na Stephano Mango
BAADHI ya
wagonjwa wanaopata matibabu katika kituo cha afya cha Mjimwema kilichopo katika
Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, wamelalamikia uhaba mkubwa
wa dawa kituoni hapo na kusema waganga wanawashauri kununua dawa katika maduka
binafsi ambako zinauzwa kwa bei kubwa.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, wagonjwa hao walisema kwa muda mrefu wamekuwa
wakifika kituoni hapo kwa lengo la kutaka kupata matibabu, lakini badala yake
wamekuwa wakipewa ushauri wa waganga na kuandikiwa dawa ambazo kwenye kituo
hicho hazipo.
Mmoja wa
wagonjwa hao, alisema kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na kidonda, lakini
kila alipokwenda kwenye kituo hicho kwa ajili ya kusafisha alikuwa akishauriwa
akanunue dawa kwenye maduka ya watu binafsi, kwani kituo hicho kina uhaba wa
dawa kwa muda mrefu.
Mgonjwa
mwingine, alisema alipofika katika kituo hicho akiwa anasumbuliwa na malaria,
aliambiwa hakuna dawa na badala yake akaelekezwa akanunue kwenye maduka
binafsi.
“Jambo la
kushangaza hata Panadol nazo wanadai hawana. Tunaiomba serikali kupitia Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii kuona umuhimu wa kuihimiza Bohari ya Dawa (MSD)
kuhakikisha inasambaza dawa kwenye zahanati na vituo vya afya kwa wakati
muafaka, ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi,” alisema.
Kwa upande
wake, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Dk. Daniel Mtamakaya,
alipohojiwa kuhusiana na malalamiko ya wagonjwa hao, alikiri kwa muda mrefu
kituo chake hakijapokea dawa kutoka MSD, jambo ambalo amedai limekuwa likileta
usumbufu mkubwa kwa wagonjwa.
Dk. Mtamakaya
alisema wamekuwa wakilazimika kuwapa ushauri wa kitaalamu wagonjwa, lakini dawa
ni lazima waende wakanunue kwenye maduka ya watu binafsi, kwani tangu Juni
mwaka huu hawajapata dawa.
Naye Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Songea, Nachoa Zacharia, alisema kuna tatizo kubwa la uhaba
wa dawa kwenye zahanati zote za manispaa hiyo kikiwamo kituo cha afya cha
Mjimwema.
Chanzo: Taaanzania Daima
0 comments:
Post a Comment