HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imeombwa kuufuta Mfuko
wa Vidung’ata, unaohudumia wakulima wa kahawa wilayani humo.
Ombi hilo lilitolewa na wanachama wa Chama cha Ushirika wilayani Mbinga (MBIFACU).
Walisema hayo juzi katika mkutano wao kwa nyakati tofauti. Walisema
mfuko huo umekuwa ukiwanufaisha baadhi ya watendaji waliopo serikalini
na sio wakulima hao.
Kwamba makato ya fedha wanazokatwa katika kila msimu wa mavuno ya
kahawa ni makubwa mno. Fedha hizo zililenga kununua dawa ya kuhudumia
zao hilo, lakini cha kushangaza dawa hizo kwa ajili ya wakulima,
zimekuwa haziwafikii. Lengo la kuunda Mfuko wa Vidung’ata ni kudhibiti
wadudu wanaoshambulia mti wa kahawa, hasa katika kipindi cha masika.
Fedha wanazokatwa, Sh 50 kwa kila kilo moja ya kahawa mnadani Moshi, ilipaswa zikafanye kazi iliyolengwa na sio vinginevyo.
Walishauri waunde mfuko wa pembejeo za kilimo wao wenyewe na makato
ya fedha zao, yaelekezwe huko; na si jambo hilo kushughulikiwa na
watendaji wa serikali.
Mkulima wa kata ya Ngima, Wilson Kapinga, alisema wanaukataa mfuko
huo kutokana na baadhi ya watendaji wa serikali, mabwana shamba, kukosa
uaminifu wa kufikisha dawa kwa wakulima. Dawa hizo huishia mikononi mwao
na kujinufaisha wao binafsi.
Kapinga alisema maofisa ugani hao, muda mwingi wamekuwa wakiishi
mjini badala ya kuwa karibu na wakulima vijijini. Kitendo hicho
kinawafanya washindwe kuwajibika ipasavyo, ikiwamo kuwafundisha wakulima
utunzaji bora wa mazao yao shambani.
Mkulima mwingine wa kahawa, Peter Komba wa kata ya Myangayanga
alisema umefika wakati watendaji hao wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Kwamba kutowajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi, liwe fundisho
kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Mwenyekiti wa MBIFACU wilayani Mbinga, Stanley Lupogo aliunga mkono
hoja hizo. Alitaka wakulima wa kahawa kuzalisha zao hilo kwa wingi na
kwa ubora unaokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi.
Chanzo Gazeti la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment