Na
Mwinyi Sadallah
Sheikh
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Waziri Ally Chilakwechi, amepigwa na
watu wasiojulikana baada ya kumvamia nyumbani kwake eneo la Mchangani mjini
Tunduru na kujeruhiwa vibaya.
Sheikh Chilakwechi akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu kutoka katika
Hospitali ya Wilaya ya Tunduru alikolazwa, alisema alishambuliwa na watu
wasiojulikana juzi.
Akielezea mkasa huo, alisema siku ya tukio alifuatwa na watu watatu majira ya
saa 2:30 usiku nyumbani kwake wakidai kuwa kuna vurugu zimetokea katika msikiti
wa Kitumbini eneo la Majengo, hivyo anahitajika kwenda kutuliza vurugu hizo.
Alisema kwa kuwa alikuwa hawatambui watu hao, isingekuwa vyema kwenda huko
kutokana na umbali kwa kuwa kutoka nyumbani kwake hadi kwenye msikiti huo ni
zaidi ya kilomita mbili.
Shekhe Chilakwechi alisema baada ya kuwajibu hivyo, watu hao walitoka nje na
ghafla kundi jingine la watu lilimvamia kwa kumrushia mchanga usoni na kuanza
kumshambulia sehemu kadhaa za mwili.
Alisema wakati watu hao wakiendelea kumshambulia, mke wake alitoka nje na
kuanza kupiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani ambao walitoka na
kuanza kuwakimbiza watu hao na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyejulikana kwa
jina la Rajabu Abdallah Likoto (17).
Shekhe huyo alisema mtu huyo alikamatwa baada ya kukwama kwenye matope wakati
anavuka mto Mlingoti na alijeruhiwa kwa kukatwakatwa na mapanga. Mtuhumiwa huyo
naye amelazwa katika hospitali hiyo.
MGANGA WA WILAYA ANENA
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, Dk. Fred
Wenandi, akizungumzia tukio hilo, alisema Sheikh huyo amejeruhiwa vibaya
usoni na amelazwa katika hospitali hiyo na anaendelea na matibabu.
KAULI YA DC
Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho, alithibitisha taarifa za kupigwa kwa
Sheikh huyo na kufafanua kuwa alimtembelea hospitalini kumjulia hali.
Nalicho alisema bado hazijafahamika sababu za kushambuliwa kwa Sheikh huyo na
kwamba uchunguzi wa tukio hilo unafanywa na vyombo vya dola.
“Nilikuwa na Sheikh katika sherehe za miaka 50 ya Kanisa la Biblia
zilizofanyika hivi karibuni wilayani hapa katika kuendeleza mahusiano na dini
nyingine. Ni mtu anayependa mahusiano mazuri na dini nyingine, sifahamu sababu
za kushambuliwa kwake,” alisema.
VIONGOZI WA UAMSHO KORTINI
Viongozi saba wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar jana wamefikishwa mahakamani na
kusomewa shitaka la kufanya uchochezi na kusababisha vurugu na uvunjifu wa
amani, maafa, na mtafaruku dhidi ya Serikali.
Viongozi waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe ni kiongozi
mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi Ahmed (41), mkazi wa Mbuyuni.
Wengine ni Sheikh Mselem Ali Mselem (52), mkazi wa Kwamtipura; Sheikh Mussa
Juma Issa (37), mkazi wa Makadara; Sheikh Azzan Khalid Hamdan (43), mkazi wa
Mfenesini; Suleiman Juma Suleiman (39), mkazi wa Makadara; Hassan Bakari Suleiman
(39), mkazi wa Tomondo na Khamis Ali Suleiman.
ULINZI MKALI WA POLISI
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani majira ya saa 4:00 za asubuhi wakiwa
chini ya ulinzi mkali wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakisindikizwa na
magari matatu yenye namba PT 873, PT 1159, PT 859 na gari walilokuwa
wamepakizwa washitakiwa hao ni PT 1891.
Aidha, viongozi hao wa Uamsho walikuwa wamezungukwa na askari wasiopungua 10
katika kila gari moja, waliobeba bunduki aina ya SMG zisizopungua 25 mbali na
mabomu ya machozi kama hatua za tahadhari kwa vurugu zozote endapo zingetokea
katika viwanja vya Mahakama hiyo.
Ulinzi uliimarishwa katika eneo hilo la Mwanakwerekwe na askari wa Jeshi la
Polisi na vikosi vya SMZ na kabla ya kuwasili kwa viongozi hao, wananchi wote
waliojitokeza mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo waliamriwa kuondoka. Pia
hatua zilichukuliwa za kuzuia watu kukatisha katika njia za eneo hilo.
Vile vile, maeneo ya shule nne zilizopo jirani na Mahakama ya Mwanakwerekwe
wanafunzi wote walitakiwa kurejea majumbani kabla hata ya washitakiwa
hawajafika kwa lengo la kuhakikisha eneo hilo linakuwa na utulivu.
Akiwasomea mashitaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Maulid Ame Mohamed,
alidai kuwa viongozi hao wa Uamsho Agosti 17 majira ya saa 11:00 jioni,
wanadaiwa kufanya makosa ya uchochezi na kufanya fujo kinyume na kifungu cha
45(10) (a) na (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 ya mwenendo wa makosa
ya Jinai ya Zanzibar.
Alidai kuwa watuhumiwa hao wakiwa katika Msikiti wa Magogoni Msumbiji,
walitenda kosa la uchochezi na kusababisha uvunjifu wa amani, matukio ya
vurugu, maafa na kusababisha mtafaruku dhidi ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Baada ya kusomwa mashitaka dhidi yao, ulitokea mvutano mkali huku wakili wa
upande wa utetezi, Abdallah Juma Mohamed, akitaka wateja wake waachiwe huru na
kesi itupiliwe mbali kwa madai kuwa imefunguliwa kinyume na kifungu cha 45(1)
(a) na (b) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Alidai kuwa sheria hiyo inasema hakuna mtu atakayefunguliwa mashtaka kabla ya
kutolewa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka cha wahusika kufunguliwa kesi na
kueleza kwa nini upande wa mshitaka haujaweka wazi juu ya kuwepo kwa kibali
hicho mbele ya Mahakama.
“Mheshimiwa Hakimu, kesi zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, Mahakama isiingie
katika mtego huu, washitakiwa hawapaswi kujibu mashitaka waliyosomewa kwa vile
hakuna kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka,” alidai Abdallah Juma na kuongeza:
“Naamini Mahakama hii ipo kwa mujibu wa sheria, haiendeshi shughuli zake kama
kesi za kwenye mwembe wala haipigi ramli wala bao katika utekelezaji wa
majukumu yake, hivyo naomba wateja wangu waachiwe, labda kibali hicho kiwe
kimepenyezwa mezani kwako sasa hivi,” aliiambia Mahakama.
Hata hivyo, hoja hiyo ilitupiliwa mbali baada ya kuthibitika kuwa taratibu za
ufunguaji kesi zimefuatwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka kilikuwepo na
Hakimu Msaraka Ame Pinja, alikionyesha na kuwataka washitakiwa kujibu mashitaka
dhidi yao.
Hoja zilizoibuliwa na upande wa utetezi katika kesi hiyo, ni pamoja na ombi la
kutaka kupatiwa hati ya mashitaka pamoja na haki ya dhamana kwa washitakiwa hao
na jopo la mawakili watatu walielezea na kuvitaja vifungu na kuiomba Mahakama
hiyo kupunguza masharti ya dhamana.
Waliyataja masharti hayo kuwa ni washitakiwa kudhaminiwa na wafanyakazi wa
serikali, barua ya Sheha na kuangaliwa uwezo wa washitakiwa endapo watatikiwa
kutoa fedha taslimu kwa ajili ya dhamana wakati hali zao za kiuchumi sio nzuri.
Wakili wa washitakiwa hao, Suleiman Salum, alidai kuwa ni vigumu kwa
wafanyakazi wa serikali kujitokeza kuwawekea dhamana kutokana na woga na vile
vile ofisi nyingi za masheha hivi sasa zimefungwa kwa kuwakomoa ndugu na jamaa
wanaofuatilia kuwekewa dhamana jamaa zao wasifanikiwe kupata barua za
kuwachukulia dhamana.
Alidai kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa kwa kuwa ofisi za masheha zimefungwa na
wameacha magizo kuwa watakapouliziwa na mtu yeyote wajibiwe kuwa wamesafiri,
jambo ambalo alidai linawanyima wateja wake haki ya kupata dhamana.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Serikali, Maulid Ame Mohamed, alimtaka wakili huyo
kuacha kuzungumza nadharia na badala yake kuonyesha ushahidi kuhusu madai yake
ya dhamana ikiwamo masheha kufunga ofisi na watumishi wa umma kuogopa kuwawekea
jamaa zao dhamana kwa sababu kesi hiyo imefunguliwa na mwajiri wao ambaye ni
serikali.
“Hakuna chombo cha habari kilichowahi kuripoti kuwa ofisi za masheha
zimefungwa, hivyo ni vyema akaonyesha ushahidi wa yote anayodai mbele ya
mahakama,” alidai Mwanasheria huyo wa Serikali.
Baada ya mwanasheria huyo kutoa maelezo hayo, Wakili wa utetezi, Suleiman
Salum, alidai kuwa wateja wake wana haki ya kupatiwa dhamana kwa vile ni watu
wenye heshima na busara na hata polisi walikwenda wenyewe, lakini pia
wamesaidia kwa kiwango kikubwa kupatikana kwa hali ya amani na utulivu miongoni
mwa wafuasi wao.
Hoja hiyo ilisisitizwa na Abdallah Juma Mohamed, kwa kuileza mahakama hiyo kuwa
Ibara ya 12 (1) (6) (a), inaeleza haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji
kufanyiwa uamuzi wa Mahakama au chombo kingine kinachohusika.
Alidai kuwa ibara hiyo inasema mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya
kusikilizwa na pia haki ya kukata rufaa kutokana na maamuzi ya mahakama au
chombo kingine kinachohusika.
“Tulizo la washitakiwa sio mabomu wala virungu, bali ni dhamana kwa kuwa hivi
sasa utulivu unatokana na wao, ndio maana hali ya amani inaendelea na wananchi
wanafanya shughuli zao kama kawaida,” alidai.
Wakili huyo alidai kuwa washitakiwa hao, wana haki ya kupata dhamana kwa vile
kosa hilo sio la mauaji, uhaini au uhalifu wa kutumia silaha, bali
wanashitakiwa kwa makosa ya jinai ambayo bado Mahakama haijathibitisha kama
wametenda makosa hayo.
Baada ya mvutano uliochukua muda mrefu katika Mahakama hiyo iliyojaa askari na
wafuasi wa Uamsho waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo, Hakimu Msaraka Ame Pinja
alieleza kuwa suala la dhamana ni haki ya washitakiwa, lakini Mahakama haiwezi
kuamua kwa haraka, kunahitajika kutafakari kwa umakini kabla ya kutoa uamuzi.
Aliongeza kuwa vile vile si jambo la busara suala hilo la dhamana kuamuliwa
haraka haraka na pia kuchelewesha maamuzi, hivyo aliiahirisha kesi hiyo hadi
Oktoba 25, mwaka huu na kwamba mahakama itatoa uamuzi wa kuwapa dhamana
ama la.
Wakati wanafunzi waliporuhusiwa kuondoka shuleni, baadhi yao walikuwa
wakilalamikia vurugu za Uamsho zinazosababisha kukosekana kwa utulivu na
kushindwa kuendelea na masomo kutokana na kurudishwa nyumbani mara kwa mara
kutokana na vitendo hivyo.
”Tunamuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwachukulia
hatua wahusika wote wa vurugu, sisi tunakosa kuendelea na masomo, leo (jana)
tulikuwa tunafanya mitihani ya majiribio, lakini tumeshindwa kuendelea, baada
ya walimu kutuambia turudi nyumbani,” alisema mwanafunzi mmoja.
Mwanafunzi mwingine wa shule ya Mwanakwerekwe C aliyejitambulisha kwa jina la
Rahma, alisema watu wanaofanya vurugu na kuathiri masomo yao, hawataingia
peponi kwa kuwa vitendo hivyo vinamkera na kumchukiza Mwenyezi Mungu.
Chanzo:
Nipashe
0 comments:
Post a Comment