WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru
Kawambwa amekipongeza Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph, tawi la Songea, mkoani
Ruvuma, kwa kufundisha masomo ya sayansi kwa kuwa itapunguza uhaba wa wataalamu
wa kada hiyo.
Dk. Kawambwa alisema hayo mjini hapa jana wakati wa
mahafali ya nne ya chuo hicho yaliyohudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa,
serikali, wazazi wa wahitimu na wananchi mbalimbali.
Alieleza kuwa anathamini mchango unaotolewa na chuo
hicho kwa kuwa nchi yoyote haipati maendeleo bila wataalamu wa sayansi hivyo ameuomba
uongozi wa chuo hicho kuongeza udahili wa wanafunzi hao.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Tanzania, Dk.
Arul Raj, alimwomba waziri huyo kuangalia uwezekano wa serikali kutoa mikopo
kwa wanafunzi wa stashahada badala ya mikopo hiyo kutolewa kwa wanafunzi wa
shahada peke yake kwa vile baadhi yao wanashindwa kumudu gharama za masomo.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Joseph
Mkirikiti, aliwataka wazazi kuwahimiza vijana wao kujiunga na chuo hicho ili
wapate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kulifanya taifa lipige hatua ya
maendeleo tofauti na ilivyo sasa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chuo hicho Askofu
John Ndimbo wa Jimbo Katoliki Mbinga ameipongeza serikali kwa ushirikiano
katika ufanisi wa chuo hicho kwa madai kwamba bila ya kupata ushirikiano huo wasingefanikiwa.
Katika mahafali ya chuo hicho kilichoanzishwa mwaka
2004 wahitimu 96 wa masomo ya sayansi ya kompyuta walitunukiwa vyeti.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment