na Julius Konala, Songea
MKUU
wa Mkoa (RC) wa Ruvuma, Said Mwambungu, amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri
za wilaya na manispaa mkoani humo kuwawajibisha kwa kuwasimamisha kazi au
kuwafukuza maofisa watendaji wa vijiji na kata wazembe ambao watashindwa
kuwadhibiti watu wanaofanya uharibifu wa mazingira kwa kuchoma moto na kukata
miti ovyo.
Mwambungu
alitoa agizo hilo jana wakati akifungua kongamano la kuweka mikakati ya
kudhibiti moto hatarishi kwenye maeneo ya misitu mkoani humo lililoandaliwa na
kitengo cha Misitu Uenezi, Kanda ya Kusini.
Mkuu
huyo wa Mkoa (RC), alisema maofisa watendaji hao wengi wao wamekuwa
wakiwafumbia macho wananchi wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira na kwamba
vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa viumbe hai na uoto wa asili ambao ni
rasilimali ya taifa kwa vizazi vijavyo.
“Vitendo
hivi vya uharibifu wa misitu vimekidhiri sana hasa katika tarafa ya Madaba kwa
kazi ya kuendeleza biashara ya uchomaji wa mkaa kinyume na taratibu za uvunaji
wa misitu hiyo kwa kuwa kasi ya ukataji misitu haiendani na upandaji miti,”
alisema Mwambungu.
Aidha,
aliwaonya mabwana miti kuacha tabia ya kukaa ofisini kwa lengo la kutoa vibali
vya uvunaji wa misitu badala yake wazungukie vijijini kwa ajili kutoa elimu kwa
wananchi juu ya utunzaji wa mazingira.
Kwa
upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko, akifunga kongamano
hilo alisema katika kukabiliana na tatizo hilo ni vema kamati za mazingira
katika kata na vijiji zikapewa nguvu ili kupunguza kasi ya uharibifu huo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment