SERIKALI kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda
ya Songea, imelazimika kuongeza bei ya kununulia mahindi ya wakulima
mkoani Ruvuma kutokana na ushindani mkubwa, baada ya kuwepo kwa wanunuzi
binafsi wengi wanaonunua mahindi kwa bei kubwa.
Kutokana na ushindani uliopo, NFRA kuanzia Novemba 7, mwaka huu
ililazimika kupandisha bei ya kununua mahindi hadi kufikia Sh 580 kwa
maeneo ya vijijini na Sh 600 kwa watakaoleta katika kituo kikuu cha
Ruhuwiko mjini Songea.
Hayo yalisemwa na Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Majuto
Chabruma, alipozungumzia kazi ya ununuzi wa mahindi katika vituo
mbalimbali vilivyotengwa katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma.
Chabruma alisema mwaka huu Serikali ilituma Sh bilioni 6.4 kwa ajili
ya kununua mahindi tani 12,000 za awali huku malengo ikiwa ni kununua
tani 22,000 na bado wanaendelea na kazi hiyo japo hawajafikia lengo lao.
Hata hivyo, kuna ushindani mkubwa wa soko kutoka kwa watu na kampuni
binafsi ambazo zimeingia mkoani Ruvuma kwa ajili ya kununua mahindi.
Chabruma alisema serikali imeona ni vyema kuongeza bei ya mahindi ili
kukabiliana na ushindani wa bei iliyopo sokoni, jambo lililosababisha
kupungua kwa mahindi.
Alisema bado wakala unaendelea kununua ziada ya mahindi ambayo bado
ipo kwa wakulima na wauzaji wengine katika kituo cha Ruhuwiko Songea na
amewashauri wakulima mkoani Ruvuma ambao bado wana mahindi nyumbani
kuyauza kwa wakala huo.
Alisema hatua hiyo itaiwezesha serikali kufikia malengo yake na nchi
kwa jumla iwe na akiba na kuwezesha kutoa nafaka hiyo pindi
kutakapojitokeza uhaba wa chakula nchini.
Aidha, Chabruma aliwakumbusha wakulima mkoani Ruvuma kuanza
maandalizi ya msimu mpya wa kilimo wakati huu kwani mvua za kwanza
zimeshaanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, pamoja na
baadhi ya mikoa mingine nchini.
0 comments:
Post a Comment