Mussa Mwangoka, Mbinga-Ruvuma yetu
UONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma umejiwekea mikakati kamambe ya kuongeza makusanyo ya halmashauri hiyo katika mwaka ujao wa fedha kwa kutumia vyema rasilimali zinazotokana na ziwa Nyasa na kuaanisha vyanzo kadhaa vya kukusanya kodi.
Akizungumza katika kikao cha pamoja baina Kamati ya Fedha na Wataalamu wa Halmashauri hiyo katika ziara yao ya siku nne mkoani Rukwa, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo , Oddo Kiliani Mwisho alisema kuwa wametumia muda mwingi kujifunza katika eneo la Ziwa Tanganyika mkoani Rukwa na kubaini dosari kadhaa zilizokuwa zikisababisha kupungua kwa pato la halmashari yao.
“Baada ya kufanya ziara mkoni Rukwa hususani katika maeneo ya mwambao mwa Ziwa Tanganyika tumebaini dosari kadha wa kadhaa ambazo zimekuwa zikisababisha kupungua kwa pato katika Halmashauri yetu ya Mbinga” alisema Mwisho
Kwa mujibu wa Mwisho ufuatia ziara yao mkoani Rukwa wamebaini kuwa kuna vyanzo vingi vya mapato ambavyo wamekuwa wakivipoteza kwenye Ziwa Nyasa hivyo watatumia maarifa waliyoyapata na kuweka mikakati ya kuboresha ukusanyaji wa mapato kwenye ziwa hilo kama zinavyonufaika Halmashauri za Wilaya ya Sumbawanga na Nkasi kwenye Ziwa Tanganyika.
Alisema licha ya kuwa Halmashauri hiyo ya Mbinga imeweza kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kufikia zaidi ya Sh bilioni 1.8 katika mwaka huu wa fedha unaokwisha lakini bado wanayo nafasi ya kuongeza pato la halmshauri hiyo iwapo watatumia fursa zilizopo kwenye Ziwa Nyasa.
0 comments:
Post a Comment