Home » » Mabishano yatawala kikao cha kupanga Bei ya korosho

Mabishano yatawala kikao cha kupanga Bei ya korosho



Ruvuma
Mkutano wa Wadau wa Korosho umetangaza bei ya korosho kwa msimu wa mwaka 2013/14 kwa Sh. 1,000 kwa kilo kwa daraja la kwanza na daraja la pili Sh. 800 baada ya wadau kubishana na wabunge.

Bei ilitangazwa rasmi kuanza kwa msimu wa ununuzi wa zao hilo kuanzia mwezi huu katika mkutano huo uliohudhuliwa na wadau hao wakiwamo wabunge wa mikoa ya  kusini .
Wadau hao walipinga bei hiyo na kupendekeza korosho kuuzwa kwa Sh, 1,200 na kupingwa vikali na wakulima.

Kikao hicho kilichowashirikisha wanasiasa hususani wabunge wakionekana kupigia debe bei ya Sh. 1,200, huku wakulima  wakihofia  endapo korosho itauzwa kwa bei hiyo huenda wakajikuta katika wakati mugumu kwa kushindwa kulipwa fedha zao kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita.

Mkulima wa korosho wa Kijiji cha Maundo Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, Abdul Chinemba, alisema bei iliyopitishwa mwaka jana imewasababishia baadhi yao kukosa malipo yao hadi sasa huku akishauri korosho kuuzwa kwa Sh.1,000, ambayo itamwezesha mkulima kulipwa fedha zake bila kukidai chama cha msingi.

Mkulima kutoka Wilaya ya Nanyumbu mkoani humo, Fatuma Chisanga, aliomba mkutano huo usiendeshwe kisiasa huku akitoa angalizo kutorudia makosa yaliyofanywa katika mkutano uliopita.

Awali akitangaza bei dira ya zao hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Juma, alisema kuwa bodi hiyo ilipendekeza korosho kuuzwa kwa Sh. 800 kwa kilo kwa daraja la kwanza na la pili Sh. 600.

Mbunge wa Tunduru, Mtutula Mohamed Mtutula, alimuomba  Mwenyekiti wa wadau hao, Hemed Mkali kuwachunguza  waliopendekeza bei dira hiyo.

“Mwenyekiti wewe ni mwanasiasa wa siku nyingi, naomba hawa watu waliopendekeza bei hii wachunguzwe kama kweli wanamapenzi ya dhati, nikisema hivi naamini hata wewe unaelewa kwa kuwa unatambua ninamaanisha kitu gani. Sina imani na hawa watu waliopitisha bei dira na wala sidhani kama wanatutakia mema, ” alisema Mtutula.

Mbunge wa Newala ambaye pia ni Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Geogre Mkuchika, alishauri mkutano huo kutopunguza bei hiyo huku akihofia endapo  mkutano huo utapitisha bei ya Sh. 1,000, utasababisha matatizo makubwa kwa wananchi wao.

Baada ya  vuta nikuvute hiyo, Mwenyekiti wa wadau alipata wakati mgumu na kupendekeza wadau kupiga kura ili kufahamu bei wanayohitaji katika msimu huu.

Baada ya kupigwa kura, wadau hao walipendekeza bei korosho kuuzwa kwa Sh. 1,000  hivyo wabunge kujikuta wakishindwa.

 
CHANZO: NIPASHE


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa