Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HALMASHAURI ya Wilaya Kilwa imeagiza tani 90 za mahindi mkoani Ruvuma kwa ajili ya kaya zilizoathiriwa na mafuriko.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, Twaib Mbasha aliyasema
hayo alipozungumza na wajumbe wa Baraza la Madiwani lililofanyika jana.
Alisema halmashauri imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na tatizo hilo.
“Gari liko njiani likitokea mkoani Ruvuma linalosafirisha mahindi kuletwa wilayani hapa,” alisema.
Mbasha alisema ni vigumu kuwaacha wananchi hivi hivi bila ya kutoa msaada kwao, kwani hawakutegemea kama wangepatwa na mafuriko.
Alisema juhudi nyingine zilizochukuliwa ni kuwasiliana na ofisi ya
Mkuu wa Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu ili kupata
vyakula, dawa na huduma nyinginezo wanazohitaji wananchi hao.
Madiwani walisema hali si nzuri kwa kata zote, zilizopata mafuriko
mwezi uliopita, kwani zinahitaji chakula na kuna hatari ya kutokea
magonjwa ya milupuko.
Diwani wa Nanjilinji, Ally Yusufu alisema ekari 3,875 za mashamba ziliathiriwa na mafuriko ya Januari 22 hadi 26 mwaka huu.
Mazao ya chakula yaliyoathiriwa kwenye ekari hizo ni ekari 1,675 za
mahindi, 207 mpunga, ekari 88 mtama, 144.5 muhogo, 1755 ufuta na ekari
tatu za migomba.
Alisema kaya zilizoathirika ni 771 zenye watu 3,084. Watu hao hawana
mahala pa kuishi na sasa wanaishi kwa majirani, marafiki, ndugu na
jamaa.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment