Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akijibu swali Bungeni leo mjini Dodoma. |
Na Jacquiline Mrisho,
Dodoma.
Serikali
imetenga jumla ya shilingi bilioni 13.17 katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa
lengo la kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya mkoa wa Ruvuma ili
kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata maji safi na salama.
Kiasi
hicho cha fedha kimetajwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi
Gerson Lwenge alipokuwa akijibu swali la Mhe. Jacqueline Ngonyani (Viti Maalum)
lililohoji juu ya muda ambao Serikali itapeleka majisafi na salama katika Mkoa
huo.
Waziri
amesema kuwa Mpango wa Utekelezaji wa Maji Vijijini ulioanza mwaka 2006/ 2007, mkoa
wa Ruvuma ulipangiwa vijiji 80 na kati ya vijiji hivyo jumla ya vijiji 76
vilipata maji safi na salama.
“Asilimia
kubwa ya vijiji vilivyokuwa katika miradi hiyo vimepata maji safi na miradi
iliyobakia ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji hivyo kwa mwaka huu wa
fedha Ruvuma imetengewa kiasi cha fedha cha bilioni 13.17 ili changamoto ya
maji safi na salama katika mkoa huo iishe kabisa”, alisema Lwenge.
Ameongeza
kuwa Serikali imeendelea na mipango ya kuboresha huduma hizo katika miji ya
Songea, Mbinga, Namtumbo na Tunduru iliyopo katika mkoa huo ambapo kwa mji wa
Songea, mradi wa ukarabati wa chanzo cha maji cha mto Ruhila Darajani umekamilika
kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6.
Amefafanua
kuwa kukamilika kwa chanzo hicho mnamo mwezi Februari mwaka huu kumeongeza
kiasi cha upatikanaji wa maji wa jumla ya lita milioni 6 kwa siku ambapo wakazi
164,162 wamenufaika katika Manispaa hiyo.
Aidha,
Mhandisi Lwenge amebainisha kuwa kwa sasa Serikali imekamilisha usanifu wa kina
na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya uboreshaji wa huduma hizo katika
miji iliyopo katika mkoa huo.
“Serikali
inaendelea na jitihada ya kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
hiyo ambayo kwa mji wa Tunduru mradi utagharimu
Dola za Kimarekani milioni 7.3, mji wa Namtumbo ni Dola za Kimarekani
12.08, na Dola za Kimarekani 11.86 kwa ajili ya mji wa Mbinga”, alisema
Mhandisi Lwenge.
0 comments:
Post a Comment