Home » » Ripoti: Wazee hawapati huduma za afya bure

Ripoti: Wazee hawapati huduma za afya bure

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Wazee  
Mwandishi wa vitabu, Pearl Buck aliwahi kuandika “jamii lazima ihakikishe inatengeneza mazingira mazuri kwa wazee ili kila anayefikia hatua hiyo ya maisha asijione tofauti na watu wa rika jingine, kwa sababu ni hatua ambayo kila mwanadamu ataifikia iwapo hatafariki dunia mapema”.
Fikra kama hizo ndizo zimefanya nchi nyingi kutengeneza mifumo ambayo inawawezesha wazee waishi maisha mazuri ambayo yanawafanya kutojisikia kunyanyapaliwa.
Hivi karibuni taasisi isiyo ya kiserikali nchini, Twaweza ilifanya utafiti ambao ulibainisha kuwa ni mtu mmoja tu kati ya watu 20 wenye umri zaidi ya miaka 60 ambaye hupata huduma za afya na matibabu bila kulipa gharama zozote kwenye vituo vya afya nchini.
Siyo kwamba hawaitaki huduma hiyo, bali mazingira ya upatikanaji wa huduma hizo siyo rafiki na hivyo kuwafanya wazee wenye uwezo kidogo wakimbilie katika hospitali za binafsi na wale wengine kubaki wakisubiri miujiza itokee.
Jitihada za serikali kuimarisha sekta ya afya zimeendelea kupambana na vikwazo baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya vituo vya afya ambavyo vinatoza fedha kwa wazee na watoto wakati wa kutoa huduma hizo jambo ambalo ni kinyume na sera ya afya ya wazee na watoto.
Idadi hiyo ni sawa na asilimia 6 tu ya watu wanaozidi umri huo, kwa maana ya wazee wanaofadika na huduma za bure.
Mbali na kundi hilo kuonekana kunyimwa haki yao ya msingi, utafiti huo pia ulifanywa kwa kundi jingine ambalo ni la watoto walio na umri chini ya miaka mitano. Kwenye kundi hilo imebainika kuwa ni mtoto mmoja kati ya watano mwenye umri chini ya miaka hiyo, ambaye hupata huduma za afya na matibabu bure. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 18 tu ya watoto wanaofaidika na huduma hizo.
Mtafiti kutoka taasisi hiyo, Elvis Mushi anasema kuwa kutokana na mambo yanayotendeka kwenye vituo hivyo vya afya na matokeo waliyoyapata, ni dhahiri kuwa makundi hayo mawili yanayotakiwa kupata haki yao ya msingi hayatendewi haki.
“Wagonjwa wananyimwa haki zao za kupata huduma za afya kikamilifu kama inavyotakiwa. Inafahamika fika kuwa wanatakiwa kupewa huduma hizo bila malipo, halafu bado wanatozwa fedha. Hiyo si sawa,” anasema Mushi.
Mtafiti huyo anasema kuwa huenda wagonjwa wengine wakawa wanateseka kwa kuugulia nyumbani kutokana na ukweli kwamba hawana fedha za kulipia huduma za afya.
Hata hivyo, Mushi anatoa tahadhari kuwa kutokana na usimaminzi mbovu wa Serikali juu ya huduma zinazotolewa kwenye vituo vingi vya afya vilivyopo chini yake, huenda ikawa sababu kubwa inayochangia wananchi wengi kuvisusia vituo hivyo.
“Kutoridhika na usimamizi wa Serikali kwenye huduma za afya kunaweza pia kusababisha wananchi kutopendelea kwenda kupata matibabu na huduma katika vituo vya afya,” anasema Mushi.
Utafiti huo uliofanywa kati ya Mei na Juni 2013 ukiwa na lengo la kubaini iwapo vituo vya afya vipo kwa ajili ya kuwahudumia watu na uliojumuisha zaidi ya nusu ya watu (asilimia 57) waliotembelea vituo vya afya kwa dhumuni la kutibiwa au kumsindikiza mgonjwa, ulibaini kuwa wagonjwa kutoka kwenye makundi hayo mawili huwa wanatozwa fedha kinyume na mpango uliowekwa na Serikali.
Mpango wa Serikali ni kutoa bure huduma za afya kwa makundi hayo mawili, lakini dhumuni hilo linaonekana kuendeshwa kinyume na baadhi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma hizo nchini.
Mratibu wa mradi wa wazee wa shirika la Helpage International, Juliana Bernard anasema zipo sababu nyingi zinazowafanya wazee wasipate huduma stahili pamoja na Serikali kuweka sera inayotoa mwongozo.
Anasema kama kweli Serikali ina nia ya kuhakikisha wazee wanapata huduma hizo bila usumbufu wowote, iweke vipaumbele ikiwemo kuwawekea waangalizi maalumu angalau katika kila hospitali kadhaa nchi nzima.
“Ni kweli Serikali inaonekana kuwa na nia ya kuwasaidia wazee, lakini kwa hali halisi ya hospitali zetu, siyo rahisi kwa sababu wauguzi na madaktari wengi hawana weledi. Wanadharau wazee. Kama wangekuwa na madaktari wao au na wodi zao maalumu pengine hali ingekuwa tofauti,” anasema Juliana.
Anaongeza kuwa Serikali iongeze bajeti katika huduma za afya ambayo itawezesha wazee kupata huduma zao ikiwemo hiyo ya kuwawekea wauguzi na madaktari wao.
“Wakati mwingine hata daktari hampimi mzee akijiaminisha kuwa haumwi bali uzee unamsumbua. Watoa dawa nao huwanyima dawa wazee, hali ambayo imewavunja moyo na kuwafanya wengine waamue kufia majumbani mwao,” anasema Juliana.
Sera ya Afya inasemaje?
Sera rasmi ya Afya ilitayarishwa na kupitishwa mwaka 1990 inasema kuwa msisitizo wa sera hiyo ulikuwa ni kuinua hali ya afya kwa wananchi wote na kipaumbele kilitolewa kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuugua. Sera hiyo inafafanua kati ya makundi ambayo yamepewa kipaumbele ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Watoto wanatakiwa kupewa huduma ya afya bila malipo.
Sera hiyo ya mwaka 2003 inaweka wazi kuwa umri wa miaka 60 ndio unaozingatiwa kuwa kigezo cha uzee ni umri wa miaka 60 na kuendelea.
Katika kipengele cha huduma ya afya kwa wazee, sera inasema kuwa kutokana na umri huo wengi wao huwa na magonjwa ya mara kwa mara na ya muda mrefu, hali ambayo ni ya kawaida katika kipindi hicho cha maisha ya biandamu.
Hali hiyo inahitaji uangalizi na matunzo maalum ya kitaalamu hivyo kutokana na hilo huduma za afya kwa wazee zitakuwa zikitolewa bure.
Pamoja na ukweli huo, huduma za afya hazipatikani kwa urahisi kwa wazee walio wengi na mara nyingi ni ghali na kuwa utaratibu wa kutoa huduma bure kwa wazee, bado una upungufu, inasema sera hiyo.
Pia inaeleza kuwa kutakuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa watumishi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wazee na namna ambavyo wanapaswa kuhudumiwa tofauti na makundi mengine.
Jambo hilo linaungwa mkono na mkuu wa Twaweza, Rakesh Rajani ambaye anasema kuwa licha ya kuwa na sera hizo, bado kuna changamoto lukuki zinazozikabili.
Rajani anasema hakuna utekelezaji mzuri wa sera hizo ambazo malengo yake ni mazuri kwa kuwa wagonjwa kutoka kwenye makundi hayo mawili wanaendelea kuteseka bila sababu za msingi.
“Wazee na watoto wanaumia kwa sababu hizo sera zilizowekwa hazitekelezwi. Kungekuwa kuna ufualiliaji na usimamizi mzuri, labda haya yote yasingetokea,” anasema Rajani.
Mkuu huyo anasema kuwa sera hizo zimebaki kuwa maneno yaliyoko kwenye maandishi tu, lakini ufuatiliaji wake ni hafifu.“Serikali inahitaji kutimiza ahadi zake za kufuatilia utekelezaji, kuwatunuku wanaotoa huduma nzuri, na kuwawajibisha wale wanaotoa huduma duni. Vinginevyo Serikali itapoteza uaminifu wake na watu maskini wataendelea kuteseka,” anasema Rajani.
Wizara ya Afya yakemea
Naibu Waziri wa Afya, Dk Kebwe Steven anasema kuwa sera ya afya inaweka wazi kuwa kuna makundi maalum yanayotakiwa kupewa huduma za afya bure kutokana na mahitaji yao, likiwamo kundi la watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wazee walio na umri wa kuanzia miaka 60.
Steven anafafanua kuwa mbali na makundi hayo mawili ya watoto na wazee kuna makundi mengine pia yanayopaswa kupata huduma za afya bila kutozwa gharama za matibabu. “Magonjwa ya kudumu kama pumu, kifua kikuu, Ukimwi na magonjwa mengine yaliyoainishwa kwenye sera pamoja na wale wasiona na wasio na uwezo kwa maana ya wenye kipato kidogo, wanatakiwa kupata huduma za afya bure,” anabainisha Waziri Kebwe.
Anasisitiza kuwa hivyo ndivyo sera inavyoeleza na kwamba kinyume na hapo ni ukiukwaji wa matakwa yaliyowekwa na serikali chini ya sera hiyo.
“Tuliweka sera kwa madhumuni maalum lakini ikitokea kwenye badhi ya vituo vya umma wanatoza fedha kwa wagonjwa kutoka kwenye makundi hayo, tutachukua hatua kali dhidi yao,” anasisitiza Waziri Kebwe.
“Tunafahamu kuwa wako baadhi ya watumishi wa umma ambao si waaminifu na si waadilifu hivyo na ninaahidi kuwa tutakula nao sahani moja. Kama wizara kamwe hatuwezi kukubaliana na hilo.”
Vilevile Kebwe amekemea vikali kuhusiana na hilo hivyo amewataka viongozi wote kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa wanaohusika na wizara hiyo kushirikiana na wadau wangine wa afya nchi kutoa taarifa juu ya suala hilo ili wizara iweze kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa