HOT NEWS PICHA: WAZIRI NCHIMBI AFANYIWA VURUGU NA WANANCHI WAFUNGA BARABARA ‏

Wananchi wenye hasira wakifunga njia kwa kutumia vyuma vya kingo vya daraja kuzuia msafara wa Dkt.Emmael Nchimbi kupita wakati akienda kwenye mkutano wa hadhara ambao baadae ulifanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya kutwa ya matarawe iliyopo katika manispaa ya Songea (picha na Gideon Mwakanosya)
Diwani wa kata ya Matarawe (CCM) Makene  aliyesimama katikati akijaribu kuwatuliza wananchi wa kata hiyo ambao walifunga barabara itokayo mjini kwenda matarawe kwa zaidi ya masaa mawili wakimshinikiza mbunge wao Dkt. Nchimbi awasaidie kulipanua daraja ambalo wamedai kuwa limekuwa likisababisa ajari nyingi pamoja na vifo aliyesimama nyuma yake ni Dkt Nchimbi
 (Picha na Gideon Mwakanosya)

MSAFARA WA WAZIRI NCHIMBI WAPIGWA MAWE




MSAFARA wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, umepigwa mawe na wananchi waliojitokeza kuzungumzia kero ya daraja la Matarawe, ambalo linadaiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya watatu mwezi Oktoba mwaka huu.
Tukio hilo limetokea jana saa 10:00 jioni hadi saa 12:00,  ambapo wananchi hao wakiwa na hasira walifanya fujo wakimshinikiza Nchimbi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Songea  Mjini awasaidie kupanua daraja  hilo ambalo kwa  muda mrefu limesababisha kutokea kwa ajali za mara kwa mara katika eneo hilo.
Wananchi hao wa Kata ya Matarawe,  Manispaa ya Songea, wakiwamo waendesha  pikikipiki maarufu kwa jina la ‘yeboyebo’  walifunga barabara kwa  zaidi ya saa mbili huku wakifanya fujo za kung’oa kingo za daraja, kuweka  magogo na mawe  katikati ya daraja na kuchoma matairi moto  ili kumzuia kiongozi huyo asiweze kupita na atoe majibu ya kina juu ya daraja hilo.



Hatua hiyo ilililazimu Jeshi la Polisi kuwatawanya  wananchi hao kwa kuwafyatulia mabomu ya machozi ili kukabiliana na uharibifu pamoja na kuruhusu msafara huo uweze kupita.
Aidha, kufuatia vurugu hizo, Jeshi la Polisi liliweza kuwashikilia watu wanane.
Hata hivyo Dk. Nchimbi alilazimika kusimama na kushuka kwenye gari lake  akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa  chama na serikali akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Joseph Mkirikiti,  ambapo aliwapa pole kwa ajali zinazotokea huku akiwataka kuwa na subira  wakati ombi lao linashughulikiwa.
“Natoa pole sana kwa msiba na ajali ambazo zimetokea nimewasikia, na ninaahidi  nitawajengea daraja  hili, kama nimeweza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami bila maandamano wala kufungiwa barabara nitashindwa daraja?” alihoji.
Nchimbi alisema kuwa vitu hivyo vinavyozungumzika hakuna haja ya kufanya maandamano na kuwataka wananchi hao kuhudhuria mkutano wake kwa kuwa anajua ufinyu wa daraja hilo na ameahidi kulifanyia maboresho zaidi.
Naye Diwani wa kata hiyo,  James Makene, aliungana na kundi la wananchi hao na kumueleza Nchimbi kuwa  hiyo ni changamoto ambayo wakazi wake  wamekuwa wakilia kwa kipindi kirefu.
Aidha, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Deusdedit Msimeki, alisema kuwa kufuatia vurugu hizo tayari watu wanane wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa zaidi ili kuwabaini vinara wengine waliosababisha  fujo hizo.
TANZANIA DAIMA

Nchimbi apokelewa na malalamiko ya rushwa Ruvuma

Wananchi wa Manispaa ya Songea wamemlalamikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Dr. Emmanuel John Nchimbi kuhusu vitendo vya Rushwa vinavyofanywa na Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma.

Wananchi wa Manispaa ya Songea wamesema wanapokuwa na Matatizo ya kufikishana Polisi na wao wanapokubaliana kufuta kesi badala yake Polisi huomba Rushwa ili kesi ifutwe.

Waziri wa Mambo ya Ndani Dr. Emmanuel Nchimbi akijibu hoja hiyo ya Asikali police kuomba rushwa ili kesi ifutwe amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikubaliani na vitendo vya Hujuma, mpaka sasa Serikali kwa mwaka 2013 imeshafukuza Askari police 117 waliobainika kuwa na Makosa.

Wananchi wakiwa katika Mkutano wa Hadhara Eneo la Mahenge Kata ya Mjini wameomba Serikali kudhibiti vitendo vinavyofanywa na Jeshi la Polisi. Pia walimlalamikia Waziri kuhusu Uchafu uliokithiri katika Manispaa ya Songea,

Waziri wa Mambo ya Ndani amesema  Manispaa Songea imeshaagiza Magari Mawili ambayo yatasaidia kupunguza kuzoa takataka zilizopo katika Maghuba.

MSAFARA WA WAZIRI WA MAENDELEO UVUVI NA MIFUGO WAPATA AJALI

Dereva wa Shirika la Umeme TANESCO Tawi la Songea, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kusababisha ajali katika Msafara wa Waziri wa Maendeleo Mifugo na  Uvuvi Dr David Mathayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsmeki ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Ajali ilyotokea kutoka Mbambabay – Songea na kusababisha watu 5 kujeruhiwa ambao walilazwa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.

Akimtaja Dereva anayeshikiliwa na Polisi amesema ni Ahamadi Hamisi 33 ambaye alikuwa akiendesha Gari lenye lenye No. za Usajili SU 37788  TOYOTA Hilax iliyoigonga gari no stk 9906 mali ya RAS Mkoa wa Ruvuma Akiwataja waandishi wa habari walio pata ajali na kulazwa ni   Joseph Mwambije, Lauf Mohamed, Lauf Mohamed, Cresensia Kapinga na Joicy Joliga na mwingine ni Abiria mmoja aliyekuwa kwenye Gari la TANESCO.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsmeki amesema Madereva wa Shirika la TANESCO  Mkoani Ruvuma pamoja na kupewa onyo wamekuwa wakiendelea kwanda kwa  mwendo kasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsmeki amesema Madereva wa Shirika la TANESCO ambao huendesha kwa kasi gari zao, mara nyingi wapitapo mitaani wamekuwa wakizomewa na Wananchi ikiwa ni ishara ya kupinga mwendo mkali lakini hata hivyo wao huishia kuongeza mwendo . 

Dereva Ahamad Hamis anayeshikiliwa na Polisi anahojiwa na upelelezi utakapokamilika atapelekwa Mahakamani.  

Waziri wa Maendeleo, uvuvi na Mifugo Dr. David Mathayo alikuwa Ziarani Mkoani Ruvuma kwa kutoa Majibu ya Utafiti juu Samaki waliokuwa wanakufa Ovyo katika Ziwa Nyasa Wilayani Nyasa na kugundua ilitokana na Uchafuzi wa Hali ya Hewa na siyo Sumu.

UNYAMA WA KUTISHAA

Mkazi wa mjini Songea, anadaiwa kujeruhiwa kwa mapanga na mtu anayedaiwa kuwa mumewe kisha kumuua shangazi wa mkewe. Mwanamke huyo, Agatha Honde (19), ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Mletele, eneo la Nonga Nonga, mjini humo, anadaiwa kucharangwa mapanga na mtu huyo. Mtuhumiwa huyo inadaiwa kuwa baada ya kitendo hicho, alimuua shangazi wa Agatha kwa kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake. Agatha alisema anajisikia maumivu makali yanatokana na majeraha akidai yametokana na kukatwakatwa na panga sehemu mbalimbali za mwili wake na mtuhumiwa kwa sababu za kimapenzi.
Agatha alisema mwenza wake huyo kutokana na sababu zisizojulikana, aliamua kuachana naye na kwenda kuishi kwa shangazi yake.
Lakini akasema mtuhumiwa alimfuata na kumjeruhi kabla ya kumuua shangazi yake (55).
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi, alisema baada ya mtuhumiwa huyo kufanya unyama huo, alikimbia na kwamba, Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta popote alipo kwa hatua za kisheria. CHANZO: NIPASHE

Wanakijiji wapigwa mabomu

Vurugu kubwa zimetokea katika kijiji cha Ntunduwalo, wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma na Jeshi la Polisi kulazimika kufyatua mabomu ya machozi baada ya wakazi wa kijiji hicho kufunga barabara kuzuia magari yaliyobeba makaa ya mawe yasipite wakishinikiza hadi walipwe fidia.

Tukio hilo lilitokea juzi asubuhi wakati magari hayo yaliyobeba makaa ya mawe kutoka mgodi wa Mngaka yalipofika katika kijiji hicho, wananchi walijipanga barabarani kuyazuia na kusababisha vurugu ambazo baadaye zilizimwa na polisi waliofika eneo la tukio.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deudedit Nsimike alisema kufuatia vurugu hizo, watu 20 wakiwamo Mwenyeviti wa serikali ya kijiji hicho na maofisa watendaji wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano zaidi.

Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Mwenyekiti wa serikali ya kijiji  cha  Ntunduwalo, John  Nyimbo  (36), Matrida Nchimbi (49) ambaye  ni Afisa Mtendaji wa kata ya Rwanda, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ntunduwalo, Joachim Ngaponda, Mwenyekiti wa kamati ya miradi ya kijiji hicho, Garusi Komba  (49 na John  Joachim Mahai  (45), mkazi wa kijiji cha Malindindo.

Kamanda Nsimike alisema wanakijiji hao waliyazuia magari hayo kwa lengo la kuishinikiza serikali iwalipe nyongeza ya fidia ambayo  wanadai kwa muda mrefu.

Alisema wananchi hao wanadai kuwa malipo waliyolipwa awali baada ya eneo lao kuchukuliwa na mwekezaji aliyenunua mgodi huo, walipunjwa wakati wanafanyiwa tathmini ya mali zao kutokana na serikali kutumia sheria ya zamani badala ya sasa.

 Aliongeza kuwa wananchi hao katika kufanikisha azma yao, waliwatanguliza wanawake na watoto mbele na kukaaa katikati ya barabara huku wakidai kuwa wamechoshwa na ahadi za serikali zisizotekelezeka.

Alisema kabla ya wananchi hao kutekeleza mkakati huo, Katibu Tawala Wilaya ya Mbinga, Idd Mponda, aliwasihi waondoe kizuizi ili magari yaendelee na kazi ya kusomba makaa ya mawe, lakini walikataa na kumweleza kuwa hawamuitaji kumuona yeye pamoja na watu wengine wala Mkuu wa wilaya hiyo bali wanachotaka walipwe fedha zao wanazodai na si vinginevyo.

Aidha, Kamanda Nsimeki alisema pamoja na polisi  kuwashikilia wanakijiji hao jana asubuhi vurugu  zilirejea tena na kwamba polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya  wanakijiji hao.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu, amesema kuwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Senyi Ngasa kukutana na wananchi hao wakati mgogoro huo ukitafutiwa ufumbuzi.

Wanakijiji hicho kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita wamekuwa wakiidai serikali sehemu ya fedha ya fidia ambayo hawakulipwa badala yake kampuni ya Tancol ilipewa kazi ya kuchimba madini hayo chini ya usimamizi wa NDC.
CHANZO: NIPASHE

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa