MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance
Mwamengo, amepiga marufuku shughuli zote za kibinadamu kufanyika
kandokando ya vyanzo vya maji kupunguza tatizo la uhaba wa maji ambalo
limekumba eneo kubwa la wilaya hiyo.
Aidha Mwamengo, amezuia pia shughuli za kibinadamu ikiwamo kilimo
katika milima jirani ya chanzo na mradi wa maji katika kijiji cha
Kigonsera ambapo baadhi ya watu wamesababisha mradi wa maji katika
kijiji hicho uliotumia kiasi kikubwa cha fedha kushindwa kufanya kazi.
Mwamengo alipiga marufuku shughuli hizo hivi karibuni wakati
akizungumza na wananchi wa kijiji hicho na kuziagiza mamlaka
zinazohusika kuhakikisha zinalinda vyanzo vyote vya maji kijijini hapo.
Pia aliwaagiza watendaji wa vijiji na kata, kuwasaka na kuwafikisha
mahakamani watu wote waliosababisha mradi huo kushindwa kufanya kazi
iliyokusudiwa licha ya serikali kutumia fedha nyingi kutekeleza mradi
huo kuwaondolea wananchi kero hiyo ya muda mrefu.
Aliwataka watendaji hao, kuwashirikisha askari mgambo kufanya msako
kabambe ambao utafanikisha kuwapata wahusika na pia kufanya doria ya
mara kwa mara katika maeneo hayo muhimu kuzuia watu wachache wanaoharibu
vyanzo hivyo.
“Kama watendaji mtashindwa kupata waharibifu hao wa vyanzo vya maji
mimi mwenyewe kuanzia wiki ijayo nitaanza msako kuwatafuta watu ambao ni
kikwazo katika mipango mingi ya maendeleo wilayani kwetu,” alisema
Mwamengo.
Chanzo Gazeti la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment