Na.Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Mhe. Dkt. Abdallah Possi ameiasa jamii
kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika shughuli zote za maendeleo ili
kusaidia kuwainua na kuondokana na dhana ya utegemezi na kuwakwamua
kiuchumi.
Dkt.Possi ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Wilaya za Mbinga, Songea Vijijini na Nyasa mkoani Ruvuma ambapo alitembelea Shule zenye kuhudumia watu wenye mahitaji maalum za Songea Boys, Luhira, Huruma na Kituo cha Kulelea wenye ulewavu cha Peramiho Disabled Persons Action (PEDIPA) na Kituo cha kulele wazee na wenye ukoma cha Nge Wilayani Nyasa.
Katika ziara hiyo Mhe.Possi alibaini changamoto
nyingi za watu wenye ulemavu na kuishauri jamii namna pekee ya kutatua
changamoto wanazokabiliana nazo ni jamii kuona umuhimu wa kuwashirikisha
watu hao katika mipango yote ya maendeleo.
“Halmashauri
ziandae mipango ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kuweza kushiriki
kikamilifu katika kujitafutia kipato na hii itasaidia kuondokana na hali
ya utegemezi na kuondoa mitazamo hasi juu ya watu wenye ulemavu kuwa
hawawezi” .Alisema Mhe.Possi.
Waziri
Possi alisisitiza kuwa ni lazima Halmashauri ziwe na ubunifu wa miradi
ya maendeleo itakayo walenga watu wenye ulemavu, “Ni vyema sasa kuwe na
jitihada za makusudi za kuunda miradi maalum kwa ajili ya kuwapa nafasi
za ushiriki ili kujitafutia vipato na kuyakabili mazingira yao,
ikumbukwe wakina mama waliachwa nyuma kwa muda mrefu ila baada ya kupaza
sauti zao tunaona sasa wanasikika hivyo hivyo iwe kwa watu wenye
ulemavu” Alisitiza Dkt.Possi.
Aidha
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyasa Dkt.Osca Albano alisisitiza
kuyapokea maelekezo yote ya Naibu Waziri Mhe.Possi kwa vitendo na
kumhakikishia kuwa Wilaya yao itakuwa mstari wa mbele katika
kulitekeleza hilo.
“Sisi
tunafanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Halmashauri hivyo ni vyema
tukalichukua hilo kuangalia namna tunavyoweza kuliweka katika mipango
yetu yote ya maendeleo ili kuwasaidia na kufikia lengo la serikali,”
alisema Dkt. Albano.
Nae
Katibu Tawala Wilaya ya Songea Bw. Edmund Siame aliomba halmashauri
zote ziwe zinatoa mrejesho mapema juu ya maagizo yanayotolewa na
viongozi wa juu huku Mwalimu Elswida Charles anayehudumia wanafunzi
wenye mahitaji maalum akimweleza Dkt. Possi kuwa watu wenye ulemavu
wanafarijika kutokana na jitihada anazofanya kuwainua watu wenye
ulemavu.
0 comments:
Post a Comment