Na. Lilian Lundo – MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikishirikiana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) inaendelea kuagiza dawa ili kuhakikisha zinapatikana muda wote.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Mpoki
Ulisubisya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar
es salaam wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa dawa nchini.
“Kumekuwepo na taarifa
zisizo na ukweli zilizotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali
inayofuatilia masuala ya afya nchini kwamba MSD inaupungufu mkubwa wa
dawa ambapo taarifa hiyo inasema kuwa kuna makopo 173 ya dawa za paracetamol nchi nzima, taarifa ambazo hazina ukweli wowote” alifafanua Dkt. Ulisubisya
Aidha ameeleza kuwa MSD
imepokea makopo 10,000 ya vidonge vya paracetamol na kusambazwa katika
vituo vyote vya kutoa huduma za afya nchi nzima.
Vile vile alisema kuwa MSD imesaini mkataba na mtengenezaji wa ndani kwa ajili ya kutengeneza makopo 138,000 ya dawa za paracetamol
yenye ujazo wa vidonge 1,000 ambazo zitaanza kupokelewa wiki ya kwanza
ya mwezi Octoba mwaka huu na kusambazwa katika vituo vinavyotoa huduma
za Afya nchini.
Hata hivyo alibainisha
kuwa antibiotics na dawa za kupunguza maumivu (Ciprofloxacin,
Ceftriaxone, Diclofenac, Co-trimoxazole, Amoxycyline, Doxycycline na
Metronidazole) ambapo zilikuwa zikihitajika zaidi zimeshapokelewa na MSD
na kupelekwa katika kanda zote za MSD kwa ajili ya kusambazwa kwenye
vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Aliendelea kwa kusema
kuwa, dawa za Miradi Msonge ambazo zinatibu na kuzuia magonjwa ya
Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu, Ukoma, Kichaa cha Mbwa, Uzazi wa Mpango na
chanjo mbalimbali zipo za kutosha kwenye Bohari.
Pia amesema kwa chanjo ambazo ziliripotiwa kutokuwepo zinatarajia kuwasili nchini kuanzia Octoba
2, 2016, ambapo kwa wale waliotakiwa kupata chanjo hizo lakini
hawakupata kutokana na ukosefu huo watataarifiwa ili kuweza kufika
kwenye vituo vya afya na kupata chanjo hizo.
Akielezea juu ya hali
ya upatikanaji wa dawa nchini Dkt. Ulisubisya alisema kuwa, kwa sasa
upatikanaji wa dawa nchi ni asilimia 53 ambapo katika aina 135 za dawa
muhimu, aina 71 za dawa hizo zinapatikana ghalani na nyingine zipo
kwenye vituo vya kutolea huduma.
Dkt. Ulisubisya alisema
kuwa hali ya upatikanaji wa dawa itaimarika zaidi Octoba mwaka huu
ambapo Serikali inategemea kupokea kiasi kikubwa cha dawa pamoja na
chanjo.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment