Home » » HATUTAKUWA KIKWAZO CHA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI - NAIBU WAZIRI JUMA AWESO

HATUTAKUWA KIKWAZO CHA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI - NAIBU WAZIRI JUMA AWESO

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amesisitiza kuwa wizara yake haitakuwa kikwazo cha utekelezaji wa ahadi ya Rais, Dkt. John Magufuli ya kuwapatia wananchi majisafi na salama, bali itasimimamia utekelezaji wa miradi hiyo ipasavyo ili ikamilike kwa wakati na kuleta tija.
Aweso alizungumza hayo katika ziara yake ya kikazi aliyoianza katika mkoa wa Ruvuma, ambapo anakagua utekelezaji wa miradi ya maji katika wilaya zote mkoani humo.
‘‘Niwahakikishieni  wizara haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini, zaidi ya kuhakikisha miradi yote tunayoitekeleza inaleta tija na kumaliza kero ya maji kwa wananchi kulingana na maagizo ya Rais. Hivyo, lazima fedha zifike kwa wakati na zitumike kwa usahihi ili miradi yote ikamilike kwa wakati kulingana na mikataba,’’ alisema Naibu Waziri.
‘‘Ni jukumu langu kusimamia hilo na ninawaagiza watendaji wote wasimamie miradi yote hatua kwa hatua na watoe taarifa sahihi za maendeleo yake, ili sisi viongozi tujue changamoto na kutoa msukumo katika kufanikisha miradi hiyo  itakayokuwa na tija na thamani halisi ya fedha zinazotumika,’’alisisitiza Aweso.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji ametoa pongezi kwa SOUWASA kwa usimamizi mzuri wa miradi na hatua inazozichukua kwa nia ya kumaliza kero ya maji katika maeneo ya mji huo kama Midizini na Misufini ambayo yalikuwa na kero kubwa, lakini kwa sasa wananchi kukiri kupata huduma hiyo.
Katika ziara hiyo ameanza kwa kutembelea Wilaya ya Songea, ambapo ametembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Songea (SOUWASA) na kuweza kuzungumza na menejimenti yake, pamoja na watumishi.
Aidha, alitembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika wilaya hiyo ikiwemo eneo la mradi wa Bwawa la Luhira, mtambo wa kutibu na kusafishia maji wa Matogoro, mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi Songea.
Huduma ya maji kwa mji wa Songea kwa sasa ni asilimia 79, ambapo lita milioni 10.6 zinazalishwa kwa siku na mahitaji yakiwa ni lita milioni 14 kwa siku kwa wakazi wa mji huo. Upanuzi wa mradi wa maji wa Songea mjini unaondelea hivi sasa unategemea kuongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 90 kwa mji wa Songea.                                                                                                                                                                                                                                                                            
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso (wa kwanza kulia) akikagua sehemu ya mtambo wa kutibu wa kutibu na kusafisha maji wa Matogoro, pamoja na Meneja Ufundi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Songea (SOUWASA), Mhandisi John Kapinga.
 Mtambo wa kutibu na kusafisha maji wa Matogoro, Songea Mjini, mkoani Ruvuma
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (SOUWASA), Mhandisi Patrick Kibasa katika eneo la Misufini.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akishuka baada ya kukagua tanki la mradi wa Mtendewawa, wilayani Songea Mjini, mkoa wa Ruvuma.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa