WATU wenye ulemavu wilayani Namtumbo, Ruvuma wamedai rasilimali za
taifa zinawanufaisha zaidi watu wasiokuwa na ulemavu ukilinganisha na
watu wenye ulemavu.
Walitoa madai hayo kwenye mafunzo yaliyotolewa na shirika lisilo la
kiserikali la kuwaendeleza watu wenye ulemavu na yatima (SHIKUWATA) kwa
ufadhili wa The Foundation For Civil Society yalifanyika wilayani
hapa.
SHIKUWATA imeendesha mafunzo ya siku tano kwa watu wenye ulemavu Kata
ya Namtumbo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kujua sera ya maendeleo
na huduma kwa watu wenye ulemavu.
Wakichangia mada kwa nyakati tofauti juzi, waliiomba serikali
kuzingatia uwiano katika mgawanyo wa rasilimali za taifa, ajira, kupewa
matibabu bure kama ilivyo kwa watu wasiokuwa na ulemavu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa shirika
hilo, Magreth Mapunda, aliwataka washiriki hao kufuatilia mafunzo hayo
kikamilifu ili yaweze kuwasaidia kujua haki zao za msingi.
Aliwataka watu hao wenye ulemavu kuwa huru katika kuchangia kero na
changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye mafunzo hayo, ili waweze
kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na serikali.
Mratibu wa shirika hilo, Laura Martin, alisema wameamua kuendesha
mafunzo hayo katika Kata ya Hanga, Namtumbo, Msindo na Namabengo kwa
ajili ya kuwawezesha kujua sera inayozungumzia kundi lao kwa lengo la
kuelewa kama inatekelezwa baada ya kugundulika kuwepo kwa tabaka kubwa
la kuwatenga na mgawanyo wa rasilimali za taifa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment