Home » » Elimu yaondoa Presha kwa Wazazi Mwaka mmoja wa Serikali ya JPM

Elimu yaondoa Presha kwa Wazazi Mwaka mmoja wa Serikali ya JPM

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Bijampola ni kijana aliyekuwa na bidii sana shuleni, ndoto yake ilikuwa awe rubani pindi akimaliza masomo yake ya taaluma hiyo. Kwa bahati mbaya kwa kijana huyo, wazazi wake walikosa ada ya kumsomesha, hivyo akaishia darasa la nne na ndoto yake ikaishia hapo, kwa sasa ni mtoto wa mitaani, inasikitisha. Je Bijampola angekuwa anasoma kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano ndoto yake ingezimika au ingetimia! Bila shaka ingetimia kwani Serikali hii imeamua kutoa Elimu ya Msingi bure.
Kati ya mambo ya kupongezwa na kuungwa mkono ni hili suala la ELIMU BURE. Hakika Rais John Pombe Joseph Magufuli na Serikali yake wanawajali wananchi na hasa wa kipato cha chini ambao ndio wengi. Hili nalisema bila kificho kwani kutoa elimu kuanzia awali, msingi hadi sekondari ni jambo la kushukuru sana na litafanya vipaji vingi viweze kuibukka kwani wazazi hawatashindwa kuwapeleka watoto wao shule kwa kisingizio cha kukosa ada. Hongera Mzee wa Hapa Kazi Tu.
Kwa msingi huu au mfumo huu ndoto za akina Bijampola haziwezi kufa tena ni lazima zitimie. Ni dhahiri kwamba watoto wengi walikuwa wanazagaa mitaani pasipo kwenda shule kwa sababu wazazi wao hawakuwa na uwezo wa kuwasomesha. Baada ya elimu kutolewa bure tunaona watoto wa mitaani kupungua kwa kiwango kikubwa.
Katika hotuba ya Mhe. Rais ya kufungua Bunge la 11 mnamo Novemba 20, 2015 mjini Dodoma, Dkt. Magufuli alisema yafuatayo kuhusu elimu, “Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu.  Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi.  Aidha, tutahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k. Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, kama tulivyoahidi kwenye kampeni.  Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati.  Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga mkono Benki ya walimu ili iweze kuwanufaisha zaidi”.
Wahenga husema haja ya mja hunena, muungwana ni vitendo. Usemi huu umedhihirika na Serikali ya Awamu ya Tano kutekeleza kwa vitendo yale wanayoahidi ikiwemo hili la elimu bure.
Ni ukweli usiopingika kuwa kila mwenye kuthamini utu wa Mtanzania ni lazima akubaliane na kitendo cha kiungwana kilichofanya na Serikali ya Magufuli kama Mhe. Mwenyewe anavyoinadi cha kutoa elimu bure.
Ukweli huu unadhihirishwa na Mkazi wa Mbweni ambaye ni mzazi wa watoto wawili, Bi Pelagia Mpanda anayetoa ya moyoni kuhusu elimu bure. “ Kwa kweli ninamshukuru sana Mhe. John Pombe Magufuli kwa kutoa elimu bure kwa watoto wetu, mimi nina watoto mapacha ambao nimewasomesha kwa taabu sana kuanzia chekechea hadi darasa la saba. Mamilioni ya pesa yamenitoka na si kwamba nilikuwa tajiri la hasha nimekuwa nikikopa huku na kule na fedha nyingine nikipata kwenye shughuli za ujasiriamali, lakini cha moto nilikiona.” Ameendelea kusema, “Nilivyosikia Elimu inatolewa bure hadi sekondari nilishukuru sana nikashauriana na mume wangu watoto wetu tukawapeleka sekondari ya serikali ambapo wanafanya vizuri, kwa kweli nasema Magufuli umetujali sisi watu wa hali ya chini na Mungu akulinde uendelee kutuongoza na kutusaidia,”
Mzazi huyu anaendela kusema kwa sasa hapa presha na anasomesha watoto wake kwa raha na fedha anayoipata anaielekeza kwenye miradi mingine ya maendeleo. Amemwomba Mhe. Rais atupie jicho hata kwenye shule binafsi wapunguze viwango vya ada ili wale ambao bado wanasomeshja watoto wao katika shule hizo waweze nao kupata unafuu.
Elimu bure imegusa watu wengi na kuwafurahisha, hapa Mratibu Elimu Kata ya Keko, Bi Happines Elias jijini Dar es Salaam naye anasema haya kuhusu Elimu Bure, “Kwa kweli suala la Elimu bure nimelipokea kwa mikono miwili, mimi kama mwalimu najua jinsi ambavyo wazazi wamekuwa wakiangahika na michango mbali mbali kwa ajili ya watoto wao shuleni, lakini baada ya vitu hivi kuondolewa wazazi na watoto wan amani na watoto wanafanya vizuri darasani kwa sasa kwani hawana wasi wasi wa kufukuzwa.”
Mratibu huyu ameongeza kusaema kuwa anaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kujali elimu na hasa baada ya kuondoa ada haikuishia hapo bali imetoa madawati kwa kila shule, watoto hawakai chini tena. Ameongeza kuwa yeye kipindi anafundisha aliwahi kudondoka darasani wakati akipitapita katikati ya wanafunzi katika harakati za kukwepa kuwakanyaga akadondoka chini. Hivyo kwa sasa anasema adha hiyo haipo tena na anataraji ata viwango vya ufaulu vitaongezeka kwani mazingira ya kusomea yameboreshwa.
Kuhusu furaha ya Elimu bure, binti Mariam Yahaya, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Bunju Sekondari yeye anasema suala la Elimu bure amelifurahia sana kwani baada ya kumaliza  darasa la saba hakuwa na uhakika wa kuendelea na masomo ya sekondari kwani wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumlipia ada. Hivyo anasema, “Kwa kweli nimeruha sana kuwa Serikali inatoa elimu bure, hivyo nina hakika nitaendelea na masomo yangu bila wasi wasi.”

Picha ya Wanafunzi wakiwa Darasani


Naye   Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ambaye ndiye msimamizi wa shule za msingi na sekondari nchini anafafanua jinsi serikali ilivyojipanga kugharamia elimu ya msingi, “SERIKALI inapeleka Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kugharimia elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.”
Simbachawene anabainisha kuwa katika mpango huo, Serikali itagharimia gharama zote za  mtihani wa kidato cha nne kwa wanafunzi wote, tofauti na miaka yote ambapo wanafunzi hutozwa gharama za mitihani. Anasema fedha hizo zitatolewa moja kwa moja na Serikali kupia  Baraza la Mitihani (NECTA).
“Majukumu ya Serikali kuhusu utoaji elimu bila malipo yameelezwa katika waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2015, Serikali itabeba jukumu hili. Kutokana na kuwabana mafisadi tumeweza kupata fedha za kutosha,”anasisitiza Simbachawene.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali inatoa ruzuku ya uendeshaji wa shule Sh 10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh 25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kila mwaka.
Simbachawene anaongeza kuwa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya fidia ya ada Sh 20,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya kutwa na Sh 70,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka.

Ama kweli Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha dhamira ya dhati ya kumkomboa mwanachi hasa wa kipato cha chini. Elimu Kwanza na maendeleo yanafuata. Hii inadhihirisha kuwa Serikali hii imezidi kutambua kuwa Elimu ni Ufunguo wa Maisha na ndio maana suala la elimu limepewa kipaumbele na kuingizwa kwenye mradi wa matokeo makubwa sasa (BRN)
Ni mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ambapo mengi mazuri yameonekana katika Elimu hasa ili lililowaondolea wazazi wengi adha ya mikopo ili wawapelek watoto wao shule. Heko JPM na Falsafa yako ya Hapa Kazi Tu imedhihirika kwa vitendo.
MWISHO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa