na Stephano Chitete, Songea
WASAFIRISHAJI wa mizigo mkoani Ruvuma, wameitaka Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuona umuhimu wa kuwalipa deni lao la sh milioni 375 wanazozidai kwenye kitengo cha Taifa cha kuhifadhi mahindi kilichopo (SGR).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wasafirishaji hao ambao wameomba majina yao yahifadhiwa, walisema kuwa walikopwa kuyasafirisha mahindi hayo kwa ahadi kuwa fedha zao wangelipwa mara baada ya kumaliza kazi lakini hadi sasa hawajalipwa.
Walisema kuwa wafanyabiashara wengine waliikodisha serikali magodauni ili wahifadhi mahindi hayo kwa sababu yale ya kituo cha hifadhi kilichopo mjini hapa hayakuwa na uwezo wa kumdu mahindi yote.
Walisema kuwa walijitahidi kwa uaminifu mkubwa kufanya kazi hiyo ya kubeba mahindi kutoka kwenye maeneo ambayo miundombinu yake ni mibovu pasipo kujali vipuri vya magari na mafuta kupanda bei.
“Tuna mikopo ya benki na tunalipa kodi mbalimbali zikiwamo za Mamlaka ya Mapato (TRA) na kuchangia michango mbalimbali ya maendeleo mkoani hapa lakini tunashangazwa na kitendo cha serikali kutowathamini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani hapa, Mays Mkwembe, alisema kuwa wafanyabiashara wengi ambao waliikopesha serikali wamekuwa wakihangaika sana katika shughuli zao kutokana na kuidai fedha nyingi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko, alikiri kuwa wafanyabiashara wanaidai serikali kutokana na huduma waliyoitoa hivyo wasubiri kidogo kwani wanaandaa utaratibu wa kuwalipa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment