Na:
Genofeva Matemu - WHUSM
Wadau wa tasnia ya
filamu nchini wameipongeza Serikali kuwashirikisha katika mchakato wa uandaaji
na ukamilishaji wa Sera ya filamu nchini.
Hayo yamesemwa na
wadau mbalimbali walioshiriki katika kikao cha kupitia uchambuzi wa hali halisi
ya tasnia ya filamu kwa ajili ya maandalizi ya Sera ya filamu kilichofanyika
mapema wiki hii.
Akizungumza wakati wa
kikao hicho Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa
sekta ya filamu hapa nchini imekuwa ikisimamiwa na kongozwa na Sera ya
Utamaduni ya mwaka 1997 lakini kutokana na kukua kwa tasnia ya filamu ilionekena
kuwa kuna uhitaji wa Sera ya Filamu itakayo kuwa dira na mwongozo katika kukuza
tasnia hiyo.
Bibi. Fissoo amesema
kuwa Bodi imekamilisha hatua ya uchambuzi wa hali halisi ya sekta ya filamu kwa
kiasi kikubwa kwa kupitia machapisho mbalimbali pamoja na kuangaia mifano ya
nchi zilizopiga hatua katika sekta ya filamu kama vile Afrika ya Kusini, Kenya,
Nigeria pamoja na kuzingatia mchango mkubwa kutoka kwa wadau wenyewe ambao
wamewezesha kupatikana kwa takwimu muhimu.
Aidha Muigizaji wa
filamu nchini Bw. Saidi Jangala amesema kuwa sera inayoandaliwa iweke maelekezo
ya kuzingatia utengenezaji wa filamu zinazobeba historia ya Kitanzania kama
vile historia ya Majimaji, pia sera hiyo ianishe mikakati mahsusi ya
upatikanaji wa mitaji pamoja na kuipa kipaumbele michezo ya kuigiza kwani
michezo hiyo ndiyo chachu kuu ya weledi katika uigizaji.
Naye Msanii wa filamu
nchini Bw. Chiki Mchoma ameiomba kamati ya kuanda sera ya filamu kuhakikisha
sera inayoandaliwa inaelekeza wadau wa filamu kuandaliwa mifumo ya elimu pamoja
na kuweka misingi ya kufilisi wanaojihusisha na uharamia wa kazi zao na
kuwawajibisha wanaonunua kazi zitokanazo na uharamia.
Hata hivyo mtaalamu
wa Kiswahili Pro. Hermas Mwansoko ameitaka kamati ya kuandaa sera ya filamu
kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye filamu zetu kusaidia
kuzitofautisha filamu za Kitanzania na zingine.
Kukamilika kwa sera
ya filamu nchini kutabadilisha kabisha taswira nzima ya sekta ya filamu hapa
nchini kwani itatoa dira ama mwelekeo wa tasnia. Hii itawezesha kuongezeka kwa
fursa za uwekezaji katika tasnia, kuweka mwongozo kuhusu motisha na fursa za
mitaji, uzalishaji wa bidhaa bora zenye kuzingatia weledi pamoja na filamu
kuangaliwa kama chombo cha kukuza uchumi kwa manufaa kwa Taifa na watanzania
wote.
0 comments:
Post a Comment