TAKUKURU: WAANDISHI PIGENI VITA RUSHWA



Na Alex Nelson Malanga

Afisa Habari----Mji Mbinga

Mbinga. Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewataka waandishi wa habari wa Wilaya ya Mbinga kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya rushwa.

Akizungumza wakati wa kikao kazi na waandishi wa habari Jumatatu ya Julai 29, Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Mbinga Bw. Frederick Msae alisema waandishi wa habari wana jukumu la kuelimisha wananchi kuhusu haja ya kuchagua viongozi waadilifu.

“Waandishi wa habari mna uwezo wa kuwafikia wananchi kiurahisi. Tumieni vema kalamu zenu kuwaelimisha wananchi kuhusu haja ya kuchagua viongozi pasipo vitendo vyovyote vya rushwa,” alisema kamanda Msae.

Aliongeza: “Waandishi wa habari msipopiga kelele kuhusu rushwa wakati wa uchaguzi, wananchi watachagua viongozi ambao hawatakuwa na msaada wowote kwa jamii.”

Ni haja ya serikali kuona wananchi wanachagua viongozi ambao wataweza kuchanganua na kupambanua changamoto mbalimbali ambazo wanakumbana nazo katika jamii.

 “Viongozi wanaohitajika ni wale ambao watapatikana kwa njia ya haki na hivyo kuwa daraja kati ya wananchi na serikali katika mambo mbalimbali,” alisema Bw. Msae.

Bosi huyo wa TAKUKURU kwa ngazi ya wilaya alionya kuwa waandishi wa habari wasipokuwa mstari wa mbele katika kupiga vita rushwa, itaathiri imani ya hadhira yao.

Bw. Msae pia alieleza umuhimu wa waandishi wa habari kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa pindi vinapofanyika au vinapo pangwa kufanyika.

Hii, alieleza, itaisaidia TAKUKURU kuwashughulikia wahusika na hatimaye kuondoa vitendo vya rushwa katika wilaya ya Mbinga.

Pia, alisema waandishi wa habari kama kioo cha jamii, wanapaswa kuwa waadilifu kwa kutoa taarifa sahihi kwa umma pamoja na kuwanadi, pale inapobidi, wagombea wote pasipo upendeleo.

“Mnapaswa kutoa taarifa za wagombea wote bila upendeleo wowote na bila kupokea rushwa,” alihitimisha Bw. Msae.

 

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA ORYX WAGAWA MITUNGI YA GESI 1,050



Na Alex Nelson Malanga


Afisa Habari----Mji Mbinga


Mbinga. Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga kwa kushirikiana na Kampuni ya Gesi ya Oryx Tanzania jumanne (Julai 23) waligawa mitungi ya gesi 1,050 kwa wananchi wa Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma.


Ugawaji wa mitungi hiyo yenye thamani ya Sh45 milioni unalenga kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.



Kati ya mitungi ya gesi 1,050 iliyotolewa katika ukumbi wa One Pacific uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Mkoani Ruvuma, kampuni ya Oryx ilitoa mitungi 700 na Mhe. Judith mitungi 350.


“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa nishati safi ya kupikia imejidhatiti katika kuhakikisha tunaongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia,” alisema Mhe. Judith huku akiipongeza kampuni ya Oryx kwa mchango wake wa mitungi ya gesi 700.


Kupitia Mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), Serikali imedhamiria kuongeza kaya za watanzania zinazotumia nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 10 ya sasa mpaka asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.


Ikiwa ni sehemu ya jitihada za  kuongeza matumizi ya nishati safi, mpaka sasa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imesambaza mitungi ya gesi ya ruzuku 83,500 yenye thamani ya Sh3.5 bilioni, kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Nishati.



Kama hiyo haitoshi, aliongeza Mhe. Judith, mwaka huu wa fedha serikali imepanga kutoa mitungi 452,445 yenye thamani ya Sh10 bilioni.

“Lengo letu ni kupunguza gharama za nishati safi ya kupikia na kwa kufanya hivyo naamini tutachochea matumizi ya nishati hiyo,” alisema Mhe. Judith.


Agenda ya nishati safi ya kupikia ni muhimu sana kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu na kwa kutambua hilo Mhe. Rais Dkt. Samia amekua kinara katika kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.


Sifa hiyo ya Mhe. Rais haiishii Tanzania tuu, bali imevuka hadi mipaka ya nchi hii mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Hii inadhihirishwa na yeye kuzindua ‘programu’ ya nishati safi ya kupikia Afrika yenye lengo la kuleta mageuzi na kumkomboa mwanamke.


Uzinduzi huo ulifanywa mwishoni mwa mwaka jana huko Dubai, Falme za Kiarabu wakati wa Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28).


Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Bw. Araman Benoit alisema: “Tunataka jamii ya Tanzania iachane na nishati chafu ambayo sio mbaya kwa afya tuu, bali ni hatari kwa mazingira pia.”

 

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa