Home » » MAJEMBE WAILALAMIKIA MANISPAA YA SONGEA

MAJEMBE WAILALAMIKIA MANISPAA YA SONGEA

KAMPUNI ya Majembe Auction Mart imeilalamikia halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kwamba haijatoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya ulipaji wa ushuru (Service Levy), kabla kampuni hiyo haijaanza kazi ya ukusanyaji.
Majembe Auction Mart imeingia mkataba na manispaa hiyo kuwa wakala wake wa ukusanyaji ushuru.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Majembe Auction Mart Nyanda za Juu Kusini, Nelson Mwasomola, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, baada ya wafanyabiashara wa manispaa ya Songea kuituhumu kampuni hiyo kuwa wanatumia nguvu katika ukusanyaji wa ushuru ambao wenyewe hawajapewa elimu juu ya ulipaji huo.
Mwasomola, alisema kuwa wafanyabiashara wana haki ya kulalamika, kwa sababu halmashauri ilitakiwa iitishe mkutano wa kuwatambulisha kabla ya kuanza kazi jambo ambalo halijafanywa tangu Julai Mosi mwaka huu waliposhinda zabuni hiyo.
Aliongeza kuwa, kitendo cha kutokutoa elimu kwa wakati kimesababisha Majembe kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kukataa kulipa ushuru, jambo linalosababisha malumbano kati ya wafanyabiashara na vijana wa kampuni hiyo.
"Sisi tuliiandikia barua halmashauri yenye kumbukumbu namba MAM/MNS/GC/10 ya tarehe 17 mwezi wa kumi mwaka huu, tukiitaka manispaa iitishe mkutano wa wafanyabiashara itutambulishe kwao na pia iwaelimishe juu ya sheria mpya ya ushuru wa ‘Service Levy’ ambao ulikuwa unatozwa kwa makampuni tu,” alisema.
Alifafanua kuwa, baada ya halmashauri kushindwa kutoa elimu hiyo wameanza kubandika matangazo ya ufafanuzi na kuwaelimisha zaidi wafanyabiashara na kwamba, hadi sasa hawajaanza rasmi kukusanya ushuru wakisubiri zoezi hilo kukamilika.
Aidha, alisema wamepewa orodha ya wafanyabiashara 2,836 na viwango wanavyotakiwa kulipa, ambako nusu yao imebainika kuwa hawana leseni za biashara wala vibanda vyao havina namba, jambo ambalo linawafanya wakwepe kulipa ushuru.
Hata hivyo, alisema ushuru unaolalamikiwa ni mdogo ambao mfanyabiashara anatakiwa kulipa kati ya sh 300 hadi 500 kwa siku na wengine wanalipa senti 50 kwa siku na kwamba, baadhi yao hawana uwazi katika biashara zao hali inayosababisha halmashauri kukosa mapato.
Wafanyabiashara hivi karibuni waliilalamikia kampuni hiyo wakati wa mkutano wao uliofanyika ukumbi wa Familia Bombambili kuwa, kampuni hiyo inatumia nguvu katika ukusanyaji wa ushuru, hali inayosababisha ugomvi wa kutokuelewana.
Inadaiwa kuwa Lazaro Mahenge, muuzaji katika duka moja eneo la Sovi hoteli alipigwa kwa kile kilichoelezwa alikataa kulipa ushuru.
Akijibu tuhuma hizo, Mwasomola alikataa kufanya tukio hilo, isipokuwa kijana huyo alikuwa anamshawishi mmoja wa wafanyabiashara aliyekuwa anaelimishwa juu ya ulipaji wa ushuru kuwa asikubali kuzungumza na watoza ushuru.


Mwasomola, alidai kuwa alichaniwa nyaraka za serikali hivyo katika harakati za kutaka kuziokoa, alimsukuma na sio kumpiga.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa