Home » » MAHAKAMA YAAMURU MAITI IFUKULIWE

MAHAKAMA YAAMURU MAITI IFUKULIWE

MGOGORO wakugombea Mwili wa mzee Cleophas Senga (80) Mkazi wa Chanji, Wilayani hapa, mkoani Rukwa, umechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi kufukua maiti ya mzee huyo kwa amri ya Mahakama na kuihifadhi katika hospitali ya hospitali ya Mkoa wa Rukwa.
Maiti hiyo ilifukuliwa jana, majira ya saa 4:40 asubuhi katika makaburi ya Mandela, huku baadhi ya mitaa mjini hapa ikisimamisha huduma za biashara kwa muda wakati umati wa watu ukiwa umejitokeza kushuhudia tukio hilo.
Baadhi ya akinamama waliojitokeza kushuhudia zoezi la ufukuaji wa maiti hiyo waliangua kilio baada ya kuona maiti ikitolewa kaburini na kuingizwa katika gari la polisi aina ya Toyota Landcruiser lenye namba za usajili PT 1275.
Akiongea na mwandishi wa habari, mdogo wa marehemu, Dominiki Senga, alisema mgogoro huo umetokana na mke wanne wa marehemu huyo.
“Wakati marehemu alipostaafu kazi ya udaktari alijenga nyumba Chanji na kufungua duka la dawa akawa anaishi na baadhi ya watoto wa mke mkubwa ambaye nae alikuwa ameshaolewa na mume mwingine na kuwaacha watoto kwa baba yao,”alisema.
Dominiki alisema marehemu alianza kuumwa miezi mitatu iliyopita ndipo kabla mauti hayajamkuta.
Alisema tangu mzee amefariki Novemba 7, mwaka huu wamekuwa wakivutana ambapo mke mdogo wa marehemu na mtoto wake wa kiume wanataka wao ndio wamzike marehemu kwa madai kuwa walikuwa wakimuuguza na wadogo zake na wanandugu pamoja na familia ya mke mkubwa wakitaka ukoo ukamzike marehemu kwa taratibu za kiukoo.
Mvutano huo uliwafikisha wanandugu mahakamani kuomba msaada wa kisheria juu ya nani mwenye haki ya kumzika marehemu.
“Kinachoshangaza tukiwa mahakamani mke mdogo wa marehemu na mwanae anayeitwa Cleophas Senga waliuchukua mwili wa marehemu mochwari na kwenda kuzika katika makaburi ya mandela mjini,”alisema.
Alisema waliamua kumueleza hakimu ndipo akatoa amri ya kufukua mwili wa marehemu na kuuhifadhi mpaka Mahakama itakapotoa uamuzi juu nani anapaswa kumzika mzee huyo.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa