Home » » CCM YATAKA MAGUFULI AUNGWE MKONO.

CCM YATAKA MAGUFULI AUNGWE MKONO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais Dk. John Magufuli.
Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma kimewataka wanachama wake kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli, katika kupambana na ufisadi na kuwabana wakwepa kodi.
 
Rai hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho, wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi, wakiwamo wanachama wa chama hicho kwenye maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM, yaliyofanyika katika kata ya Subira, mjini hapa. 
 
Mwisho alisema kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk. Magufuli, amesaidia kwa kiasi kikubwa kurudisha imani kwa Watanzania na kuifanya CCM kupendwa na kuwa na nguvu zaidi.
 
“Inashangaza kuona baadhi ya wanachama ambao waligombea nafasi mbalimbali za uongozi kipindi cha uchaguzi mkuu mwaka jana kwa bahati mbaya majina yao hayakupitishwa kwenye kura za maoni, wamekuwa mstari wa mbele katika kuikosoa serikali. Hiyo inaonyesha walivyo dhaifu na wachanga kisiasa,” alisema.
 
Kutokana na hali hiyo, alitoa onyo kali kwa wagombea hao walioshindwa na kuendeleza makundi, migogoro na kuwa mstari wa mbele katika kupinga na kukwamisha shughuli za maendeleo.
 
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Taqnzania (UWT), Kuruthum Mhagama na katibu wake, Chiku Masanja, waliwashukuru wanawake kwa kuichagua na kuipa ushindi CCM.
 
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Juma Mpeli, alisema ajenda ya uchaguzi imekwisha kilichobaki ni chama kuisimamia serikali katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ikiwamo kuhakikisha mikopo inatolewa kwa makundi ya vijana na wanawake, kufutwa kwa ushuru mdogo mdogo, kushughulikia madai ya watumishi na kuimarisha chama katika ngazi zote.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa