Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu akiongoza watu mbalimbali
kumpongeza Askofu Mkuu mpya wa Jimbo la Songea, Damian Dallu katika
Kanisa la Mtakatifu Mathias Mulumba Kalemba mjini Songea jana
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Damian Dallu
amesema Katiba Mpya itapatikana iwapo wajumbe wa Bunge la Katiba
watakuwa na maadili ya kiroho kwa kufuata maagizo ya Mwenyezi Mungu bila
kupindisha ukweli wa mchakato wa maoni ya Katiba.
Amesema kupotosha ukweli wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba unaweza kuipeleka nchi kubaya.
Hayo aliyasema jana katika Ibada maalumu ya
kumsimika rasmi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mtakatifu
Mathias Mulumba lililopo Mjini Songea ambayo ilihudhuriwa na maelfu ya
waumini, viongozi wa chama na Serikali, viongozi wa madhehebu ya dini
pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne
Makinda.
Askofu Dallu alisema wapo watu wanaodhani kuwa
iwapo Katiba Mpya itapatikana matatizo yao yatakwisha kitu ambacho
hakina ukweli kwa madai kuwa hata Katiba iliyopo imeongoza nchi kwa
miaka 50 na watu waliungana kiroho na siyo kwa kupitia makaratasi ambayo
yanaweza kuchakachuliwa.
Alisema Watanzania hawana budi kumwomba Mungu
asaidie kupata viongozi watakaoweza kuliongoza taifa kuanzia ngazi za
chini hadi juu kwa kufuata maadili ili nchi isije ikaiingia kwenye
machafuko.
Akitoa salamu za Mkoa wa Ruvuma Mkuu wa Mkoa, Said
Mwambungu alisema kuwa Serikali itatoa ushirikiano kwa askofu huyo
katika kuunga mkono juhudi na mafanikio yanayofanywa na Kanisa Katoliki
katika kutoa huduma zake kwenye Sekta ya afya, elimu, kilimo na maji.
Alisema mafanikio hayo yamechangiwa na viongozi wa
dini ambao walikuwa wakijituma kwa bidii kusaidia wananchi bila kujali
madhehebu wanayotoka kitu ambacho kimeipa Serikali faraja na inaomba
ushirikiano huo kuendelea.
Spika Makinda akitoa salamu kwa niaba ya Serikali
amewataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii badala ya kuitegemea
Serikali au kanisa kuwaletea maendeleo jambo ambalo linarudisha nyuma
maendeleo binafsi.
Naye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,
Tarcisius Ngalalekumtwa amempongeza Askofu Dalu kwa kukubali kushika
nafasi hiyo na kukemea tabia za wizi na mauaji kuwa ni kinyume cha
matendo ambayo hayampendezi Mungu.
Alisema dhamira safi, upendo na wema, upole, ukarimu na rehema ndiyo matunda na zabibu za kumtolea Mwenyezi Mungu
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment