UELEWA mdogo kuhusu aina ya sumu inayozalishwa na kuvu waishio kwenye
udongo au mimea na nafaka zilizooza, umesababisha vita dhidi yake
nchini kutofanikiwa ipasavyo hivyo kuhatarisha afya za walaji.
Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Florens Turuka
alisema sumu hiyo ijulikanayo kama aflatoxins, inasababisha usalama
mdogo wa chakula na inahatarisha afya kwa walaji .
Akizungumza jijini Dar es Salaam kwenye mkutano uliozungumzia
mapambano dhidi ya sumu hiyo , Turuka alisema sumu hiyo pia inaharibu
biashara ya bidhaa za mazao hasa nafaka.
Pamoja na mambo mengine, wajumbe wa mkutano huo walijadili namna bora
ya kuhusisha mapambano ya sumu hiyo kwenye miradi, programu na mipango
mbalimbali.
Dk Turuka alisema, serikali itatoa kila aina ya ushirikiano
kuhakikisha kuwa juhudi zote za mapambano dhidi ya aflatoxin
zinafanikiwa. Kwa mujibu wa Turuka, aflatoxin ni tatizo kubwa kwenye
mfumo wa chakula nchini hususan kwenye mahindi, karanga na maziwa.
“Vyakula hivi ni kati ya vinavyoliwa kwa wingi hapa nchini,” alisema.
Alisema bado juhudi kubwa zinatakiwa kufanywa kuondokana na tatizo
hilo ambalo huweza kusababisha saratani ya ini. Utafiti wa hivi karibuni
umeonesha kuwa maeneo ya ukanda wa Mashariki na Magharibi nchini ndiyo
yaliyoathirika zaidi na sumu hiyo katika mfumo wa vyakula.
Alishukuru Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa juhudi zake za kudhibiti sumu hiyo.
Pia alishuruku timu ya wadau wanaopambana na sumu hiyo (Partnership
for Aflatoxin Control in Africa -PACA) kwa kuratibu mkutano huo. Licha
ya Tanzania ambaye ni mwenyeji, mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe
kutoka Gambia, Malawi, Senegal na Uganda.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment