WILAYA ya Songea mkoani Ruvuma inakabiliwa na tishio la kugeuka
jangwa kutokana na wananchi kukata miti, kuchoma misitu moto na baadhi
ya watumishi wasiokuwa waadilifu kuruhusu wafugaji kutoka mikoa
mbalimbali nchini kuingiza idadi kubwa ya mifugo bila kufuata sheria.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Polole Mgema wakati
akitoa salamu za serikali katika kikao cha Baraza la Madiwani cha
Halmashauri ya Wilaya ya Songea kilichofanyika katika Kijiji cha Lundusi
katika Kata ya Maposeni.
“Kuna uharibifu mkubwa katika mlima Lihanje na nimekuwa nikitoa
maagizo kwa watendaji wetu mara kwa mara kusitisha shughuli za kilimo
katika mlima ule, hata hivyo bado imeonekana baadhi ya wananchi
wanaendelea kukata miti na kufanya shughuli zao za kibinadamu,” alisema
Mgema na kuongeza: “Kuna watumishi ambao ni wagumu sana kutekeleza
maagizo ya serikali sasa mimi mwenyewe nitaanza operesheni ya kuwaondoa
ndugu zenu, lakini msije kunilaumu kwa hatua nitakayochukua.”
Kwa mujibu wake, ataanza kupita kijiji hadi kijiji kwa ajili ya
kuwatangazia wananchi kuhusu mpango wa serikali kutunza mlima Lihanje
kutokana na umuhimu wake baada ya kuona watumishi waliopewa dhamana ya
kusimamia uhifadhi wa mazingira katika mlima huo kushindwa kutimiza
wajibu wao kwa sababu wanazozijua. Aidha, amewataka watumishi na
madiwani kusimamia vema agizo la serikali la kutoruhusu uingizaji mifugo
kutoka mikoa mingine na kuzuia biashara ya mkaa kwenda nje ya Wilaya ya
Songea.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment