Home » » KATIBU MKUU UN AZUNGUMZIA MPAKA WA ZIWA NYASA

KATIBU MKUU UN AZUNGUMZIA MPAKA WA ZIWA NYASA

Na Mwandishi wetu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki- Moon, amepongeza msimamo wa Tanzania kutafuta majawabu ya amani katika kujadiliana kuhusu mzozo wa mpaka kati yake na Malawi kwenye Ziwa Nyasa.

Amesema uamuzi wa Tanzania ndiyo njia sahihi na inayokubaliwa kimataifa kutafuta na kupata suluhisho la migogoro ya namna hiyo.

Ban Ki Moon ametoa pongezi hizo kwa Tanzania mjini hapa juzi wakati alipomkaribisha na kukutana kwa mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko New York, kwa ziara ya siku mbili.

“Majuzi nilikutana na Rais Joyce Banda wa Malawi na akanielezea mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa na mazungumzo ambayo nchi zetu mbili zinafanya ili kupata ufumbuzi wa amani. Hii ndiyo njia sahihi na Umoja wa Mataifa unaunga mkono njia hiyo,” Ban Ki Moon alimemweleza Rais Kikwete.

Rais Kikwete alimweleza Katibu Mkuu huyo wa UN kuwa Tanzania bado inaamini kuwa njia sahihi na maelewano zaidi ni kutafuta ufumbuzi wa mvutano huo wa mpaka kwa njia ya mazungumzo.

Rais Kikwete alisema: “Wazo la awali la kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili la miaka mingi sana lilitokana na Rais wa Malawi, marehemu Bingu wa Mutharika ambaye aliniandikia barua ya kutaka nchi zetu zianze mazungumzo kuhusu mzozo huo. Nasi tulikubali. Hivyo, ndivyo tulivyoanza kuzungumza.”

Rais Kikwete alisema kuwa Tanzania inaongozwa na msingi mkuu wa mipaka inayopita kwenye maeneo ya maji ambako mipaka hiyo inakuwa katikati.

“Mpaka kati ya Malawi na Msumbiji kwenye ziwa hilo hilo, Nyasa, umekuwa katikati ya Ziwa tokea mwaka 1954 wakati nchi hizo zilipokubaliana kusahihisha makosa ya kuuweka mpaka huo nje ya Ziwa. Mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye mto mkubwa zaidi unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa uko katikati ya mto wenyewe,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kila mahali ambako nchi zinatengenishwa na maji, mpaka unakuwa katikati ya nchi.  Sisi tunadhani hata kwenye mpaka wetu wa Malawi kwenye Ziwa Nyasa ni lazima uwe katikati ya Ziwa.”
Chanzo: Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa