MBINGA WATAKIWA KUCHANGAMKIA NHIF

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) amewataka wajasiriamali mkoani Ruvuma kuchangamkia mpango maalumu wa matibabu wa Kikoa waweze kuhudumiwa kwa gharama ya Sh 90,000 kwa mwaka.
Ofisa Mwandamizi wa mfuko huo mkoani Ruvuma, Calytus Mpangala aliwaambia wajasiriamali kutumia fursa hiyo adimu iliyotolewa na serikali kupitia NHIF wawe na uhakika wa kupata huduma bora za matibabu bila kutumia fedha ya mfukoni.
Mpangala alikuwa akizungumza na wateja wa Benki ya Wananchi Mbinga (MCB) katika Wilaya ya Nyasa waliojiunga katika vikundi vya ujasiriamali.
Alisema NHIF inahamasisha wananchi waliopo katika vikundi maalumu vya kiuchumi kama vile vikundi vya kilimo, mama lishe, migahawa na vinginevyo kuchangia Sh 96,000 ambayo Sh 78,600 inakwenda bima ya afya.
Zilizobaki ni kwa ajili ya shughuli za uendeshaji, riba na gharama za wafuatiliaji ambao ni MCB ambao ni mawakala wa NHIF.
Mpangala alisema, kiasi hicho cha fedha kitamwezesha mwana kikundi kupata matibabu kuanzia kwenye zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mkoa na hata hospitali ya rufaa popote nchini pale mwanachama wa mfuko huo atakapohitaji kutibiwa, isipokuwa baadhi ya gharama kama usafiri, malazi na chakula zitakuwa za mwanachama mwenyewe.
Chanzo Gazeti la Habari leo
 

Aflatoxin yahatarisha afya za walaji

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.




UELEWA mdogo kuhusu aina ya sumu inayozalishwa na kuvu waishio kwenye udongo au mimea na nafaka zilizooza, umesababisha vita dhidi yake nchini kutofanikiwa ipasavyo hivyo kuhatarisha afya za walaji.
Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Florens Turuka alisema sumu hiyo ijulikanayo kama aflatoxins, inasababisha usalama mdogo wa chakula na inahatarisha afya kwa walaji .
Akizungumza jijini Dar es Salaam kwenye mkutano uliozungumzia mapambano dhidi ya sumu hiyo , Turuka alisema sumu hiyo pia inaharibu biashara ya bidhaa za mazao hasa nafaka.
Pamoja na mambo mengine, wajumbe wa mkutano huo walijadili namna bora ya kuhusisha mapambano ya sumu hiyo kwenye miradi, programu na mipango mbalimbali.
Dk Turuka alisema, serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kuhakikisha kuwa juhudi zote za mapambano dhidi ya aflatoxin zinafanikiwa. Kwa mujibu wa Turuka, aflatoxin ni tatizo kubwa kwenye mfumo wa chakula nchini hususan kwenye mahindi, karanga na maziwa.
“Vyakula hivi ni kati ya vinavyoliwa kwa wingi hapa nchini,” alisema.
Alisema bado juhudi kubwa zinatakiwa kufanywa kuondokana na tatizo hilo ambalo huweza kusababisha saratani ya ini. Utafiti wa hivi karibuni umeonesha kuwa maeneo ya ukanda wa Mashariki na Magharibi nchini ndiyo yaliyoathirika zaidi na sumu hiyo katika mfumo wa vyakula.
Alishukuru Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa juhudi zake za kudhibiti sumu hiyo.
Pia alishuruku timu ya wadau wanaopambana na sumu hiyo (Partnership for Aflatoxin Control in Africa -PACA) kwa kuratibu mkutano huo. Licha ya Tanzania ambaye ni mwenyeji, mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe kutoka Gambia, Malawi, Senegal na Uganda.


Chanzo Gazeti la Habari leo

RUSHWA YA NGONO HUCHANGIA KURUDISHA NYUMA KASI YA MAENDELEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

RUSHWA YA NGONO HUCHANGIA KURUDISHA NYUMA KASI YA MAENDELEO

 Mratibu wa Asasi ya kuinua maendeleo ya Jamii na Kuhifadhi Mazingira (Ececo)Ndosho Hamisi akisisitiza jambo wakati akitoa mada juu ya madhara ya rushwa ya ngono iliyofanyika kijiji cha Duga wilayani Mkinga iliyokuwa na lengo la kuwapa uelewa jamii ya wasichana wa wafuigaji wa kimasaia iliyofanyika
 Baadhi ya wananchi wa Kata ya Duga Maforoni wakifuatilia mada mbalimbalio zilizokuwa zikiwasilishwa
 Katibu wa Asasi ya Kuinua Jamii na Kuhifadhi Mazingira (ECECO TANZANIA),Said Kamba akisisitiza jambo kwa washiriki wa semina hiyo
 Diwani wa Kata ya Duga Maforoni Ally Ally akizungumza katika semina hiyo

IMEELEZWA kuwa rushwa ya ngono imekuwa ni tishio hapa nchini hali inayochangia kurudisha nyuma kasi ya maendeleo kwani imekuwa ikipunguza demokrasia na utawala bora kwa watanzania jambo ambalo linapaswa kupigwa vita kwa vitendo.

Hayo yalisemwa juzi na Mratibu wa Asasi ya Kuinua Maendeleo ya Jamii na Kuhifadhi Mazingira (Ececo), Ndosho Hamisi wakati wa semina ya rushwa ya ngono iliyofanyika Kijiji cha Maforoni Kata ya Duga wilayani hapa na kufadhiliwa na Women Fund Tanzania  (WTF)iliyokuwa na lengo la kuwapa uelewa juu mambo hayo kwa wasichana na wanawake hasa wa jamii ya wafugaji wa kimasai.

Alisema kuwa tatizo hilo limekuwa likichukua kasi kwenye sekta nyingi na kusababisha kukandamiza haki za wanaostahili kuweza kupata fursa za kuweza kupata nafasi za kukuza uchumi wao na hivyo wengi wao kuishia katika hali duni.

  “Ukiangalia leo hii unaweza kutaka kitu Fulani mahali lakini kwa sababu hauna sifa ambazo zinapaswa kukipata basi yanaweza kutumika mazingira ambayo sio sahihi ili uweze kukipata kutokana na kumtimizia mahitaji yake mlengwa na hili limekuwa tatizo kubwa “Alisema.

 “Ni kosa kisheria mtu mwenye mamlaka kumpandisha cheo mfanyakazi wake kutokana na kuwepo kwa mazingira ya rushwa ya ngono kwa sababu inasababisha kupunguza ufanisi kazini na hivyo kushindwa kupiga hatua kubwa za kimaendeleo “Alisema.

Alisema jambo hilo limekuwa na madhara mengi kwa jamii ikiwemo kupata magonjwa makubwa ikiwemo ukimwi lakini pia uzalilishaji kitendo ambacho kinapelekea kushusha utendaji na kuchangia kurudisha nyuma maendeleo.

Awali akizungumza wakati akifungua semina hiyo, Diwani wa Kata ya Duga, Ally Mohamed aliipongeza asasi hiyo kwa kuona umuhimu kuwapatia mafunzo hayo ambayo yataweza kuwapa uelewa juu ya madhara ya rushwa ya ngono na kubadilika

“Unaweza kukuta wakati mwengine watoto wadogo wanazalilika kutokana na kutokujua madhara ya rushwa ya ngono hivyo semina hii itawafungua macho kuona namna ya kuweza kupiga vita vitendo hivyo “Alisema

‘Acheni shughuli za binadamu kwenye vyanzo vya maji’

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo, amepiga marufuku shughuli zote za kibinadamu kufanyika kandokando ya vyanzo vya maji kupunguza tatizo la uhaba wa maji ambalo limekumba eneo kubwa la wilaya hiyo.
Aidha Mwamengo, amezuia pia shughuli za kibinadamu ikiwamo kilimo katika milima jirani ya chanzo na mradi wa maji katika kijiji cha Kigonsera ambapo baadhi ya watu wamesababisha mradi wa maji katika kijiji hicho uliotumia kiasi kikubwa cha fedha kushindwa kufanya kazi.
Mwamengo alipiga marufuku shughuli hizo hivi karibuni wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho na kuziagiza mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinalinda vyanzo vyote vya maji kijijini hapo.
Pia aliwaagiza watendaji wa vijiji na kata, kuwasaka na kuwafikisha mahakamani watu wote waliosababisha mradi huo kushindwa kufanya kazi iliyokusudiwa licha ya serikali kutumia fedha nyingi kutekeleza mradi huo kuwaondolea wananchi kero hiyo ya muda mrefu.
Aliwataka watendaji hao, kuwashirikisha askari mgambo kufanya msako kabambe ambao utafanikisha kuwapata wahusika na pia kufanya doria ya mara kwa mara katika maeneo hayo muhimu kuzuia watu wachache wanaoharibu vyanzo hivyo.
“Kama watendaji mtashindwa kupata waharibifu hao wa vyanzo vya maji mimi mwenyewe kuanzia wiki ijayo nitaanza msako kuwatafuta watu ambao ni kikwazo katika mipango mingi ya maendeleo wilayani kwetu,” alisema Mwamengo.

Chanzo Gazeti la Habari Leo
 

Mbinga waukataa Mfuko wa Vidung’ata

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imeombwa kuufuta Mfuko wa Vidung’ata, unaohudumia wakulima wa kahawa wilayani humo.
Ombi hilo lilitolewa na wanachama wa Chama cha Ushirika wilayani Mbinga (MBIFACU).
Walisema hayo juzi katika mkutano wao kwa nyakati tofauti. Walisema mfuko huo umekuwa ukiwanufaisha baadhi ya watendaji waliopo serikalini na sio wakulima hao.
Kwamba makato ya fedha wanazokatwa katika kila msimu wa mavuno ya kahawa ni makubwa mno. Fedha hizo zililenga kununua dawa ya kuhudumia zao hilo, lakini cha kushangaza dawa hizo kwa ajili ya wakulima, zimekuwa haziwafikii. Lengo la kuunda Mfuko wa Vidung’ata ni kudhibiti wadudu wanaoshambulia mti wa kahawa, hasa katika kipindi cha masika.
Fedha wanazokatwa, Sh 50 kwa kila kilo moja ya kahawa mnadani Moshi, ilipaswa zikafanye kazi iliyolengwa na sio vinginevyo.
Walishauri waunde mfuko wa pembejeo za kilimo wao wenyewe na makato ya fedha zao, yaelekezwe huko; na si jambo hilo kushughulikiwa na watendaji wa serikali.
Mkulima wa kata ya Ngima, Wilson Kapinga, alisema wanaukataa mfuko huo kutokana na baadhi ya watendaji wa serikali, mabwana shamba, kukosa uaminifu wa kufikisha dawa kwa wakulima. Dawa hizo huishia mikononi mwao na kujinufaisha wao binafsi.
Kapinga alisema maofisa ugani hao, muda mwingi wamekuwa wakiishi mjini badala ya kuwa karibu na wakulima vijijini. Kitendo hicho kinawafanya washindwe kuwajibika ipasavyo, ikiwamo kuwafundisha wakulima utunzaji bora wa mazao yao shambani.
Mkulima mwingine wa kahawa, Peter Komba wa kata ya Myangayanga alisema umefika wakati watendaji hao wachukuliwe hatua za kinidhamu. Kwamba kutowajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi, liwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Mwenyekiti wa MBIFACU wilayani Mbinga, Stanley Lupogo aliunga mkono hoja hizo. Alitaka wakulima wa kahawa kuzalisha zao hilo kwa wingi na kwa ubora unaokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi.

Chanzo Gazeti la Habari Leo
 

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa