na hivyo kuongeza makusanyo ya Halmashauri,” alisema Bw. Kuziwa.



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Bw. Joseph Rwiza alisema kuna haja ya wao kupunguza utegemezi kutoka Serikali kuu.

“Kwetu sisi tunaona suluhisho la kupunguza utegemezi kutoka Serikali kuu ni kutengeneza mazingira rafiki ya kuwa na uchumi jumuishi,” alisema Bw. Rwiza.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga John Ndimbo alisema kama Mbinga inataka kusimama yenyewe lazima ihakikishe inatumia ipasavyo rasilimali zake asilia.

“Tunapaswa kutumia ipasavyo fursa tulizonazo kama tunataka tusiwe wategemezi kwa Serikali kuu,” alishauri Askofu Ndimbo.
 



WANANCHI MJI MBINGA WATAKIWA KUSHIRIKI MIRADI YA BOOST

Na Alex Nelson Malanga

Afisa Habari----Mji Mbinga

Mbinga. Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga wametakiwa kushiriki ipasavyo katika utekelezaji wa miradi ya BOOST yenye thamani ya Sh419.1 milioni kwa kutoa nguvu kazi.

Serikali kupitia mradi wa uboreshaji elimu ya awali na msingi (BOOST), imeipatia Mji Mbinga kiasi hicho cha fedha kwaajili ya ujenzi wa madarasa 15 na matundu 30 ya vyoo katika shule za msingi Beruma, Masumuni, Nazareth, Changarawe na Luhangai.

Akizungumza siku ya Ijumaa (Agosti 2) katika shule ya msingi Nazareth, Bw. Xavery Mwihava, Afisa Elimu Takwimu, Idara ya Elimu ya Awali na Msingi, Halmashauri ya Mji Mbinga, alisema kuwa nguvu za wananchi zitaokoa fedha ambazo zingetumika kuajiri vibarua.

Alisema badala ya kutafuta kibarua kufanya shughuli ndogo ndogo kama kusafisha eneo, kuchimba msingi, kusogeza maji na matofali, wananchi wanapaswa kufanya wenyewe ili pesa itakayookolewa isaidie shughuli nyingine za ujenzi.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetupatia pesa, shukrani yetu ni kwa sisi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi,” alisema Bw. Mwihava.

Bw. Mwihava aliye mwakilishi Afisa Elimu Awali na Msingi, Halmashauri ya Mji wa Mbinga, katika utambulisho wa miradi ya BOOST aliongeza: “Hii miradi ni yenu, hivyo mnapaswa kuonesha  uzalendo wa hali ya juu.|

Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kushirikiana na walimu, kamati ya shule na uongozi wa Serikali ya mtaa ili miradi itekelezwe kwa ubora zaidi.

“Inatakiwa tuimbe wimbo mmoja, haitapendeza wananchi kuwaachia walimu, kamati ya shule au serikali ya mtaa peke yao, ” alisisitiza.

Miradi ya BOOST itakayotekelezwa mwaka huu wa fedha ni ujenzi wa madarasa manne na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Changarawe (Sh106.2 milioni) na madarasa matatu na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Nazareth (Sh82.2 milioni).

Miradi mingine ni ujenzi wa madarasa matatu na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Masumuni (Sh82.2 milioni) na madarasa matatu na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Beruma (Sh82.2 milioni).

Pia mradi mwingine utakaotekelezwa ni ule wa ujenzi wa madarasa mawili ya mfano ya elimu ya awali na matundu sita ya vyoo Shule ya Msingi Luhangai (Sh66.3 milioni).
 



TAKUKURU: WAANDISHI PIGENI VITA RUSHWA



Na Alex Nelson Malanga

Afisa Habari----Mji Mbinga

Mbinga. Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewataka waandishi wa habari wa Wilaya ya Mbinga kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya rushwa.

Akizungumza wakati wa kikao kazi na waandishi wa habari Jumatatu ya Julai 29, Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Mbinga Bw. Frederick Msae alisema waandishi wa habari wana jukumu la kuelimisha wananchi kuhusu haja ya kuchagua viongozi waadilifu.

“Waandishi wa habari mna uwezo wa kuwafikia wananchi kiurahisi. Tumieni vema kalamu zenu kuwaelimisha wananchi kuhusu haja ya kuchagua viongozi pasipo vitendo vyovyote vya rushwa,” alisema kamanda Msae.

Aliongeza: “Waandishi wa habari msipopiga kelele kuhusu rushwa wakati wa uchaguzi, wananchi watachagua viongozi ambao hawatakuwa na msaada wowote kwa jamii.”

Ni haja ya serikali kuona wananchi wanachagua viongozi ambao wataweza kuchanganua na kupambanua changamoto mbalimbali ambazo wanakumbana nazo katika jamii.

 “Viongozi wanaohitajika ni wale ambao watapatikana kwa njia ya haki na hivyo kuwa daraja kati ya wananchi na serikali katika mambo mbalimbali,” alisema Bw. Msae.

Bosi huyo wa TAKUKURU kwa ngazi ya wilaya alionya kuwa waandishi wa habari wasipokuwa mstari wa mbele katika kupiga vita rushwa, itaathiri imani ya hadhira yao.

Bw. Msae pia alieleza umuhimu wa waandishi wa habari kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa pindi vinapofanyika au vinapo pangwa kufanyika.

Hii, alieleza, itaisaidia TAKUKURU kuwashughulikia wahusika na hatimaye kuondoa vitendo vya rushwa katika wilaya ya Mbinga.

Pia, alisema waandishi wa habari kama kioo cha jamii, wanapaswa kuwa waadilifu kwa kutoa taarifa sahihi kwa umma pamoja na kuwanadi, pale inapobidi, wagombea wote pasipo upendeleo.

“Mnapaswa kutoa taarifa za wagombea wote bila upendeleo wowote na bila kupokea rushwa,” alihitimisha Bw. Msae.

 

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA ORYX WAGAWA MITUNGI YA GESI 1,050



Na Alex Nelson Malanga


Afisa Habari----Mji Mbinga


Mbinga. Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga kwa kushirikiana na Kampuni ya Gesi ya Oryx Tanzania jumanne (Julai 23) waligawa mitungi ya gesi 1,050 kwa wananchi wa Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma.


Ugawaji wa mitungi hiyo yenye thamani ya Sh45 milioni unalenga kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.



Kati ya mitungi ya gesi 1,050 iliyotolewa katika ukumbi wa One Pacific uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Mkoani Ruvuma, kampuni ya Oryx ilitoa mitungi 700 na Mhe. Judith mitungi 350.


“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa nishati safi ya kupikia imejidhatiti katika kuhakikisha tunaongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia,” alisema Mhe. Judith huku akiipongeza kampuni ya Oryx kwa mchango wake wa mitungi ya gesi 700.


Kupitia Mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), Serikali imedhamiria kuongeza kaya za watanzania zinazotumia nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 10 ya sasa mpaka asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.


Ikiwa ni sehemu ya jitihada za  kuongeza matumizi ya nishati safi, mpaka sasa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imesambaza mitungi ya gesi ya ruzuku 83,500 yenye thamani ya Sh3.5 bilioni, kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Nishati.



Kama hiyo haitoshi, aliongeza Mhe. Judith, mwaka huu wa fedha serikali imepanga kutoa mitungi 452,445 yenye thamani ya Sh10 bilioni.

“Lengo letu ni kupunguza gharama za nishati safi ya kupikia na kwa kufanya hivyo naamini tutachochea matumizi ya nishati hiyo,” alisema Mhe. Judith.


Agenda ya nishati safi ya kupikia ni muhimu sana kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu na kwa kutambua hilo Mhe. Rais Dkt. Samia amekua kinara katika kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.


Sifa hiyo ya Mhe. Rais haiishii Tanzania tuu, bali imevuka hadi mipaka ya nchi hii mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Hii inadhihirishwa na yeye kuzindua ‘programu’ ya nishati safi ya kupikia Afrika yenye lengo la kuleta mageuzi na kumkomboa mwanamke.


Uzinduzi huo ulifanywa mwishoni mwa mwaka jana huko Dubai, Falme za Kiarabu wakati wa Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28).


Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Bw. Araman Benoit alisema: “Tunataka jamii ya Tanzania iachane na nishati chafu ambayo sio mbaya kwa afya tuu, bali ni hatari kwa mazingira pia.”

 

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa