Polisi mkoani Ruvuma, wameingia katika kashfa, baada ya askari
wake kutuhumiwa kuiba vitu vyenye thamani ya zaidi ya Sh900 milioni
waliyokuwa wakivilinda. Vitu hivyo ni mali ya mkandarasi aliyefukuzwa
katika mradi wa ujenzi wa Barabara ya Namtumbo hadi Tunduru.
Tayari polisi 14 wamesimamishwa kazi na wanasubiri
kuvuliwa magwanda ili kufikishwa mahakamani. Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Ruvuma, Deusdedit Nsimike, jana alithibitisha habari hizi kwa njia ya
simu.
Alisema tukio hilo limelifedhehesha Jeshi la
Polisi na kwamba taratibu za kuwafukuza kazi askari hao zinaendelea
kabla ya kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Mtoa habari wetu alisema kashfa hiyo iligundulika
mwezi uliopita, lakini haikutangazwa kutokana na unyeti wake na kwamba
suala hilo limeishtua Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Ruvuma.
Akifafanua zaidi alisema kwamba Wakala wa Barabara
Tanzania (Tanroads), waliipatia polisi kazi ya kulinda mitambo, magari
na vifaa mbalimbali vya Kampuni ya Progressive Hgleig JV ya India, baada
ya kampuni hiyo kushindwa kazi na hatimaye kufukuzwa.
Alisema Serikali iliifukuza kampuni hiyo na kutoa agizo la kushikilia mali zake hadi itakapolipa fidia kwa hasara iliyoipata.
Mtoa habari ambaye jina lake linahifadhiwa alisema
askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Ruvuma, walipata zabuni ya
kulinda mali hizo, lakini baadaye imegundulika kuibwa mali za mamilioni
ya fedha.
Baadhi ya mali zilizoibwa ni pamoja na mafuta,
matairi na vipuri vya magari. Meneja wa Tanroads mkoani Ruvuma, Abraham
Kisimbo, alithibitisha habari hizo.
Alisema tukio hilo ni baya na kwamba anayeweza
kulizungumzia zaidi ni na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma au Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment