Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAKULIMA wa mahindi wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, wameiomba
serikali kuongeza fedha kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
Kanda ya Songea ili wanunue mahindi mengi kwa msimu wa kilimo wa mwaka
2016/2017.
Wakulima hao walisema kutokana na hali ya hewa ya mwaka huu, hasa
kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika maeneo mkoani
Ruvuma, wana imani uzalishaji utakuwa mkubwa, ikilinganisha na msimu
uliopita.
Walisema ni vyema sasa serikali ikaanza kutafuta fedha za kutosha kwa
ajili ya maandalizi ya ununuzi wa mazao yao, kwa kuwa viongozi wa
serikali wanapita kwa wakulima na kuwahamasisha waongeze juhudi, jambo
lililoungwa mkono na wakulima wengi wa mkoa huo.
Mkazi wa kijiji cha Mlilayoyo, Joseph Ngonyani alisema wakulima wengi
wameitikia mwito wa viongozi unaotaka kuongeza uzalishaji wa mazao ya
chakula na biashara mashambani.
Hata hivyo, wasiwasi wao mkubwa ni kama serikali itanunua mazao yao hasa mahindi, zao ambalo ni tegemeo kubwa la kiuchumi.
Robet Mapunda wa kijiji cha Hanga alisema katika msimu wa 2013/2014
na 2015, wakulima wengi walilazimika kuuza mahindi yao kwa hasara
kutokana na utaratibu uliotumika wa NFRA kuwatumia mawakala kwenda
vijijini kununua mahindi kwa bei ndogo ya Sh 200 na wao kuizuia serikali
kwa Sh 500 hadi 550 kwa kilo.
Aliongeza kuwa kutokana na utaratibu huo, hakuna mkulima aliyenufaika
na kilimo, badala yake mawakala ndiyo walifaidika na kuwaacha wakulima
wengi wakiwa masikini.
Mapunda alisema wakulima walilazimika kuuza kwa bei ya ‘kutupa’ kwa
vile walishindwa kupata nafasi ya kupeleka moja kwa moja katika vituo
vilivyowekwa na NFRA, kwani wachache ndiyo waliopata nafasi hiyo jambo
lililowaumiza wakulima wa mahindi katika maeneo mbalimbali mkoani
Ruvuma.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment