Home » » Pinda: Jifunzeni kutoka kwa wawekezaji

Pinda: Jifunzeni kutoka kwa wawekezaji


Na Amon Mtega, Songea
WANANCHI wa Kijiji cha Lipokela, Kata ya Mbingamhalule wilayani Songea, wametakiwa kuacha kuwa watazamaji kwa wawekezaji na kufurahia fursa zao bali wafanye kazi ya kujifunza kutoka kwao.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipotembelea shamba la kilimo cha kahawa la wawekezaji wa Kampuni ya Avivu Tanzania Ltd, lenye ukubwa wa ekari 1,934 lililopo kijijini wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Ruvuma.

Alisema kunufaika na wawekezaji waliopo, inatakiwa kushikamana nao zaidi kwa lengo la kujifunza namna ya utendaji kazi na hatimaye uchumi utakuwa kwa wote bila kuacha pengo kubwa kati ya mwekezaji na mwananchi mzawa.

“Msipofanya kazi hiyo ya kujifunza changamoto nyingi zitakuwa zinawakabili hasa suala la kipato ambacho huwa kinafikia mahali pakulaumiana kuwa mnaonewa kumbe si kweli bali ni uzembe wa kutokuwa tayari kupata mafunzo kutoka kwa wawekezaji,” alisema Pinda.

Alisema anapenda shamba hilo la wawekezaji liwe pia shamba darasa kwa wakulima wa kijiji hicho na vijiji vya jirani, kwa ajili ya kupata mafunzo hayo kirahisi zaidi na kwa uhakika.

Kwa upande wake, Meneja wa Shamba hilo, Medappa Genepaphy, alisema kampuni hiyo imeweza kutoa ajira kwa watu 5,000.

Alisema wameandaa miche ya kahawa itakayopandwa katika shamba hilo pamoja na kila mkulima wa kijiji hicho atapanda ekari moja ya kahawa katika shamba lake.

Aidha, alisema kampuni hiyo itasaidiana na wananchi katika huduma za kijamii ikiwamo ujenzi wa kituo cha afya na kutoa kompyuta katika shule na hatimaye wanafunzi waweze kupata elimu iliyo bora zaidi.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa